Saturday, March 16, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAIPONGEZA OFISI YA RAIS-UTUMISHI KWA KUJENGA MIFUMO YA TEHAMA


Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 16 Machi, 2024

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ameipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kubuni mifumo mbalimbali ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha utendaji kazi serikalini.

Dkt. Mhagama amesema hayo leo Machi 16, 2024 Jijini Dodoma wakati Kamati hiyo ilipotembelea Ofisi ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Sekretarieti ya Ajira na Tume ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kupokea taarifa ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hizo. 

Aidha, kwa niaba ya Kamati, Dkt. Mhagama ameipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia taasisi zake kwa kufanya kazi kubwa ya kubuni na kusanifu mifumo ambayo ni muhimu na yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini.

“Tulizoea kuona nchi za wenzetu zikibuni na kusanifu mifumo mahususi ya TEHAMA kwa maendeleo ya mataifa yao na wakati mwingine kutuuzia na sisi lakini leo tumesikia na kuona kwa macho yetu uwezo mkubwa wa vijana wetu wa ndani ya Serikali ambao wameunda mifumo muhimu kwa ajili ya Serikali yetu, hakika haya ni mapinduzi makubwa yatakayoleta ufanisi unaozingatia haki na wajibu Serikalini” alisema Dkt. Mhagama.

Kadhalika Dkt. Mhagama ameisisitiza Ofisi ya Rais-UTUMISHI kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA iliyopo na inayoendelea kubuniwa na kusanifiwa inakuwa endelevu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa umma kwa njia ya TEHAMA.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameishukuru Kamati hiyo kwa kupanga ziara hiyo muhimu na kutoa maelekezo ambayo yatafanyiwa kazi kwa haraka na kutoa mrejesho.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa mifumo yote ikiwemo HCMIS, PEPMIS HR Assessment na mifumo mingine inatumika kwa ufanisi ili kutatua changamoto mbalimbali za kiutumishi kwa wakati.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama akizungumza na Viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Watendaji wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Sekretarieti ya Ajira na Tume ya Utumishi wa Umma wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyolenga kupokea taarifa za Miradi inayotekelezwa na taasisi hizo, jijini Dodoma.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa neno la shukrani kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Sekretarieti ya Ajira na Tume ya Utumishi iliyolenga kupokea taarifa ya Miradi ya taasisi hizo jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi (kushoto) na Katibu wa Tume ya Utumishi, Bw. Mathew Kirama (kulia) wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kikazi ya kupokea taarifa ya Miradi ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Sekretarieti ya Ajira na Tume ya Utumishi iliyofanyika jijini Dodoma.


Kaimu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa Umma Bw. Innocent Bomani akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya taasisi hiyo jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango akiwasilisha taarifa za mfumo wa HCMIS kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Ofisi ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Sekretarieti ya Ajira na Tume ya Utumishi jijini Dodoma.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Wa kwanza kushoto) akijadili jambo na Watendaji wa Ofisi yake kabla ya kupokea msafara wa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria katika Ofisi za Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Jijini Dodoma.

 


 

No comments:

Post a Comment