Tuesday, March 12, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YARIDHISHWA NA UJENZI WA JENGO LA TAKUKURU

 Na. Veronica Mwafisi -Iringa

Tarehe 12 Machi, 2024

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama kwa niaba ya Wajumbe wa kamati hiyo ameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa -TAKUKURU kwa utendaji uliotukuka na unaozingatia misingi na maadili ya utumishi wa umma wakati wote.

Mhe. Mhagama amesema hayo tarehe 12 Machi, 2024 Mkoani Iringa wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Ameongeza kuwa, kamati hiyo imeona kwa macho na  imeridhika na utekelezaji wa mradi huo na haina budi kuipongeza Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora kwa usimamizi mzuri kwa TAKUKURU ambayo inatekeleza mradi huo na miradi mingine inayoendelea katika mikoa mbalimbali.

“TAKUKURU ni moja ya taasisi za umma ambayo inafanya vizuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo sisi kama kamati tumeridhishwa na utekelezaji hu una tunaomba mkandarasi asimamiwe vyema ili kazi ya ujenzi wa jengo hilo ikamilike kwa ufanisi na kwa wakati.

Aidha, Mhe. Mhagama amesema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mzalendo na mchapa kazi na anatafuta fedha kwa hali na mali kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wake, hivyo TAKUKURU ihakikishe inaendelea kudhibiti kwa ufanisi mianya ya rushwa nchini na hususani fedha za miradi ya maendeleo ili thamani ya fedha ionekane.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameishukuru Kamati kwa kupanga ziara hiyo muhimu ya kutembelea miradi ya Taasisi hiyo na miradi mingine katika ofisi yake ili kujionea utekelezaji unavyoendelea.

“Sisi kama Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa niaba ya Waziri Mhe. George Simbachawene tuko tayari kusikia, kuchukua na kutekeleza ushauri na maekelezo yenu na ya Bunge kwa ufanisi na kwa wakati” ameongeza Mhe. Kikwete.

Vilevile, Mhe, Kikwete amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za maendeleo kwa wakati na hivyo hakuna mradi wowote ambao umelala na ameihakikishia Kamati kukamilika kwa miradi yote kwa ufanisi na kwa wakati

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP. Salum Hamduni amesema ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja utakamilika mwezi Juni mwaka huu na utagharimu zaidi ya shilingi billioni 1.4 na fedha hizo ziemeshaletwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kazi inaendelea.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama akizungumza na watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mara baada ya kamati yake kukagua ujenzi wa jengo la taasisi hiyo linaloendelea kujengwa mkoani Iringa.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwaonyesha Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ramani ya jengo linaloendelea kujengwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kabla ya kukagua jengo hilo mkoani Iringa.

 

Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakielekea kukagua ujenzi wa jengo la ghorofa moja la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) linaloendelea kujengwa mkoani Iringa.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama akijadiliana jambo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati kamati hiyo ilipokuwa inakagua ujenzi wa jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) linaloendelea kujengwa Mkoani Iringa. Wengine ni wajumbe wa kamati hiyo na watumishi wa TAKUKURU.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa salamu za shukrani kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria mara baada kufanya ziara ya siku moja ya kukagua ujenzi wa jengo la TAKUKURU linaloendelea kujengwa Mkoani Iringa.


Muonekano wa Jengo la ghorofa moja la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU linaloendelea kujengwa mkoani Iringa ambalo linatarajiwa kukamalika mwezi Juni 2024



No comments:

Post a Comment