Tuesday, August 26, 2025

WATUMISHI WA UMMA NCHINI WAASWA KUACHA KUKOPA KUPITA KIASI

Na.Lusungu Helela- Dar es Salaam

 Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi Rais, UTUMISHI,  Bi.Felister Shuli amewaasa Watumishi wa Umma nchini kuacha tabia ya kukopa kupita kiasi huku akisisitiza kuwa kitendo hicho ni kinyume na maadili katika  Utumishi wa Umma nchini.

 Mkurugenzi Shuli ametoa kauli hiyo  leo Jumanne Agosti 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada ya Maadili katika Utumishi wa Umma katika Mkutano wa 13 wa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka ( TRAMPA) unaotarajiwa kufunguliwa rasmi kesho na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa.

 Amesema kitendo hicho cha Mtumishi kukopa kupita kiasi humpelekea  kupata msongo wa mawazo na kusababisha kuwahudumia wateja kwa ukali au kwa kukosa  staha kutokana msongo wa mawazo alionao unaosababishwa na  madeni 

 Ameongeza kuwa baadhi ya Watumishi waliokopa kupita kiasi hujikuta ni watu wa kuhangaika hangaika na muda mwingine huwa na  mahudhurio  hafifu kazini " huwa ni watu wa  kujificha na kukimbia kimbia  ili  wadai wake wasiweze kuwaona kwani baadhi ya wadai wao huwafuata ofisini" amesema 

 Kufuatia hatua hiyo, Bi.Shuli amewataka Watumishi kuishi kulingana na kipato chao ili wasiweze kujiingiza kwenye madeni yasiyolipika na hivyo  kusababisha kushindwa kutoa huduma bora kwa wananchi. 

 Katika hatua nyingine, Bi.Shuli amewataka watumishi wa umma kujiepusha  na  michezo ya bahati nasibu na kubashiri ( betting ) kwani ni ukiukwaji wa Maadili katika  Utumishi wa Umma nchini

 " Jiepusheni na "betting" kwani watumishi wanaocheza michezo hiyo hujikuta wakitumia muda mwingi na fedha nyingi kucheza michezo hiyo na hivyo kusababisha kukopa kupita kiasi.

 

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi Rais, UTUMISHI,  Bi.Felister Shuli akizungumza leo  jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada ya Maadili katika Utumishi wa Umma katika Mkutano wa 13 wa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka ( TRAMPA) unaotarajiwa kufunguliwa rasmi kesho na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa.    








Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA)  wakimsikiliza  Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi Rais, UTUMISHI,  Bi.Felister Shuli  wakati akiwasilisha mada ya Maadili katika Utumishi wa Umma katika Mkutano wa 13 wa  TRAMPA unaotarajiwa kufunguliwa rasmi kesho na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa.





  Rais wa  Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) Bi. Devotha Mrope  akizungumza na Wanachama wa TRAMPA kwenye  Mkutano wa 13 wa  TRAMPA ulioanza jana na  unaotarajiwa kufunguliwa rasmi kesho na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma  kutoka  Ofisi Rais, UTUMISHI,  Bw. Andrew Ponda  akizungumza leo  jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada ya masuala ya Uhamisho kwa njia ya mfumo  katika Mkutano wa 13 wa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka ( TRAMPA) unaotarajiwa kufunguliwa rasmi kesho na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa

 

No comments:

Post a Comment