Na. Veronica Mwafisi-Kondoa
Tarehe 10 Juni, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
amesema Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu Maafisa Utumishi wote
watakaobainika kuwadanganya Watumishi wa Umma wenye madai ya malimbikizo ya
mishahara kuwa wamewasilisha madai yao Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma kwa ajili ya kufanyiwa kazi wakati sio kweli.
Akizungumza na Watumishi wa
Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa leo Wilayani
Kondoa, Mhe. Ndejembi amesema kuna baadhi ya Maafisa Utumishi hawatekelezi
wajibu wao kikamilifu na kusababisha Ofisi ya Rais Utumishi kutupiwa lawama na
Watumishi.
Amewaelekeza Wakurugenzi kuwasimamia
Maafisa Utumishi wao ili watekeleze majukumu yao ipasavyo ikiwemo la
kushughulikia fomu za madai ya malimbikizo ya watumishi hao ili yafanyiwe kazi
kwa haraka kwa lengo la kupunguza malalamiko ya watumishi ambayo yanashusha ari
ya kutekeleza majukumu yao kikamifu.
“Madai ya Watumishi yakichelewa
kulipwa, mnasingizia fomu ziko UTUMISHI wakati sio kweli, mara nyingi fomu hizi
zinakuwa ziko kwenu Wakurugenzi sababu Maafisa Utumishi wenu kujifanya miungu
watu,’” Mhe. Ndejembi ameongeza.
Mhe. Ndejembi amesema madai ya
Watumishi ni haki yao ya msingi kwani
wanatumia jasho lao kulitumikia taifa, hivyo wanastahili kulipwa na si hisani.
Akizungumzia changamoto ya upandishwaji
madaraja kwa watumishi, Mhe. Ndejembi amewaelekeza Maafisa Utumishi nchini
kuhakikisha wanatenda haki kwa wanaostahili kupandishwa madaraja kama Mhe. Rais
Samia Suhuhu Hassan alivyoelekeza.
“Tujitume kwa bidii tusimuangushe
Mhe. Rais ambaye ameonyesha nia thabiti ya kuwajali Watumishi wa Umma katika
kulinda maslahi na haki zao za msingi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Mhe Ndejembi amewataka
Maafisa Utumishi kuwa makini katika mchakato wa kuwapandisha madaraja watumishi
wanaostahili kupanda na kuongeza kuwa Afisa Utumishi yeyote atakayebainika
kusababisha mtumishi kutopata haki hiyo atachukuliwa hatua.
Mhe. Ndejembi amewasisitiza
Watumishi wa Umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni,
Taratibu na Miongozo katika Utumishi wa Umma ili kuboresha utendaji kazi
utakaowezesha utoaji wa huduma bora kwa umma.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mhe.
Sezaria Makota, amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kufika Wilayani humo na
kuzungumza na Watumishi ambapo pia amesisitiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Mhe. Makota amesema hapendezwi
kuwepo kwa madai ya malimbikizo ya mishahara na ya upandishwaji vyeo ambayo
hayajafanyiwa kazi na Maafisa Utumishi katika Wilaya yake na kuongeza kuwa
hatosita kuwachukulia hatua watakaoshindwa kutekeleza maelekezo.
Mhe. Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya
kikazi Wilayani Kondoa kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma
wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmshauri ya Wilaya ya Kondoa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao leo wilayani Kondoa chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao leo wilayani Kondoa chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi leo wilayani Kondoa yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo.
Mkurugenzi wa Halmshauri ya Mji Kondoa Bw. Msoleni Dakawa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya halmashauri yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi wa Wilaya hiyo leo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Kondoa Bw. Mustapha Semwaiko akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji ya halmashauri yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi wa Wilaya hiyo leo
chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo.
No comments:
Post a Comment