Na. Veronica Mwafisi-Dar es
Salaam
Tarehe 29 Juni, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa ameutaka uongozi wa Watumishi Housing Company (WHC) iliyo chini ya
ofisi yake kutokuwa na mlengo wa kibiashara kwa kujenga nyumba za gharama nafuu
za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma wa kada za chini ili kutatua
changamoto ya makazi inayowakabili.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo kwa Mkurugenzi Mtendaji Watumishi Housing Dkt. Fredy Msemwa, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la Gezaulole Kigamboni na Magomeni jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mchengerwa amefafanua
kuwa, Watumishi Housing itaendelea kujenga nyumba za gharama nafuu ambazo Watumishi
wa Umma nchini wenye kipato cha kawaida watamudu kuzinunua.
Mhe. Mchengerwa ameuhimiza uongozi wa Watumishi Housing kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba kwenye maeneo mbalimbali ili kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba za watumishi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kutatua changamoto zote zinazowakabili Watumishi wa Umma nchini.
“Jengeni nyumba za kutosha zenye gharama nafuu katika miji mikubwa, Makao Makuu ya nchi Dodoma na maeneo ambayo yana changamoto ya miundombinu na uhaba mkubwa wa makazi ya watumishi”, Mhe. Mchengerwa amehimiza.
Ameongeza kuwa, dhamira ya
Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kutatua kero na changamoto zinazowakabili
watumishi ikiwemo uhaba wa nyumba za kuishi imelenga kujenga ari ya utendaji
kazi kwa watumishi wa umma na hatimaye wajivunie kuwa Watumishi wa Umma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Dkt. Fred Msemwa amesema ofisi yake itatekeleza maelekezo ya Mhe. Mchengerwa kwa kuongeza ubunifu ili kujenga nyumba za gharama nafuu kwa watumishi kwenye majiji na maeneo yenye uhaba wa nyumba hususani vijijini na kwenye maeneo yenye huduma za shule na afya.
Dkt. Msemwa ameahidi kuwa, ofisi yake itaendelea kubuni miradi itakayowahakikishia Watumishi wa Umma pamoja na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu kwa kuzingatia kipato chao.
Aidha, amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuipongeza ofisi yake kwa ubunifu wa miradi ya nyumba ambazo zimewawezesha Watumishi wa Umma katika maeneo yenye miradi ya nyumba za Watumishi Housing kupata nyumba za kupanga na kuishi.
Watumishi
Housing Company (WHC) ilianzishwa na Serikali mwezi Februari 2013 na kuanza
kufanya kazi kama Mfuko wa Nyumba za Watumishi na Wanachama wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii mwaka 2014 na mpaka hivi sasa imefanikiwa kujenga nyumba 917
katika mikoa 19.
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa akizungumza na watumishi wa Watumishi Housing Company (WHC) (hawapo
pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa
miradi ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la
Gezaulole Kigamboni na Magomeni jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya Watumishi wa WHC wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati
wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za
kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la Gezaulole Kigamboni
na Magomeni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Watumishi Housing (WHC) Dkt. Fred Msemwa akiwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa miradi ya ofisi yake kwa Mhe. Mchengerwa (wa kwanza kulia) wakati
wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi
ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la
Gezaulole Kigamboni na Magomeni jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye mradi wa WHC wa Gezaulole
Kigamboni wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa
miradi ya Watumishi Housing Company jijini Dar es Salaam.
Mwonekano
wa baadhi ya nyumba za Mradi wa Gezaulole uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam
unaomilikiwa na Watumishi Housing Company (WHC).
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa akiwa sehemu ya juu ya wazi ya mradi wa nyumba Magomeni na Mtendaji
Mkuu wa WHC Dkt. Fred Msemwa wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo
yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za kuwapangisha na
kuwauzia Watumishi wa Umma eneo la Magomeni Usalama jijini Dar es Salaam.
Mwonekano
wa Mradi wa nyumba wa Magomeni House unaomilikiwa na Watumishi Housing Company
(WHC) eneo la Magomeni Usalama jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment