Na. Rainer Budodi-Chato
Tarehe 15 Septemba, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amewasisitiza watumishi wa umma nchini kuongeza elimu na ujuzi kwenye maeneo yanayohusiana na taaluma zao ili kuepusha malalamiko kati yao na waajiri.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinawazokabili watumishi hao katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema baadhi ya watumishi wamekuwa wakiruhusiwa na waajiri kwenda masomoni kuongeza ujuzi katika taaluma zao, lakini wakifika huko wanabadilisha na kusoma masuala mengine ambayo hayaendani na taaluma hizo na anaporudi katika kituo cha kazi anataka kubadilishiwa kada wakati mwajiri hana uhitaji huo, hivyo kusababisha malalamiko kati ya mwajiri na mtumishi.
“Wewe ni Mwalimu umepewa ruhusa na mwajiri wako kwenda kuongeza elimu na ujuzi kwenye taaluma yako, unafika chuoni unabadilisha unasoma kitu kingine bila makubaliano na mwajiri wako na unaporudi katika kituo chako cha kazi unataka kubadilishiwa kada, hiyo ni kusababisha matatizo na mwajiri wako,” Mhe. Simbachawene amesema.
Ameongeza kuwa mtumishi anaweza kubadilishiwa kada, endapo mwajiri ataona kuna uhitaji wa kada hiyo katika eneo lake na itampasa mtumishi huyo kuanzia daraja la mwanzo kulingana na kada husika vinginevyo awe ameruhusiwa na mwajiri ambapo ataombewa mshahara binafsi,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Amesema Serikali ingeruhusu kila mtumishi kujiendeleza anavyotaka tofauti na kada yake ingekuwa vurugu, hivyo kuepuka vurugu hizo kila mmoja ajiendeleze kwenye taaluma yake kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya utumishi wa umma iliyopo.
Mhe. Simbachawene anaendelea na ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Geita yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani humo na kusikiliza changamoto za kiutumishi zinazowakabili ili kuzitatua.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri
ya Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo wakati wa ziara yake ya
kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili
watumishi wa halmashauri hiyo.
Sehemu
ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita wakimsikiliza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara
ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.
Katibu
wa Chama cha Walimu Tanzania, Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mwalimu Oscar
Magori akiwasilisha hoja kwa Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene (hayupo
pichani) wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na watumishi wa umma wa Halmashauri
ya Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua
changamoto zinazowakabili watumishi wa Mkoa huo.
No comments:
Post a Comment