Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 16 Juni, 2021
Watendaji wa Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wametoa elimu ya
masuala ya kiutumishi kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Rufiji kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu utekelezaji
wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Akizungumzia ujio wa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi hao wa CCM, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mchengerwa amesema kwa kuwa viongozi hao ni wasimamizi wa haki za watumishi na wananchi ni vizuri wakayaelewa vema majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuhimiza uwajibikaji na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika maeneo yao ya utawala.
“Nina imani mkitoka hapa mtakuwa ni chachu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kutoka kwa Watumishi wa Umma kwani Serikali imewaajiri kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,” Mhe. Mchengerwa alisisitiza.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma, hivyo amewaomba viongozi hao ambao ni wasimamizi wa haki za watumishi na wananchi katika maeneo yao, wawahimize watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara.
“Dhamira ya Mhe. Rais ni kuhakikisha haki za msingi za Watumishi wa Umma zinatekelezwa ili kuwajengea ari ya kutoa huduma bora kwa umma,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa rai kwa viongozi hao kutumia elimu waliyoipata kuhamasisha watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi.
Naye Katibu wa Umoja wa Vijana CCM Wilaya ya Rufiji, Bw. Hassan Makoba amesema, wakiwa wasimamizi wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 watawahamasisha Watumishi wa Umma kutimiza wajibu wao ili wananchi wapate huduma bora.
Bw. Makoba ameongeza kuwa, wameona nia ya dhati ya Serikali katika kusimamia upatikanaji wa haki za Watumishi wa Umma hususan upandishwaji vyeo na malipo ya madai yao mbalimbali yakiwemo malimbikizo ya mishahara, hivyo watakuwa ni mabalozi wazuri wa kuelezea nia njema ya serikali ili watumishi wawajibike ipasavyo.
Viongozi hao wamepata elimu
kuhusiana na usimamizi wa Sera na Miongozo katika Utumishi wa Umma, utaratibu
wa upandishwaji madaraja, taratibu za uhamisho, stahili za watumishi (Madai ya
malimbikizo ya mishahara na stahili nyinginezo) Uhamasishaji wa ujumuishwaji wa masuala ya Anuai za
Jamii (Jinsia, Ulemavu, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa) pamoja na
uzingatiaji wa Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka
2005.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waheshimiwa
Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi yake
iliyopo Mtumba kwenye Mji wa Serikali kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi.
Kulia kwake ni Naibu Waziri wake Mhe. Deogratius Ndejembi.
Waheshimiwa
Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao katika Ofisi
yake iliyopo Mtumba kwenye Mji wa Serikali kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi.
Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akielezea
masuala ya kiutumishi na utawala bora kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa
CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi ya
Rais-UTUMISHI kujifunza masuala
ya kiutumishi na utawala bora. Kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Mkurugenzi
wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa elimu ya masuala ya kiutumishi kwa Waheshimiwa Madiwani na
Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi ya Rais-UTUMISHI iliyopo
Mtumba Jijini Dodoma.
Kaimu
Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera, Bi. Mwanaamani Mtoo akitoa elimu ya masuala ya Sera
na Miongozo mbalimbali ya kiutumishi kwa Waheshimiwa
Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea
Ofisi Rais-UTUMISHI iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja
na Waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji na baadhi ya
Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI baada ya kikao na Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa
Wilaya ya Rufiji waliofika Ofisini kwake Jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza
masuala ya kiutumishi .
No comments:
Post a Comment