Na.
Antonia Mbwambo-Dodoma.
Tarehe
10 Aprili, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameisisitiza Wakala ya Ndege za Serikali kuendeleza misingi imara iliyoachwa na Bodi ya Ushauri ya Wakala hiyo hususan katika usimamizi wa rasilimali mbalimbali ili ziweze kutumika ipasavyo na kuleta tija kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 10 Aprili, 2026 jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya kuwaaga Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Ndege za Serikali iliyomaliza muda wake.
Waziri Kikwete ameishukuru na kuipongeza Bodi hiyo kwa utendaji kazi mzuri walioufanya wakati wote walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kumshauri. “Kimuundo, Bodi hii ni chombo cha kumshauri Waziri. Ninakiri kuwa nimekuwa nikipata ushauri wa namna ya kuboresha ufanisi wa Wakala hii ili kuweza kufikia malengo ya Serikali na kupitia ushauri huo, malengo ya Wakala yameweza kufanikiwa na utekelezaji wa masuala mbalimbali unaendelea kufanyika kama ilivyoshauriwa,” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Ameongeza kuwa, Bodi hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa weledi na uzalendo pamoja na kumpa ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu na kufanya kazi yake kuwa nyepesi. “Nina kila sababu ya kujivunia mafanikio na hatua mbalimbali za mchango wa Bodi hii katika kufanikisha shughuli za Wakala,” ameongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Ndege za Serikali, Prof. Mhandisi Idrissa Mshoro amemshukuru Waziri Kikwete kwa kuendelea kuiamini Bodi hiyo kwa kipindi chote tangu ilipoteuliwa hadi kukamilisha kipindi cha pili cha miaka mitatu.
Naye Afisa Mtendaji wa Wakala ya Ndege za Serikali, Capt. Budodi Budodi amesema Bodi hiyo ya Ushauri iliyomaliza muda wake ilizinduliwa kuhudumu kwa kipindi cha pili kuanzia mwezi Agosti, 2023 na imefikia ukomo wake kwa mujibu wa Sheria.
Capt. Budodi ameyataja majukumu ya Wakala ya Ndege za Serikali kuwa ni pamoja na kumsafirisha kwa njia ya anga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Viongozi Wakuu wengine wa Kitaifa, kuratibu na kusimamia ununuzi na ukodishaji wa ndege za Serikali kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na kusimamia mikataba ya ukodishaji ndege hizo, kufanya matengenezo ya ndege za Serikali zinazotoa huduma kwa Viongozi Wakuu wa Kitaifa na kuhakikisha usimamizi madhubuti wa Wakala.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Ndege za
Serikali, wakimpokea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete mara baada ya Waziri
huyo kuwasili katika hafla ya kuwaaga wajumbe hao jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala
ya Ndege za Serikali iliyomaliza muda wake wakati wa hafla fupi ya
kuwaaga wajumbe hao iliyofanyika Aprili 10, 2026 Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi
ya Ushauri ya Wakala ya Ndege za Serikali, Prof. Mhandisi Idrissa Mshoro
wakati Waziri huyo alipokuwa akiwasili katika hafla ya kuwaaga wajumbe
hao iliyofanyika Aprili 10, 2026 Jijini Dodoma.
Afisa Mtendaji wa Wakala ya Ndege za Serikali, Capt. Budodi Budodi akitoa neno la utangulizi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wajumbe wa Bodi hiyo Jijini Dodoma
No comments:
Post a Comment