Na Veronica Mwafisi-Muheza
Maelekezo yametolewa ya kusimamishwa kazi Watumishi wa umma 14 katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo.
Kusimamishwa kazi kwa watumishi hao, kunatokana na utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya hivi karibuni katika Mkoa wa Tanga ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza leo tarehe 19.02.2026 Wilayani Muheza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe wamesema Katika ziara aliyoifanya Waziri Mkuu mkoani Tanga, pamoja na shughuli nyingine, alitembelea na kukagua jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na kubaini uwepo wa changamoto katika utekelezaji wa mradi huo ambapo aliwaelekeza kuchukua hatua za haraka ili kubaini wahusika na kuchukua hatua stahiki.
Katika kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema, majukumu ya ofisi yake pamoja na ya Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI ni kuratibu masuala ya utumishi wa umma nchini, kwani Ofisi ya Rais UTUMISHI ndio mwajiri mkuu anayewapangia watumishi vituo vya kazi na vituo hivyo vinasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, linapotokea jambo linalohusu masuala ya kiutumishi, yeye Waziri wa UTUMISHI na Waziri wa TAMISEMI wanahusika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma na ndio maana Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Nchemba amewaelekeza kushughulikia changamoto hiyo ya utekelezaji wa mradi wa jengo hilo.
Maelekezo aliyoyatoa Waziri Mkuu kwa mawaziri hao, yalitokana na kubaini uwepo wa changamoto ya upotevu wa nondo 700 zenye thamani ya Shilingi 9,200,000.00 zilizonunuliwa kutoka Saifi Store, upotevu wa marine board 192 zenye thamani ya Shilingi 7,800,000.00, upotevu wa mifuko ya saruji 300 yenye thamani ya shilingi 4,400,000.00, kufanyika malipo ya kiasi cha Shilingi 110,600,000.00 kwa mhandisi mshauri Edge Engineering and Consulting Limited bila uwepo wa Mkataba na Shilingi 343,900,000.00 kutumika nje ya mradi kwa kulipana posho.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amefafanua kuwa, kufuatia malekezo ya Waziri Mkuu, yeye pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete walipeleka wataalam kutoka pande zote mbili ili kushughulikia suala hili katika hatua za awali.
Mhe. Prof. Shemdoe amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 37(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza akisimamiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga kuwapumzisha kutekeleza majukumu yao watumishi hao 14 ili kupisha uchunguzi.
Mhe. Prof. Shemdoe, ameongeza kuwa, kwa mujibu Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, kuunda Kamati ya Uchunguzi wa Awali ili kuwachunguza watumishi hao 14 wanaotumiwa kukwamisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala.
Aidha, amemuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa kufuatilia na kumsimamia Mkurugenzi wa Halmashauri kupata timu ya watu waadilifu watakaokuwa kwenye kamati hiyo ili kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Pia, amemtaka Mkurugenzi huyo, kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliotajwa na ambao hawakutajwa endapo watabainika kuhusika katika kusababisha changamoto katika utekelezaji wa mradi huo baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
Aidha, kwa wahusika waliotajwa katika taarifa za awali wasio watumishi Umma, Prof. Shemdoe amevielekeza vyombo vinavyohusika na uchunguzi ikiwemo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchukua hatua stahiki dhidi yao.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza
wakati wa kikao kilichofanyika mkoani Tanga kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa
fedha katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akizungumza nao wakati wa kikao kilichofanyika mkoani Tanga kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI,
Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na Watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wakati wa kikao kilichofanyika mkoani Tanga kufuatia
tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la
utawala la halmashauri hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akizungumza nao wakati wa kikao kilichofanyika mkoani Tanga kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo.






No comments:
Post a Comment