Monday, March 24, 2025

UTUMISHI WASISITIZWA KUYAFAHAMU KIKAMILIFU MAADILI YA MSINGI YA OFISI NA KUYAZINGATIA KATIKA UTENDAJI

Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 24 Machi, 2025

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wamesisitizwa kuyafahamu kwa ufasaha maadili ya msingi ya Ofisi hiyo na kuyazingatia katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufikia lengo la utoaji wa huduma bora kwa umma.

Hayo yamesemwa leo Machi 24, 2025 kwa nyakati tofauti na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi pamoja na Mwanasaikolojia Dkt. Chris Mauki wakati wa mafunzo yanayofanyika kila Jumatatu kwa watumishi wa ofisi hiyo kwenye Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Daudi amesema ni wakati sasa wa watumishi hao kubadilika kiutendaji, “tubadilike ili tuwatumikie wadau wetu kwa weledi, tumepata somo zuri la mabadiliko ya utamaduni, mabadiliko haya yaanze na sisi na sio kwa kulazimishwa.” Amesisitiza.

Aidha, Bwana Daudi ametoa wito kwa watumishi hao kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika taasisi za fedha ili watakapofikia umri wa kustaafu wasipate changamoto zozote katika kuendesha maisha yao nje ya utumishi wa umma.

“Tunashukuru tumepata pia elimu ya uwekezaji, kutoka Watumishi Housing Investments (WHI) nawashauri tuwekeze, tunaweza tukaanza kuwekeza kidogo kidogo mpaka ukifika muda wa kustaafu utakuwa umewekeza kwa kiasi kikubwa.” Amesisitiza Bw. Daudi

Awali, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala-WHI, Bw. Pascali Massawe wakati akiwasilisha mada kuhusu Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa FAIDA FUND amesema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuwanufaisha Watanzania wote wa kipato cha chini, kati na cha juu ambao wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya kupata mtaji wa kuwekeza kwenye masoko ya fedha na mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi. 

Bw. Massawe amesema, gawio la Mfuko wa Faida linaleta tija kwa watu wote ambao watawekeza kwenye Mfuko huo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi, hivyo WHI inaendelea kutoa elimu kwa watumishi wa umma na wananchi ili wajitokeze kwa wingi kununua vipande katika mfuko huo.

“Mfuko wa Faida ni salama kwa watu wote ambao wanataka kuepuka upotevu wa fedha, hivyo natoa wito kwa watumishi wote wa umma na wananchi kujitokeza kununua vipande ili wanufaike na uwekezaji katika mfuko huu,” Bw. Massawe amesisitiza.

Kwa upande wake, Mtaalam wa Saikolojia, Dkt. Chris Mauki wakati akiwasilisha mada kuhusu mabadiliko ya utamaduni, amesema endapo Watumishi wa Umma watakuwa na utamaduni wa kuzingatia maandiko waliyojiwekea kwenye taasisi basi wananchi watanufaika kwa kupata huduma bora kwa ustawi wa taifa.

 “Tumejiwekea maandiko mengi sana lakini hatuyafuati, tuna Dira, Dhima na Maadili ya Msingi katika Ofisi yetu, hivyo ili twende vizuri katika utendaji inabidi kuyazingatia haya,” Dkt. Mauki amesisitiza.

Dkt. Mauki ameongeza kuwa utamaduni unajengwa na mambo mengi ikiwemo tabia, matendo, miendendo, imani, alama, desturi na hadithi, hivyo amewaomba kujitathmini na kuwajibika pasipo kushurutishwa katika kuwatumikia Watanzania.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi wa ofisi hiyo yaliyofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Sehemu ya Wakurugenzi na Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakifuatilia mafunzo kuhusu mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Fedha na Utawala-WHI, Bw. Pascali Massawe akiwasilisha mada kuhusu mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND wakati wa mafunzo kwa watumishi wa ofisi hiyo yaliyolenga kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji kazi.


Mtaalam wa Saikolojia, Dkt. Chris Mauki akifafanua jambo kwa Wakurugenzi na Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakati akiwasilisha mada kuhusu Utamaduni wa Taasisi au Ofisi kwenye mafunzo yanayotolewa katika ofisi hiyo lengo la kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji kazi.


Sehemu ya Wakurugenzi na Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Sehemu ya Wakurugenzi na Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.



No comments:

Post a Comment