Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 29 Juni, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
amezindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi
ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI.
Akizindua mfumo huo leo
ofisini kwake jijini Dodoma, Mhe Mchengerwa amesema, uzinduzi wa mfumo huo ni
sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kutatua changamoto zinazowakabili
Watumishi wa Umma na wananchi.
Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo
huo utamuwezesha yeye na wasaidizi wake kupata taarifa za malalamiko yanayohusu
huduma zinazotolewa katika taasisi za umma, ikiwa ni pamoja na kupokea maoni,
pongezi kwa Mhe. Rais na Ofisi yake.
Amefafanua kuwa, mfumo huo pia
utawawezesha kufanya ufuatiliaji wa namna malalamiko yanavyopokelewa na kufanyiwa
kazi na kuongeza kuwa, mfumo unampa nafasi ya kutoa maelekezo ya
ushughulikiwaji wa malalamiko hayo pale anapoona kuna ulazima wa kufanya hivyo.
“Popote nitakapokuwa, iwe
safarini, ofisini au nyumbani, nitaweza kuona malalamiko yote yanayowasilishwa ofisini
kwangu na namna yanavyofanyiwa kazi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amesema mfumo
huo ni rafiki kwa watumiaji, hivyo kila mtumishi na mwananchi mwenye hoja ataweza
kuutumia bila changamoto yoyote kwa njia ya tovuti kwa anuani ya www.swu.utumishi.go.tz, simu janja kwa
kupakua SWU kutoka kwenye play store,
na simu ya kawaida kwa kutumia msimbo wa *152*00# na kuchagua namba 9 na baadae
namba 2 ili kuwasilisha malalamiko.
Aidha, katika kuadhimisha siku
100 za utendaji kazi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Mhe. Mchengerwa
amezindua Jarida la Utumishi la Habari na Matukio ili kuuhabarisha umma namna
Ofisi yake inavyomsaidia Mhe. Rais kutekeleza jukumu la usimamizi wa Utumishi
wa Umma na Utawala Bora.
Mhe. Mchengerwa ameongeza
kuwa, jarida hilo litauhabarisha umma juu ya mafanikio ya Serikali
yanayopatikani na utekezaji wa majukumu kwenye eneo la Utumishi wa Umma na
Utawala Bora.
“Jarida hili litakuwa linatoka
kila baada ya miezi mitatu na litakuwa na maudhui ya utekelezaji wa maelekezo
ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa na matukio mbalimbali ambayo ofisi imekuwa
ikiyafanya kwa masilahi ya umma hapa nchini,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Mhe. Mchengewa ametoa wito kwa
watumishi wenye habari za kiutumishi na utawala bora zenye manufaa kwenye
utumishi wa umma na umma kwa ujumla kuwasilisha taarifa hizo ili ziweze
kuchapishwa kwenye jarida hilo.
Awali akimkaribisha Mhe.
Mchengerwa kuzindua mfumo huo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, amefarijika
kuona utekelezaji wa maelekezo ya kuanzishwa kwa mfumo wa ushughulikiaji wa
malalamiko ya watumishi na wananchi umekamilika.
Mhe. Ndejembi amesema,
anakumbuka siku ya kwanza ya Mhe. Mchengerwa kuripoti kazini, alitoa maelekezo
ya kufanya kazi kidigitali katika kusikiliza kero, kupokea malalamiko na maoni
ambayo yatatumika kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa na Ofisi ya
Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, hivyo amefurahi kuona mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA
UTUMISHI kuzinduliwa rasmi.
Akitoa neno la utangulizi
kabla ya uzinduzi, Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro amempongeza Mhe.
Mchengewa kwa kuwahamasisha watendaji wake kutekeleza majukumu kwa njia ya
kidijitali ili kurahisiha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma na wananchi.
“Mfumo huu wa SEMA NA WAZIRI
WA UTUMISHI ni zao la hamasa yako ya utatuzi wa changamoto za watumishi na
wananchi zitakazowasilishwa kupitia mfumo huo”, Dkt. Ndumbaro ameeleza.
Mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA
UTUMISHI uliobuniwa na wataalam wa ndani wa TEHAMA umelenga kupunguza au
kuondoa kabisa kero na malalamiko ya Watumishi wa Umma na wananchi kama ambavyo
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani ameazimia katika utawala wake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na vyombo
vya habari kuhusu mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi,
ujulikananao kama SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) aliouzindua leo jijini
Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kushoto
kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijiandaa kubonyeza
kitufe leo jijini Dodoma ili kuzindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko
ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI
(SWU). Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akimkaribisha Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa kuzungumza na
vyombo vya habari kabla ya kuzindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko ya
watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU)
leo jijini Dodoma.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi kabla ya
uzinduzi wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi
ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) leo jijini Dodoma.
Mwonekano wa mfumo wa kushughulikia
malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA
UTUMISHI (SWU) uliozinduliwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Waandishi wa Habari kwenye uzinduzi wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) leo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akionyesha jarida
la Utumishi Habari na Matukio mara baada ya kuzindua jarida hilo leo jijini
Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi akishiriki
uzinduzi wa jarida hilo na kushoto kwake ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI,
Dkt. Laurean Ndumbaro.
No comments:
Post a Comment