Wednesday, February 5, 2025

WAELIMISHA RIKA OFISI YA RAIS-UTUMISHI WATAKIWA KUTOA ELIMU KUHUSU UIMARISHAJI WA AFYA KWA WATUMISHI

 Na. Mwandishi Wetu-Dodoma

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uendelezaji Sera, Sehemu ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Mwanaamani Mtoo ametoa wito kwa Waelimisha Rika wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kutoa elimu kwa watumishi walio kwenye Idara na Vitengo vya Ofisi hiyo namna ya kutunza na kuimarisha afya ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa masilahi mapana ya  taifa.

Bi. Mtoo ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo yaliyotolewa kwa Waelimisha Rika hao yaliyolenga kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.

Amesema kuwa Waelimisha Rika katika ofisi ni watu muhimu hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kufahamu mbinu mbalimbali za kutumia katika utoaji wa elimu na namna ya kuimarisha afya za watumishi wenzao ili ziwasaidie katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuzingatia utunzaji ya afya bora.

“Ninyi ni watu muhimu sana katika ofisi zetu, naamini mafunzo haya yatawajengea uwezo mkubwa wa kutoa elimu na kuwaelekeza watumishi wenzenu namna ya kutunza na kuimarisha afya iliyo bora, na hapa niwakumbushe kuzingatia lishe iliyo bora ili muweze kutekeleza majukumu ya taifa,” Bi. Mtoo amesema.

Akiwasilisha mada kuhusu lishe bora, Afisa Lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Bi. Nusrat Rubambura amesisitiza masuala ya kuzingatia katika kuimarisha afya ikiwemo kufanya mazoezi, kunywa maji ya kutosha pamoja na kula vyakula mchanganyiko kutoka katika makundi sita ikiwemo nafaka, mizizi na ndizi za kupika, asili ya wanyama, jamii ya kunde, mbogamboga, matunda na Mafuta salama.

Akizungumza kwa niaba ya Waelimisha Rika hao, Mwenyekiti wa Waelimisha Rika Bw. Kokolo Lusanda ameahidi watashirikiana katika kutoa elimu kwa watumishi wenzao ili kuzingatia utunzaji wa afya zao na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

 

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uendelezaji Sera, Sehemu ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Mwanaamani Mtoo akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo Waelimisha Rika wa Idara na Vitengo vya ofisi hiyo ili kupambana na Afua za VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza mahali pa kazi.


Sehemu ya Waelimisha Rika, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakifuatilia mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo Waelimisha Rika wa Idara na Vitengo vya ofisi hiyo ili kupambana na Afua za VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza mahali pa kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba.


Afisa Lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Bi. Nusrat Rubambura (aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu lishe bora wakati wa mafunzo kwa Waelimisha Rika wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaliyolenga kuwajengea uwezo Waelimisha Rika wa Idara na Vitengo vya ofisi hiyo ili kupambana na Afua za VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza mahali pa kazi.


Sehemu ya Waelimisha Rika, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uendelezaji Sera, Sehemu ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Mwanaamani Mtoo (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo Waelimisha Rika wa Idara na Vitengo vya ofisi hiyo ili kupambana na Afua za VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza mahali pa kazi.

 

Sehemu ya Waelimisha Rika, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakifuatilia mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo Waelimisha Rika wa Idara na Vitengo vya ofisi hiyo ili kupambana na Afua za VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza mahali pa kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba.


No comments:

Post a Comment