Na Lusungu Helela- IRINGA
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Iringa huku akiitaka Mikoa mingine kuiga mfano wa Iringa kwenye matumizi bora ya fedha za Mfuko huo.
Mhe.Sangu ametoa pongezi hizo leo baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Isele kilichopo Kata ya Mlenge, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kinachoendelea kujengwa na TASAF.
Kituo hicho cha Afya hadi kukamilika kwake kitakuwa na uwezo wa kuwahudumia zaidi ya wananchi 12,000 na kimelenga kupunguza vifo vya akina mama wajawazito pindi wanapojifungua pamoja na wagonjwa wengine.
Mhe. Sangu amesema Kituo hicho ni moja ya vituo 15 vya Afya vya kimkakati vinavyojengwa nchi nzima kupitia mradi wa TASAF kwa mwaka wa fedha 2025/2026
Amesema ujenzi wa vituo hivyo ni kielelezo cha umakini wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) katika kutekeleza Ilani yake ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote pasipo kujali mazingira wanayoishi lengo likiwa ni kupunguza vifo hususan vya akina mama wanapojifungua.
Ninawapongeza wananchi wa Isele licha ya kuletewa fedha za ujenzi wa kituo hiki na TASAF lakini nanyi mmejitolea kiasi cha Sh. milioni 19 na mmeshiriki kwenye kazi za kuchimba msingi pamoja na kusogeza mchanga, hii ni ishara ya uhitaji na utayari wa kukitumia Kituo hiki, amesisitiza Mhe.Sangu
Nimejionea majengo ikiwemo wodi la akina mama wajawazito pamoja na wodi ya wagonjwa wa kawaida yana ubora na thamani ya fedha inaonekana, hongereni sana kwa usimamizi makini "
Katika hatua nyingine, Mhe.Sangu ameridhishwa na ujenzi wa vivuko vya watembea kwa miguu vilivyojengwa katika maeneo korofi katika mitaa ya Ndwika na Kitwilu katika Manispaa ya Iringa ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi kwani walikuwa hawawezi kwenda shule pindi mvua ikinyesha.
"Watoto wetu walikuwa hawawezi kuvuka mvua ikinyesha, shughuli za kiuchumi pia zilikuwa zinasimama kwani wa upande wa pili walikuwa hawawezi kuja kwetu na sisi tulikuwa hatuwezi kwenda upande wa pili" amesema Juma Mwakarobo mmoja wa wakazi wa eneo Kitwilu.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata hiyo, Mhe. Msafiri Nzalamoto ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha za ujenzi wa Kituo hicho katika eneo analoliongoza huku akibainisha kuwa Kituo hicho kitakuwa mkombozi kwa wananchi wake hususan akina mama wajawazito ambao wengi wao walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo.
Ujenzi wa Kituo hiki umekuja wakati muafaka tunaahidi kukitunza ili kuhakikisha maono ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito yanatimia kwa wananchi wa Isele" amesema Mhe. Nzalamoto.
Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ambaye pia ni Mhandisi wa Miradi ya TASAF Mhandisi Emmanuel Chuwa alisema utekelezaji wa miradi unalengo la kuboresha huduma za kijamii katika maeneo ya wananchi Mkoani Iringa
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akizungumza leo na wananchi wa mtaa wa Kitwilu katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mara baada ya kukagua na kutembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akizungumza leo na wananchi wa kijiji cha Isele katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mara baada ya kukagua na kutembelea Kituo cha Afya ikiwa ni moja ya mradi ya maendeleo unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Sehemu ya wananchi wa Mtaa wa Ndyuka na Kitwilu katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu mara baada kutembelea na kukagua kivuko cha watembea kwa miguu
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akiwa ameongozana na wananchi wa Kijiji cha Isele mara baada ya kutembelea na kukagua Kituo cha Afya cha Isele kinachoendelea kujengwa katika eneo hilo.
Baadhi ya majengo ya Kituo cha Afya cha Isele yanayojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Ndyuka na Kitwilu katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakimshangilia Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu mara baada kutembelea na kukagua kivuko cha watembea kwa miguu
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Ndyuka na Kitwilu katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakimshangilia huku wakiagana naye Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu mara baada kutembelea na kukagua kivuko cha watembea kwa miguu
No comments:
Post a Comment