Na.
James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe
18 Juni, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
amesema, Taasisi ya Uongozi (UONGOZI
Institute) imeandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Viongozi wa
Kisiasa na Viongozi Watendaji katika Utumishi wa Umma yatakayotolewa kuanzia
wiki ijayo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, mafunzo hayo ni
sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anayetaka
viongozi kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya taifa.
Mhe. Mchengerwa amesema hayo, mapema leo mara baada ya kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, wajumbe wa bodi hiyo waliteuliwa hivi karibuni na Mheshimiwa Rais.
Mhe. Mchengerwa amefafanua
kuwa, miongoni mwa viongozi watakaopatiwa mafunzo ni Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu
Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala
wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi Wasaidizi na Wakurugezi wa Idara katika Taasisi za Umma.
Ameongea kuwa, mafunzo hayo
elekezi yatakayotolewa yatawaandaa viongozi hao kutambua majukumu yao na
kutekeleza kikamilifu wajibu wao, kwa mujibu wa Viapo vya Ahadi ya Uadilifu
katika Utumishi wa Umma walivyovitoa.
Mhe.
Mchengerwa amesema, ukienda katika mataifa mengine ya Afrika Taasisi ya UONGOZI
inasifika kwa kuwaandaa viongozi mbalimbali na imekuwa ni tegemezi katika kujenga
uwezo wa viongozi barani Afrika, hivyo Serikali imeona ni vema taasisi hii
itumike ipasavyo kutoa mafunzo kwa viongozi nchini ili waweze kuzingatia Miiko
ya Uongozi na Maadili ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewakumbusha viongozi wote kuwa, cheo ni dhamana hivyo kila kiongozi anaowajibu wa kuhakikisha anakitumia cheo chake kwa uadilifu mkubwa na kwa masilahi ya taifa.
“Viongozi tambueni uongozi ni dhamana hivyo mnapaswa kuongeza ufanisi kiutendaji kwa kushiriki mafunzo yatakayotolewa na Taasisi ya UONGOZI hivi karibuni” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amesema Serikali inatarajia kuwa, baada ya viongozi kupata mafunzo haya ya kuwajengea uwezo, hakutakuwa na kiongozi yeyote atakayekwenda kinyume na Kanuni za Maadili ya Utendaji kazi katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005.
Mara baada ya Mhe. Mchengerwa kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI, Mwenyekiti wa bodi hiyo Dkt. Stergomena Tax amemshukuru Mhe. Rais kwa kumteua yeye pamoja na wajumbe wengine wa bodi hiyo na kuahidi kuwa, watahakikisha wanatekeleza jukumu kubwa la Taasisi ya UONGOZI la kuwajenga viongozi ambao wataleta maendeleo endelevu katika taifa.
Dkt. Tax amesema, wao kama bodi wanatambua umuhimu wa kuwa na viongozi mahiri wenye uwezo wa kuiwezesha nchi kupata maendeleo katika sekta mbalimbali nchini, hivyo watatekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kutumia uwezo na uzoefu walionao.
Bodi
ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI iliyozinduliwa leo inaundwa na Mwenyekiti
Dkt. Stergomena Tax, Makamu Mwenyekiti Dkt. Laurean Ndumbaro na wajumbe wengine
ni Prof. Penina Mlama, Prof. Samuel Wangwe, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Mhe. Ritta
Swan, Bi. Susan Mlawi, Bi. Lina Soiri na Bw. David Walker.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI na wageni
waalikwa wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
(hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika leo katika Ukumbi
wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es
Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi
ya UONGOZI Bw. Kadari Singo akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya
taasisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) kabla ya waziri huyo
kuzindua Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI uliofanyika leo katika Ukumbi
wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa
katika picha ya pamoja na Wajumbe wa
Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI
wakionyesha vitendea kazi alivyowakabidhi leo kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
Taasisi ya UONGOZI, Dkt. Stergomena Tax
akitoa shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa mara baada ya Waziri huyo
kuzindua bodi hiyo leo katika Ukumbi
wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa
katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI na
watumishi wa taasisi hiyo mara baada ya
kuzindua bodi hiyo leo katika
Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini
Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuzindua Bodi ya Wakurugenzi
Taasisi ya UONGOZI leo katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment