Na.
James K. Mwanamyoto – Chato
Tarehe
19 Disemba, 2020
Chuo cha Utumishi wa Umma
Tanzania (TPSC) kiko mbioni kujenga kampasi Wilayani Chato, Mkoani Geita
itakayotoa fursa ya mafunzo kwa Watumishi wa Umma na wananchi wa Kanda ya Ziwa.
Akikagua eneo litakalojengwa
Kampasi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika ameridhika na eneo lililotengwa
kwani ni rafiki kwa usalama na utoaji wa elimu.
Mhe. Mkuchika amesema, Kanda
ya Ziwa pekee ndiyo ilikuwa haijabahatika kuwa na Kampasi ya Chuo cha Utumishi
wa Umma, hivyo fursa hii ni muafaka na itakuwa na manufaa kwa Watumishi wa Umma
na wakazi wa eneo la Kanda hii.
Akizungumzia uamuzi wa
kujenga Kampasi hiyo Wilayani Chato, Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, Halmashauri
ya Wilaya ya Chato imetoa kiwanja hicho bure tofauti na maeneo mengine ya Kanda
ya Ziwa ambayo yangekigharimu Chuo fedha nyingi kununua kiwanja.
Mhe. Mkuchika ameishukuru
halmashauri kwa kutoa kiwanja na kumhimiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Chato kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa hati kwani Chuo kiko tayari kuanza
ujenzi mapema iwezekavyo.
Naye
Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel
Shindika amewathibitishia wakazi wa Kanda ya Ziwa kuwa, fedha za kuanza ujenzi
zimeshapatikana, hivyo kinachosubirikiwa ni hati.
“Tukikabidhiwa
hati ya kiwanja, tutaanza ujenzi wa madarasa mapema iwezekanavyo ili wakazi wa
Kanda ya Ziwa wanufaike na huduma zinazotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma
kama ilivyo katika Kanda zingine,” Dkt. Shindika amesisitiza.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe.
Medard Kalemani amemtaka Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo kuwasilisha maombi ya
kupatiwa umeme katika eneo hilo ili kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa kampasi
hiyo.
Mhe.
Kalemani ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kampasi
hiyo ambayo itatoa fursa ya mafunzo na ajira kwa wakaohitimu na kuongeza kuwa,
chuo kitajengwa eneo ambalo ni salama na kitalindwa kwa ushirikiano wa
wananchi.
Akizungumzia
eneo ambalo Chuo kitajengwa, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Mhe. Robert
Gabriel Luhumbi amesema, ujenzi wa kampasi hiyo ukikamilika, itakuwa ni chachu
ya maendeleo kutokana na muingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali watakaokuja
kupata mafunzo na utavutia uwekezaji.
Kampasi
ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato itakayojengwa eneo la Rubambangwe
lenye ekari 41.66 itahudumia Mikoa ya Geita, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Simiyu
na Mara.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt.
(Mst) Mhe. George Mkuchika akielezea mpango wa kujenga kampasi ya Chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Wilayani Chato, Mkoani Geita alipoenda kukagua
eneo ambalo Kampasi ya chuo hicho itajengwa. Kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo
la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani na Mtendaji Mkuu
na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika.
Mtendaji
Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika
akimuonyesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika mchoro wa Kampasi ya Chuo cha
Utumishi wa Umma Wilayani Chato inayotarajiwa kujengwa Wilayani humo. Wanaoshuhudia
ni Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard
Kalemani na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi.
Sehemu
ya kiwanja ambayo kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato
itajengwa. Wanaoonekana katika picha ni baadhi ya Viongozi na Watendaji wa
Serikali wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika.
Mtendaji
Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika akitoa
ufafanuzi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika kuhusu mchoro wa Kampasi ya Chuo
cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato utakavyokuwa. Miongoni mwa wanaoshuhudia ni
Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani
na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi.
Mbunge
wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani
akimuahidi Mhe. Mkuchika kuharakisha upatikanaji wa umeme katika eneo ambalo
kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato itajengwa.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt.
(Mst) Mhe. George Mkuchika na Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa
Nishati, Mhe. Medard Kalemani wakifurahia jambo mara baada ya kupata maelezo
ya ujenzi wa kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato inayotarajiwa kujengwa
hivi karibuni.