Na
Lusungu Helela-MONDULI
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene amewataka Watanzania kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward
Lowassa kwa kuendelea kudumisha umoja, amani na mshikamano ili kuepuka
mapigano yanayoendelea katika nchi zingine.
Mhe.
Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Jumapili Februari 9, 2025 wakati wa Ibada maalumu ya
Kumbukizi ya mwaka mmoja wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania,
Hayati Edward Lowassa huku akiwataka Watanzania kuendeleza yale
yote mazuri aliyokuwa akiyafanya.
Aidha, Mhe. Simbachawene
amesema Hayati Edward Lowassa atakumbukwa daima kwa kuwagusa watu wengi kwa
namna chanya.
Amefafanua
kuwa Hayati Edward Lowassa ni Kiongozi aliyekuwa na upendo,
aliyewasaidia watu wengi na aliyependa kuzungumza na kila
mtu
bila kujali anamfahamu au hamfahamu.
Ameongeza
kuwa "Hayati Edward Lowassa ni kiongozi aliyekuwa hapendi kumuona mtu yeyote akipata
shida, alitamani kumuona kila mmoja akiwa na furaha wakati
wote" amesema.
Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene amemshukuru Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuenzi Hayati Lowassa kwa mchango
wake chanya aliokuwa akiutoa kwa maendeleo ya taifa.
“Hivi sasa tuna shule nyingi zimejengwa na zimeendelea
kujengwa, barabara, miradi ya maji imeendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu
ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan” ameongeza.
Akizungumza
kwa niaba ya Familia ya Hayati Edward Lowassa, mtoto wa
kwanza ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Mhe. Fredrick Lowassa ametumia
fursa hiyo kuwashukuru wote waliokuwa pamoja tangu baba yao
alipofariki hadi hivi sasa huku akimtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa mchango wake mkubwa kwa familia hiyo
tangu baba yao alipoanza kuugua hadi umauti ulipomkuta.
"Ikiwa
leo ni mwaka mmoja tangu baba yetu atutoke, alikuwa ni
kiongozi na nembo ya Wananchi wa Monduli, tuendelee kumuenzi
kwa mchango wake mkubwa katika kudumisha mshikamano kwa jamii
za wafugaji wa asili" amesisitiza Mhe. Fredrick Lowassa
Aidha,
Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iharakishe mchakato wa kuandaa
Makumbusho ya Hayati Edward Lowassa kutokana na ujio wa wageni wengi wanaofika
nyumbani hapo kwa ajili ya kujifunza mambo aliyokuwa akiyafanya baba yao.
Naye,
Baba Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania KKKT
Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dkt. Solomon Masangwa ameisisitiza
familia ya Hayati Edward Lowassa kuzidi kumshirikisha Mungu
katika kila jambo wanalolifanya ili
kuendelea kushikamana.
Hayati
Edward Ngoyai Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2024 na kuzikwa
nyumbani kwake Monduli tarehe 17 Februari 2024.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza katika Ibada ya Shukrani ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Monduli Mjini Mkoani Arusha.
Sehemu ya wanafamilia wa Hayati Edward Lowassa wakiwa kwenye Ibada ya Shukrani ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Ngoyai Lowassa iliyofanyika leo katika Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT) Monduli Mjini Mkoani Arusha.
Sehemu ya wanafamilia wa Hayati Edward Lowassa wakiwa kwenye Ibada ya Shukrani ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Ngoyai Lowassa iliyofanyika leo katika Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT) Monduli Mjini Mkoani Arusha.
Mbunge wa Monduli, Mhe. Fredrick Lowassa akisalimiana na baadhi ya Washarika wakati wa Ibada ya Shukrani ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa iliyofanyika leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Monduli Mjini Mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment