Na. Veronica Mwafisi-Dar es Salaam
Tarehe 10 Machi, 2025
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Idara
ya Uendelezaji Sera, Bi. Mwanaamani Mtoo amesema Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imefanya jitihada kubwa katika kuwawezesha wanawake kupiga
hatua kimaendeleo.
Bi. Mtoo ameyasema hayo leo kwenye Kongamano la
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililolenga kujadili kuhusu Wanawake na
Uongozi katika Elimu lililofanyika Ukumbi wa Mikutano Hoteli ya WhiteSands
jijini Dar es Salaam.
Amesema uwezeshwaji wa wanawake umefanyika kwa
ushirikiano wa Viongozi wa Serikali pamoja na wanawake na wanaume kwani hakuna
maendeleo ya wanawake pasipokuwa na wanaume kama ambavyo Sera ya Menejimenti na
Ajira ya Mwaka 2008 ilivyotanabaisha katika Sura ya 5 ambayo inazungumzia Anuai
za Jamii katika Utumishi wa Umma ambao umeleta msukumo mpya wa ufanisi na tija kwenye utendaji kazi kwa
kutumia ujuzi na vipaji walivyonavyo.
Aidha, Bi. Mtoo amesema kwenye Sheria ya Utumishi wa
Umma Na. 298 pamoja na Kanuni za Mwaka 2022 zimeelekeza uzingatiaji wa masuala
ya kijinsia ambapo Ofisi hiyo imetoa Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Jinsia unaopaswa
kutumika wakati wa usimamizi wa rasilimaliwatu ikiwemo kwenye masuala ya usaili
na michakato ya ajira ili kuhakikisha watumishi wanawake au kundi la jinsi
yenye uwakilishi mdogo linapewa fursa katika nafasi za ajira kwa kuzingatia
sifa na vigezo.
“Mwongozo huu ni kielelezo
tosha cha dhamira ya Serikali ya kuimarisha ujumuishwaji wa jinsia katika
Utumishi wa Umma jambo ambalo ni muhimu katika kuboresha utendaji kazi
serikalini unaoiwezesha Serikali kuimarisha uchumi wa nchi na utoaji wa huduma kwa wananchi wote.” Amesisitiza Bi. Mtoo.
Ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kuleta mapinduzi
kwenye Sekta ya Elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imewezesha kuibua viongozi
mbalimbali wakiwemo wanawake kujumuishwa na kuleta uwiano sawa wa jinsia.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kutambua
thamani ya mwanamke, inampongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo katika taifa hili.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu, Wakala wa Maendeleo ya
Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid Maulid amesema kongamano hilo limelenga kujadili
mustakabali wa Mwanamke na Uongozi katika Elimu ambapo itawawezesha kupata
maoni, ushauri na mapendekezo
yatakayoleta matokeo na mikakati itakayowezesha kupiga hatua kubwa kwa maendeleo ya ustawi wa
taifa.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Idara
ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Mwanaamani Mtoo akichangia
mada wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani lililolenga kujadili kuhusu Wanawake na Uongozi katika Elimu lililofanyika
Ukumbi wa Mikutano Hoteli ya WhiteSands jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Idara
ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Mwanaamani Mtoo akiwa katika kazi
ya vikundi wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililolenga
kujadili kuhusu Wanawake na Uongozi katika Elimu lililofanyika Ukumbi wa
Mikutano Hoteli ya WhiteSands jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu, Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu
(ADEM), Dr. Maulid Maulid akielezea malengo ya Kongamano la Maadhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani lililolenga kujadili kuhusu Wanawake na Uongozi katika
Elimu lililofanyika Ukumbi wa Mikutano Hoteli ya WhiteSands jijini Dar es
Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Mwanaamani Mtoo (kulia) akizungumza jambo na Kiongozi wa Timu (Shule Bora) Bi. Virginie Briand (kushoto) na Bi. Zainab Dhanani (katikati) kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililolenga kujadili kuhusu Wanawake na Uongozi katika Elimu lililofanyika Ukumbi wa Mikutano Hoteli ya WhiteSands jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment