Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka amewataka waajiri katika taasisi za umma kuacha tabia ya kuomba kuhamisha watumishi kutoka katika vituo vyao vya kazi na kuwapeleka kwingine kwa kisingizio cha kutokuwa na uwezo kiutendaji.
Balozi Dkt. Kusiluka amepiga marufuku hiyo leo tarehe 17 Februari, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha wakati akifungua rasmi mkutano wa sita wa Serikali Mtandao.
Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri kupenda kuwahamisha watumishi na kutaka kupewa mbadala ambapo amemuelekeza Katibu Mkuu-UTUMISHI kutofanya hivyo. “Utumishi msifanye mambo hayo ya kuhamisha hamisha watumishi kwa kigezo cha kutofaa kiutendaji badala yake wapewe mafunzo ili waendane na utendaji kazi wa taaluma husika,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa, mtumishi ambaye hayuko vizuri kiutendaji ukimuhamishia kituo kingine hawezi kubadilika kwani kinachotakiwa hapo ni kujengewa uwezo na jukumu hilo ni la mwajiri wa taasisi husika.
Amesema kila mtumishi anatakiwa kupata mafunzo ya mara kwa mara lakini ni muhimu zaidi kwa wataalamu wa TEHAMA kwani teknolojia imekuwa ikibadilika, hivyo mtaalam wa TEHAMA asipopata mafunzo ya mara kwa mara ataachwa nyuma.
Ameongeza kuwa kujengewa uwezo wa kitaaluma unaweza kutekelezwa kwa namna mbalimbali ikiwemo kufanya vikao vya ndani na kuwasikiliza au kuwapeleka katika taasisi nyingine za sekta binafsi kwa mkataba.
Aidha, amewaelekeza waajiri kuweka vizuri utaratibu wa majukumu yao ili kuwarahisishia wataalamu wa TEHAMA pindi wanapotaka kubuni na kusanifu mifumo ya TEHAMA.
Amesema TEHAMA ni kipaumbele cha Serikali na hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Viongozi wengine wamekuwa wakitumia TEHAMA kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Ameipongeza e-GA kwa kubuni na kusanifu mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambayo imekuwa ikirahisisha utendaji kazi wa kila siku serikalini. “Tuliokuwa katika Utumishi wa Umma tangu zamani tunaona, kulikuwa na vikwazo vingi wakati tunataka kuanza kusanifu mifumo yetu, kuna watu wakasema hatutaweza, lakini sasa tumeweza, niwapongeze sana e-GA, niwasisitize kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolijia ili tusiachwe nyuma,” Katibu Mkuu Kiongozi amesisitiza.
Amesema, Serikali inathamini sana mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya TEHAMA na ndio maana imekuwa ikishirikiana nao. “tuendelee kufanya kazi pamoja kwani tunajenga nchi moja, sote tunawahudumia wananchi, tuendeleze ushirikiano ili tuwahudumie wananchi kikamilifu,” amesisitiza na kutoa angalizo la kusanifu mifumo yenye kuleta tija kwa taifa badala ya kusanifu mifumo itakayosababisha uvunjifu wa Amani. “Ninyi ndio mnaobuni na kusanifu mifumo, hivyo mbuni vitu ambavyo havileti shida kwa jamii na kuwaongoza vijana wetu kutumia mifumo hiyo kwa usahihi.
Akizungumza
kwa niaba ya Katibu Mkuu Ikulu, kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi
kuzungumza na washiriki wa mkutano huo, Bw. Xavier Daudi ambaye ni Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema katika kipindi hiki cha mabadiliko ya
kasi ya teknolojia, Serikali Mtandao imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika
kuimarisha utawala bora na ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema Serikali itaendelea
kuimarisha Mamlaka ya Serikali Mtandao, kwa kuitengea rasilimali na kuimarisha
miundombinu ya TEHAMA kulingana na mahitaji na mabadiliko ya teknolojia.
Awali akitoa neno la utangulizi , Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema e-GA imeendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao, kwa kuhakikisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanakuwa shirikishi, salama, yanazingatia Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, ili kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019.
Mhandisi Ndomba alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwekeza katika sekta ya TEHAMA na kuiwezesha Mamlaka kutekeleza majukumu yake ikiwemo, ujenzi wa Mfumo unaowezesha Mifumo ya Serikali Kuwasiliana na Kubadilishana taarifa, ujulikanao kama Government Enterprises Service Bus (GovESB). Ubadilishanaji wa taarifa kupitia mfumo huu, umechochea kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kikao kazi hicho cha siku tatu kinachoongozwa na Kaulimbiu isemayo “Kuboresha Utendaji wa Serikali
kwa Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Umma Kupitia Mifumo Salama na Jumuishi ya
Serikali Mtandao” kimewashirikisha zaidi ya wadau1400 na mada 14
kuhusu serikali mtandao zitawasilishwa kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa
masuala ya TEHAMA nchini.
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses
Kusiluka akizungumza na Maafisa Masuuli, Maafisa TEHAMA na watumiaji wa Mifumo
ya TEHAMA Serikalini wakati akifungua mkutano wa sita
wa Serikali Mtandao katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC)
jijini Arusha.
Sehemu
ya Maafisa Masuuli, Maafisa TEHAMA na watumiaji wa Mifumo ya TEHAMA Serikalini
wakiwa kwenye mkutano wa sita wa Serikali Mtandao uliofanyika
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa
maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka (hayupo
pichani) kufungua mkutano wa sita wa Serikali Mtandao ulioshirikisha Maafisa
Masuuli, Maafisa TEHAMA na watumiaji wa Mifumo ya TEHAMA Serikalini uliofanyika
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses
Kusiluka (katikati mstari wa mbele) akifuatilia jambo wakati wa mkutano wa sita
wa Serikali Mtandao uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha
(AICC) jijini Arusha. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI
na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses
Kusiluka (katikati) akisikiliza maelezo kuhusu mifumo mbalimbali kutoka kwa Maafisa wa Mamlaka ya
Serikali Mtandao (eGA) kabla ya kufungua mkutano wa sita wa Serikali Mtandao uliofanyika
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha. Wa kwanza
kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict
Ndomba.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akimsikiliza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano wa sita wa Serikali Mtandao katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.




No comments:
Post a Comment