Na. Veronica Mwafisi-Kibaha
Tarehe 03 Juni, 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutumia taaluma na ujuzi waliokuwa nao katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kupokea rushwa hasa katika kipindi cha uchaguzi wa viongozi mbalimbali.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo tarehe 3 Juni, 2024 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani wakati akifungua kikao kazi cha viongozi wa TAKUKURU kilicholenga kujiimarisha zaidi katika kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Mhe.
Simbachawene amesema ni wakati sasa wa wananchi kupewa elimu kwa nguvu zote juu
ya rushwa katika uchaguzi ili kupata viongozi bora kwa maendeleo ya taifa kwani
kundi kubwa la wananchi linaamini kuwa mtu hawezi kumchagua kiongozi anayemtaka
mpaka apewe rushwa.
“Kuzuia
wananotaka kutoa rushwa pekee hakutoshi kwani makundi ya wapiga kura wanasadiki
kuwa mtu hawezi kumchagua kiongozi anayemtaka mpaka awe amepewa chochote, hivyo
tuwaelimishe na tuyaishi maisha ya kwenye vitabu vya dini kuwa anayetoa na
anayepokea rushwa, wote wana hatia,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Amesema
sote tunatambua kwamba uchaguzi wa viongozi ni jambo muhimu kwa mtu mmoja mmoja
na kwa Taifa kwa ujumla kwa sababu uchaguzi unagusa moja kwa moja maisha ya
wananchi wetu na mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.
Ameongeza
kuwa vitendo vya rushwa na makosa mengine yanayofanyika kabla au wakati wa
kuchagua viongozi, yanaharibu mchakato wa uchaguzi na huwapoka baadhi ya wapiga kura haki ya kumchagua mgombea wanayemtaka.
Na
kuongeza kuwa, vitendo hivyo huwanyima
haki baadhi ya wagombea kushiriki au kushindana kwa usawa katika uchaguzi huo. “Madhara ya uwepo wa vitendo hivi ni
pamoja na kupatikana viongozi wasiokuwa waadilifu na kuchelewa kupatikana au
kutopatikana kabisa kwa maendeleo na ustawi wa jamii ya Watanzania, kinyume na
matamanio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan. Hivyo, hatuna budi kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia vitendo hivyo
kuanzia hatua za awali kabisa za mchakato wa uchaguzi” Mhe. Simbachawene
amesema.
Akitoa
maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Mhe. Simbachawene kufungua kikao kazi
hicho, Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP
Salum Hamduni amesema kikao kazi hicho
cha siku tatu kwa viongozi hao wa TAKUKURU kimelenga kujipanga katika Kuzuia na
Kupambana na Rushwa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024 na
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
CP Hamduni ameongeza kuwa ni
wakati sasa wagombea na wananchi kufahamu madhara ya rushwa katika uchaguzi na
kuongeza kuwa watajipanga vema na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi
mkubwa bila ya kuwa na chembechembe za rushwa hatimaye kuwapata viongozi bora
kwa maendeleo ya taifa kama ilivyokusudiwa na serikali.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. George Simbachawene akizungumza na Viongozi wa TAKUKURU (hawapo
pichani) wakati akifungua kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika Kibaha
mkoani Pwani
katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.
Sehemu ya Viongozi wa TAKUKURU wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene
(hayupo pichani) wakati akizungumza nao kabla ya Waziri huyo kufungua kikao kazi cha Wakuu wa TAKUKURU
Mikoa, Naibu wa TAKUKURU Mikoa, Wakuu wa TAKUKURU Wilaya na Wakuu wa TAKUKURU
vituo maalumu kilichofanyika Shule ya
Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni akielezea lengo la kikao
kazi cha Wakuu wa TAKUKURU Mikoa, Naibu wa TAKUKURU
Mikoa, Wakuu wa TAKUKURU Wilaya na Wakuu wa TAKUKURU vituo maalumu kilichofanyika
Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene kuzungumza
na viongozi hao.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye akitoa utambulisho wa viongozi waliohudhuria kikao kazi cha Wakuu wa TAKUKURU Mikoa,
Naibu wa TAKUKURU Mikoa, Wakuu wa TAKUKURU Wilaya na Wakuu wa TAKUKURU vituo
maalumu kilichofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Pwani mara baada ya kuwasili katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo
la kufungua kikao kazi cha Wakuu wa TAKUKURU Mikoa, Naibu wa TAKUKURU Mikoa, Wakuu wa TAKUKURU
Wilaya na Wakuu wa TAKUKURU vituo maalumu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifurahia jambo na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni (kushoto) mara baada ya Waziri Simbachawene kupokea zawadi ya tai yenye nembo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa kikao kazi cha viongozi wa TAKUKURU kilichofanyika Kibaha mkoani Pwani katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya
pamoja na sehemu ya viongozi wa TAKUKURU baada ya kufungua kikao kazi cha
viongozi hao kilichofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha
mkoani Pwani. Kulia
kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.
No comments:
Post a Comment