Sunday, March 16, 2025

TAKUKURU NI CHOMBO MUHIMU KWA MAENDELEO YA TAIFA - DKT.MHAGAMA

Na.Lusungu Helela-KILIMANJARO

Mwenyekiti wa Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph  Mhagama amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni chombo muhimu kwa ustawi na maendeleo ya Taifa la Tanzania na Watu wake.

 

Amesema ndoto ya Tanzania ijayo haiwezi kutimia bila uwepo wa chombo hicho.

 

Mhe. Dkt. Mhagama ametoa kauli hiyo leo  Jumamosi Machi 15, 2025 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria ya kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la  TAKUKURU,  Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro  ambapo amesisitiza kuwa suala la TAKUKURU kuwa na majengo yake ya kisasa ni jambo lisiloepukika.

 

Amesema Kamati hiyo iliamua kuweka kipaumbele cha kuhakikisha TAKUKURU inatekeleza majukumu yake ipasavyo ambapo moja ya kipaumbele hicho ni TAKUKURU kuwa na  majengo ya kisasa yatakayokuwa rafiki na wezeshi katika kusimika  vifaa vya kidijitali ili kurahisisha utendaji kazi.

 

"Tumehakikisha TAKUKURU inakuwa na majengo ya kisasa yenye hadhi na faragha ili iweze  kutimiza majukumu yake na sio majengo ya kupanga kama ilivyokuwa mwanzo amesisitiza Mhe. Dkt. Mhagama.

 

Amesema Kamati hiyo imeendelea kuipigania Taasisi hiyo ili iendelee kuongezewa  bajeti ya fedha kila mwaka.

 

Kufuatia hatua hiyo Mhe. Dkt. Mhagama amesema huo ni mwelekeo wa Serikali katika kuhakikisha kuwa TAKUKURU inakuwa chombo huru, chenye uwezo wa kutenda haki kwenye Taifa.

 

"Sisi Wajumbe wa Kamati hii kwa pamoja tunatoa pongezi zetu za dhati kwa  Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimama imara kwenye masuala ya rushwa katika Uongozi wake " amesisitiza 

 

Ameongeza kuwa "TAKUKURU  mnafanya kazi yetu ya Kamati kuwa nyepesi, sisi Wanakamati  tunajisikia fahari na heshima kwa jinsi mnavyowatendea Watanzania, hakika tumeridhishwa sana na utendaji wenu" 

 

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa jengo hilo, Mhe. Dkt. Mhagama amesema Kamati yake  imeridhishwa na ujenzi wa jengo hilo huku akisisitiza kuwa thamani ya fedha inaonekana dhahiri kuanzia kwenye lango kuu hadi ndani ya jengo.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus  Sangu amesema utashi wa kisiasa wa Rais  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umeiwezesha  TAKUKURU kupata vitendea kazi na kutimiza majukumu yake kwenye mazingira wezeshi.

 

Amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita zaidi ya Watumishi 1000 wameajiriwa na TAKUKURU, ikiwa ni jitihada  za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuiwezesha TAKUKURU.

 

Amesema mbali na magari 88 TAKUKURU iliyowezeshwa, inatarajia kwa mara nyingine tena  kupokea jumla magari 100 ili kuwawezesha maafisa hao kutekeleza majukumu yao mahali popote na saa yeyote wanakohitajika.

 

Amesema hiyo ni nia ya dhati ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha  TAKUKURU inakuwa ni chombo chenye uhalali katika jamii.

 

"Taasisi yetu sio tu inaziangalia Taasisi nyingine bali imekuwa mfano na kioo kwa Taasisi nyingine katika kuonesha thamani halisi ya fedha iliyotumika katika ujenzi wa jengo hili la Rombo" Mhe. Sangu amefafanua.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria imehitimisha ziara yake ya siku tatu ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mikoa ya Pwani, Tanga na Kilimanjaro na kukagua mradi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.

 

 

 

Mwenyekiti wa Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph  Mhagama akizungumza mara baada ya kutembelea na  kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la  TAKUKURU,  Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro

 

Muonekano wa jengo la  TAKUKURU,  Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro ambapo Wajumbe wa Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria waliptembelea na  kukagua mradi wa ujenzi wa jengo hilo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus  Sangu akizungumza mara baada ya Wajumbe wa Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kutembelea na  kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la  TAKUKURU,  Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro

 

Mwenyekiti wa Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph  Mhagama (katikati)  akiwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo mara baada ya kutembelea na  kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la  TAKUKURU,  Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro.

 

Wajumbe wa Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakipata maelezo ya miradi ya ujenzi wa majengo yanayojengwa katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini  mara baada Wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea na  kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la  TAKUKURU,  Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro

  Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila akizungumza kabla  Wajumbe wa Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuanza  kutembelea na  kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la  TAKUKURU,  Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro

 


 

 

 

No comments:

Post a Comment