Monday, February 23, 2026

NAIBU KATIBU MKUU - UTUMISHI BW. XAVIER DAUDI AWAASA WATUMISHI WA UMMA KUWA KARIBU NA FAMILIA ZAO KUEPUSHA MSONGO WA MAWAZO NA ATHARI KATIKA UTENDAJI KAZI.

Na Eric Amani Dodoma, Tanzania

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi, amewahimiza Watumishi wa Umma nchini kutumia muda wao ipasavyo wakiwa pamoja na familia zao ili kuepuka msongo wa mawazo unaoweza kuathiri utendaji kazi wao.

Bw. Daudi ametoa wito huo wakati akizungumza na watumishi wa umma katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa ofisi hiyo leo Februari 23, 2026 jijini Dodoma ili kuimarisha ustawi wa watumishi mahali pa kazi, ambapo alisisitiza kuwa afya ya akili ni nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema kuwa watumishi wengi hawatengi muda wa kutosha wa kupumzika au kuwa karibu na familia zao hali inayoweza kusababisha uchovu wa akili na hatimaye kupunguza ufanisi kazini.

''Ni muhimu kwa watumishi wa umma kuhakikisha wanapata muda wa kuwa na familia zao, kushiriki shughuli za kijamii na kupumzika ili kujenga afya njema ya akili ambayo itawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,'' amesema Bw. Daudi.

Kwa upande wake, alieleza kuwa Ofisi ya Rais - UTUMISHI itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kazi kwa watumishi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi huku wakizingatia ustawi wao binafsi.

Aidha, Mwezeshaji ambaye ni Mwanasaikolojia, Mshauri Nasaha, Mtaalamu wa Mahusiano na Mwandishi Dkt. Chris Mauki wakati akitoa mafunzo hayo amesisitiza kuwa uwiano mzuri kati ya maisha ya kazi na familia husaidia kuongeza morali kazini, kupunguza msongo wa mawazo pamoja na kuboresha mahusiano kazini na nyumbani.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti Ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo baada ya kukamilika kwa mafunzo ya kuwajengea uwezo ambayo hufanyika kila jumatatu kwenye ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma leo Februari 23, 2026.  


Sehemu ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi Ofisi ya Rais – UTUMISHI wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa na mwezeshaji Dkt. Chris Mauki (Hayupo kwenye Picha) wakati akitoa mafunzo kuhusu watumishi wa Umma kutumia muda vizuri na familia zao ili kuepusha msongo wa mawazo unaoathari utendaji wa kazi Leo Februari 23, 2026 Dodoma, Tanzania.


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma SACP Ibrahim Mahumi akitoa neno la Shukrani kwa Menejimenti na Uongozi wa Ofisi hiyo kwa niaba ya watumishi wote wenye kumbukizi ya Siku ya kuzaliwa mwezi Februari Mtumba Jijini Dodoma.


Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakisherekea kumbukizi ya tarehe yao ya kuzaliwa leo Februari 23, 2026 katika Ofisi hiyo iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Bi Leila Mavika akifuatilia kwa kina mada iliyokuwa ikitolea na Mwezeshaji Dkt. Chris Mauki (Hayupo kwenye Picha) februari 23, 2026 katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.


Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI wakimsikiliza mwezeshaji Dkt. Chris Mauki (hayupo Pichani) wakati akitoa mafunzo kuhusu watumishi wa Umma kutumia muda vizuri na familia zao ili Kuepusha msongo wa mawazo unaoathari utendaji wa kazi Februari 23, 2026 Mtumba Jijini Dodoma.



No comments:

Post a Comment