Na. Mwandishi Wetu- Dodoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ameitaka Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu
katika Ofisi hiyo kuongeza nguvu katika eneo la mafunzo ya umuhimu wa Urithishanaji wa madaraka kwa Watumishi wa
Umma huku akiwataka Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi nchini kuwaandaa watumishi wao
ili waweze kuwa viongozi wazuri hapo baadaye
Amesema Kiongozi
mzuri ni yule anayewaandaa watumishi walio chini yake kuwa viongozi wazuri
katika siku za usoni huku akionya dhana potofu iliyojengeka kuwa ukiwaandaa
watumishi walio chini yako wataichukua nafasi uliyonayo
Amesema Serikali ina
Taasisi nyingi ambazo zinahitaji watumishi hao walioandaliwa vizuri na kwa muda
mrefu
Bw. Mkomi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 18,
2025 katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba,
jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo mara baada ya kutolewa kwa mafunzo ya Uongozi, ikiwa
ni muendelezo wa mafunzo hayo ambayo hutolewa kila wiki kwa Watumishi kwa lengo
la kuboresha utendaji kazi wao
Amesema endapo kutakuwa na
utamaduni huo wa kurithishana madaraka, watumishi watakaoandaliwa wataenda kuwa
viongozi mahali pengine na sio lazima wabaki hapo hapo.
Awali Mwezeshaji wa
Mafunzo hayo ya Uongozi, Dkt. Ntangeki Nshala amesema Uongozi sio lazima
uwe unawaongoza watu bali ni kuonesha uwezo ulionao katika eneo ulilopo
Amesema uongozi ni suala binafsi na msukumo uliopo
ndani ya mtu ndio maana uongozi unatofautiana katika ya mtu na mtu
Amesema uongozi ni kuonesha njia,kujaribu
na kujiamini katika kufanya maamuzi popote ulipo na sio lazima uwe na cheo
fulani
Aidha Dkt. Nshala amesema
Watumishi wanahitaji kuwa na ujasiri na
ndoto kubwa ya kufanya chochote
wanachohitaji huku akionya tabia ya watu wengi ya kushindwa
kuonesha uwezo wao kwa kisingizio cha uroho wa madaraka
Amesema Watumishi waliowengi mara
baada ya kuajiriwa husahau kusudi la ndoto zao na hivyo hujikuta wakiishi ili
mradi kwa sababu hali zao za kiuchumi huwa zimeimarika kidogo
" Ukiwa huna ujasiri huwezi
kufanya mambo makubwa na hivyo wengi
hujikuta wakijidumaza" amesisitiza
Dkt. Nshala
Kufuatia hatua hiyo, Dkt. Nshala
amesisitiza watumishi kujitambua na kuwa na dira na maono ya kutaka kuwa nani katika kazi na kwenye
jamii kwa ujumla
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI Bw.Juma
Mkomi akizungumza na Watumishi wa Ofisi anayoingoza mara baada ya Mwezeshaji wa
mafunzo ya Uongozi, Dkt.Ntangeki kuhitimisha kutoa mafunzo hayo
Mwezeshaji wa mafunzo ya Uongozi, Dkt. Ntangeki Nshala akitoa
mafunzo hayo kwa Watumishi wa Ofisi ya
Rais, UTUMISHI na Utawala Bora katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali
Mtumba, jijini Dodoma
Baadhi ya Wakurugenzi wa Idara mbalimbali pamoja na Watumishi wa Ofisi ya Rais,UTUMISHI
na Utawala Bora wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yanaendelea kutolewa katika Ofisi hiyo
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI Bw. Juma Mkomi akikabidhiwa
moja ya kitabu cha masuala ya Uongozi kutoka kwa Mwezeshaji wa mafunzo Dkt.
Nshala mara baada ya kutoa mafunzo ya Uongozi kwa watumishi wa Ofisi
anayoiongoza
Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora wakiwa na Mwezeshaji wa mafunzo Dkt.Ntangeki Nshala wakipata maelezo ya vitabu mbalimbali alivyowahi kuandika .
Wakurugenzi wa Idara na Vitengo katika Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora wakionesha muitikio wao juu ya mafunzo yaliyotolewa Ofisini hapo kwa kununua vitabu vinavyoelezea masuala ya Uongozi vilivyoandikwa na Dkt. Nshala.
No comments:
Post a Comment