Na. James K.
Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 04 Juni, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa
maelekezo kwa Uongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kutoa
mafunzo yatakayoimarisha Uzalendo na Utaifa ili kuzalisha Watumishi wa Umma na
Watanzania wazalendo watakaoshiriki vema katika kujenga uchumi wa taifa.
Akizungumza katika mahafali ya
33 ya chuo hicho yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amesema kutokana
na changamoto ya uzalendo kwa baadhi ya Watanzania, ni muda muafaka sasa kwa kila
mtanzania kuwa mzalendo kwa taifa lake kwa lengo la kulinda rasilimali za taifa
hivyo ni vema chuo kikajikita pia katika mafunzo ya uzalendo na utaifa.
Mhe. Mchengerwa amefafanua
kuwa wahitimu wakiwa na uzalendo watatumia vema mafunzo waliyoyapata ili kuleta
tija hususan katika kukuza uchumi wa taifa letu.
“Mafunzo mliyoyapata yasiishie
hapa bali yawe ni nyenzo na mkawe mabalozi wazuri kwa kutekeleza majukumu yenu
kwa weledi mkubwa na uadilifu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Katika kuwajengea uwezo
Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa Viongozi wa taasisi za Umma
na Halmashauri mbalimbali nchini kutenga bajeti itakayowawezesha watumishi wao
kushiriki mafunzo katika chuo cha utumishi wa umma yatakayowajengea uwezo
kiutendaji.
Mhe. Mchengerwa ameongeza
kuwa, kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma ni mojawapo ya utekelezaji wa Ilani cha
Chama cha Mapinduzi ya 2020, hivyo ameiagiza Bodi ya Ushauri na Uongozi wa Chuo
kufanya mawasiliano kwa lengo la kuzihimiza wizara na taasisi zote za serikali
ili watumishi wanaostahili kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wapate fursa
hiyo.
“Pamoja na utekelezaji wa Ilani ya CCM, dunia
inabadilika kutokana na kukua kwa teknolojia, hivyo ni lazima watumishi
washiriki mafunzo mara kwa mara kuendana na mabadiliko hayo.” Mhe. Mchengerwa
amesema.
Sanjari na hayo, Mhe.
Mchengerwa ameupongeza uongozi wa chuo na Wakufunzi kwa kutekeleza majukumu yao
ya msingi ya chuo na kuaigiza Bodi na uongozi kutekeleza maelekezo ya viongozi
mbalimbali ya kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuanzisha matawi mengi zaidi ya
chuo na kubuni mikakati mbalimbali itakayosaidia chuo hiki kuwa chuo cha mfano
ndani na nje ya nchi.
Akitoa neno la utangulizi
kabla ya kumkaribisha Waziri Mchengerwa kuzungumza na wahitimu, Mwenyekiti wa
Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florence Turuka
amesema wahitimu wamepata mafunzo mazuri yenye weledi mkubwa na kuwasihi
wahitimu hao kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kwa maslahi mapana ya taifa.
“Kutokana na mafunzo
mliyoyapata hapa naamini mtakuwa ni chachu ya maendeleo na mabalozi wazuri wa
chuo chetu huko muendako,” Dkt. Turuka amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo
na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Selemani Shindika
amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 2000 chini ya Sheria ya Wakala Na. 30 ya
mwaka 1997 kupitia Mpango wa Uboreshaji Utumishi wa Umma (PSRP) kwa lengo la
kubadilisha na kuboresha Utumishi wa Umma pamoja na kutoa mafunzo kuhusu
Utumishi wa Umma, kuratibu na kujenga utamaduni mpya wa Watumishi na Watumishi
wa Umma watarajiwa kujiendeleza ili kutoa huduma kwa weledi na ufanisi zaidi.
Dkt. Shindika amesisitiza
umuhimu watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza kushiriki mafunzo elekezi
katika Chuo cha Utumishi wa Umma ili kuwawezesha watumishi hao kufanya kazi kwa
weledi na ufanisi.
Jumla ya wahitimu 7136 kutoka
kwenye kozi 12 zinazotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wametunukiwa
Astashahada ya Awali, Astashahada, Stashahada na Shahada katika fani
mbalimbali.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akiongoza maandamano wakati mahafali ya 33 ya chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa
cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na wahitimu wakati wa mahafali ya 33 ya chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa
cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya wahitimu wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza
nao wakati wa mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC)
yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere
(JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florence Turuka akitoa
neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza
na wahitimu wakati wa mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania
(TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius
Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mkuu
wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt.
Selemani Shindika akielezea lengo la
kuanzishwa kwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakati wa mahafali ya 33 ya
chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha
Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akitunuku cheti kwa mmoja wa wahitimu kwenye mahafali ya 33
ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha
Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Wahitimu
na wageni waalikwa wakiwa kwenye mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma
Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment