Tuesday, September 12, 2023

SERIKALI YATAKA WANAOKAIMISHWA NAFASI ZA MADARAKA KUWA NA SIFA STAHIKI

 Na. Lusungu Helela-Musoma

Tarehe 12 Septemba, 2023 

Watendaji katika Taasisi za Umma wamesisitizwa kuwakaimisha nafasi za madaraka watumishi wenye sifa za kushika nafasi hizo ili kuirahisishia kazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI kutekeleza hatua zinazofuata kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.

Hayo, yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa Mkoa wa Mara katika ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa umma.

"Tunawavunja moyo watumishi wenye sifa kwa kuwa baadhi ya viongozi wanakaimisha ofisi kwa watumishi wanaowataka wenyewe na kwa mapenzi binafsi na kusahau kuwa nafasi hizo zipo kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia sifa na vigezo’’amesema Mhe. Kikwete. 

Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amewataka Maafisa Utumishi kufanya kazi zao kwa weledi na kuhakikisha wanafuatilia masuala ya watumishi wao ikiwa ni pamoja maslahi, upandishwaji vyeo na stahiki mbalimbali.

Mhe. Kikwete yuko kwenye ziara ya kikazi mkoani Mara yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani humo na kusikiliza changamoto za kiutumishi zinazowakabili ili kuzitatua.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Manispaa ya Musoma, Mkoani Mara, ikiwa ni ziara yake ya  kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto  zinazowakabili watumishi hao


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya ya Musoma, Dkt. Khalifan Haule mara baada ya kuwasili katika Manispaa hiyo ya Musoma Mkoani Mara kwa ajili ya kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili w watumishi hao


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe.Said Mtanda akizungumza na Watumishi mara baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete kuzungumza nao ambapo  amewataka Watumishi hao  kufanya kazi kwa bidii

 

Sehemu ya Watumishi wa Manispaa ya Musoma wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na leo Mkoani  hapo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji

 




No comments:

Post a Comment