Na Lusungu Helela-Bariadi
Tarehe 15 Septemba, 2023
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Ridhiwani Kikwete ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Simiyu.
Mhe. Kikwete amezitaka halmashauri zote nchini
zinazotekeleza miradi ya maendeleo hususani kwenye sekta ya huduma za jamii
kujifunza kutoka Mkoa wa Simiyu ambao una mafanikio makubwa.
Naibu Waziri ameyasema hayo mjini Bariadi baada ya
kupokea ripoti ya utelekezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa wa Simiyu ambao
pia ni miongoni mwa mikoa mitano inayotekeleza kwa majaribio miradi ya
kupunguza umasikini awamu ya nne- Tanzania Poverty Reduction Project (TPRP IV).
“Simiyu ni
miongoni mwa mikoa ya mfano kwa utekelezaji
na usimamizi mzuri wa miradi ya TASAF, nimeridhishwa sana na hatua kubwa
iliyopigwa katika utelekezaji wa shughuli hizi ambazo zina lengo la kuondoa umasikini na kurahisisha
upatikanaji wa huduma za kijamii,” amesema.
Aidha, Mhe.
Kikwete amesisitiza umuhimu wa
waratibu na wasimamizi wa miradi
ya TASAF kuendelea na ufuatiliaji wa karibu wakati wote wa utekelezaji kwa
lengo la kuhakikisha miradi yote inaendana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amesema serikali
kupitia TASAF imesitisha uhawilishaji fedha kwa walengwa kwa njia ya mitandao ya
simu na badala yake, zoezi hilo litafanyika kwa njia ya benki au mlengwa kupewa
fedha mkononi.
“Kumekuwa na changamoto kadhaa kwenye uhawilishaji
fedha kwa njia ya simu, sasa ili kuepukana na changamoto hizo kwa sasa,
walengwa watapokea fedha hizo kwa njia ya benki au kuchukua moja kwa moja,” amesema
Mhe Naibu Waziri.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, Prisca Kayombo, Mratibu wa
TASAF mkoa, Nyasilu Ndulu amesema jumla ya shilingi Bil. 9.24 zimepokelewa kwa ajili utekelezaji
wa miradi hiyo.
“Hadi sasa kaisi cha shilingi Bil. 6.03 sawa na
asilimia 65 ya fedha iliyopokelewa zimeshatumika katika ujenzi wa miradi
mbalimbali kama ya afya na elimu,” alisema.
Katika sekta ya afya TASAF imewezesha kujengwa kwa
Zahanati 9, Nyumba 14, majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) 2, jengo la upasuaji 1,
jengo la kuhifadhia maiti 1, wodi za mama na mtoto 5 pamoja na maabara 1.
“Kwa upande wa sekta ya elimu tumeweza kujenga vyumba 60 vya madarasa, ofisi 27 za walimu, matundu ya vyoo 186, maktaba 1, nyumba za walimu 4, majengo ya utawala 4 vyumba vya maabara 8 na mabweni 11,” alisema.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na walengwa wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Mtaa wa Mbiti, Kata ya Mhanga
iliyopo katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kukagua nyumba ya Mtumishi wa zahanati ya Mbiti
iliyojengwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akipata maelezo mara baada ya
kukagua nyumba ya Mtumishi wa zahanati ya Mbiti iliyojengwa kwa fedha za Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Mtaa wa Mbiti, Kata ya Mhanga iliyopo
katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiburudika na baadhi ya walengwa
wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Mtaa wa Mbiti Kata ya Mhanga
iliyopo katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kukagua nyumba ya
Mtumishi ya zahanati ya Mbiti iliyojengwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF).
Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF), Bwana Shedrack Mziray akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini na wananchi wa Mtaa ya Mbiti Kata ya Mhanga kabla ya kumkaribisha Naibu
Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete kuzungumza na wananchi wa mtaa huo mara baada ya kukagua nyumba ya Mtumishi wa zahanati ya Mbiti
iliyojengwa kwa fedha za Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF)
No comments:
Post a Comment