Sunday, May 30, 2021

VIONGOZI TUMIENI WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2021 KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WATUMISHI WALIOPO PEMBEZONI

Na. James K. Mwanamyoto-Karema, Tanganyika

Tarehe 30 Mei, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka viongozi katika Taasisi za Umma kutumia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu kutembelea maeneo ya pembezoni ili kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma, ikiwa ni pamoja na kupokea maoni na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha Utumishi wa Umma nchini.

Dkt. Ndumbaro amesema hayo katika Tarafa ya Karema akiwa ameambatana na Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ambao kwa pamoja wamehimiza uwajibikaji na ufanisi kiutendaji katika taasisi zinazosimamia utoaji wa haki kwa wananchi. 

Aidha Dkt. Ndumbaro amewata viongozi katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanajenga utamaduni wa watumishi kufanya kazi kwa bidii, na kuongeza kuwa utamaduni huo utajengwa kwa kutambua na kuwapongeza wanaofanya kazi kwa juhudi na maarifa na kwa wanaolegalega warekebishwe ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi. 

Amefafanua kuwa, watumishi wanaochapa kazi wakipongezwa kwa kuandikiwa barua au kupewa cheti kutokana na mchango wao ndio njia pekee itakayowawezesha waajiri kujenga utamaduni wa watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi. tofauti na kuchukua hatua hiyo morali ya watumishi wanaowajibika ipasavyo itashuka kwa kiwango kikubwa.

Akizungumzia kuhusu mtazamo hasi wa baadhi ya watumishi wa Tarafa ya Karema kuamini kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewataka kubadili fikra zao kwani Serikali imewaajiri kwa lengo la kuwahudumia wananchi wa eneo hilo na si kuwapa adhabu kama baadhi yao wanavyodhani.

Dkt. Jingu amewaambia watumishi hao kuwa, Utumishi wa Umma ni popote hivyo amewataka kutumia fursa zilizopo katika Tarafa ya Karema kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome amesema katika sheria na masuala ya katiba ndio taifa linapata mfumo wa utoaji haki ambapo haki zipo za aina nyingi kama vile haki madai, haki jinai pamoja na haki utawala inayosimamiwa na Katibu Mkuu - UTUMISHI kuhakikisha inakwenda sawasawa ili wananchi wapate huduma bora katika Taasisi za Umma. 

Sanjali na hilo, Prof. Mchome amesema, migogoro ya ardhi iliyopo Karema ni changamoto kama ilivyo kwenye maeneo mengine, hivyo amewataka watumishi kushirikiana na wananchi hususani wazee wenye busara katika kutatua migogoro hiyo kwa njia ya usuluhishi badala ya kukimbilia Mahakamani kwani Mahakama kwa mujibu wa Katiba ni chombo cha mwisho cha utoaji haki.

Ziara ya Makatibu Wakuu hao mkoani Katavi ililenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi mkoani humo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumzia masuala ya kiutumishi na watumishi wa Tarafa ya Karema Wilayani Tanganyika.


Watumishi wa Umma wa Tarafa ya Karema wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za watumishi wa tarafa hiyo.


Mwalimu Baraka Ambonile wa Shule ya Msingi Kapalamsenga, Tarafa ya Karema Wilayani Tanganyika akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu mkuu huyo tarafani humo.


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akipokea hoja za masuala ya kiutumishi za watumishi wa Tarafa ya Karema toka kwa Afisa wa tarafa hiyo, Bw. Mbonimpaye Nkoronko kwa lengo la kuzifanyia kazi changamoto hizo.

 


 

Saturday, May 29, 2021

VYEO NI DHAMANA TUVITUMIE VIZURI KUTOA HUDUMA KWA WANANCHI NA WATUMISHI WA UMMA-Dkt. Ndumbaro


Na. James K. Mwanamyoto-Mpanda na Tanganyika

Tarehe 29 Mei, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kuwasimamia na kuwaongoza watumishi walio chini yao kutambua kwamba, cheo ni dhamana, hivyo wanapaswa kutumia vyeo vyao vizuri kuwahudumia wananchi na wanaowasimamia badala ya kujikweza.

Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo kwa Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Katavi, Manispaa ya Mpanda na Halmashauri za Wilaya ya Nsimbo na Tanganyika wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Katavi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili  watumishi walio katika maeneo ya pembezoni mwa nchi.

Amesema hakuna haja ya wenye madaraka katika Utumishi wa Umma kuwakandamiza waliochini yao, bali wanapaswa kutengeneza mazingira ya amani mahala pa kazi ili wao na wanaowasimamia washiriki kuujenga utumishi wa umma wenye msingi imara wa maadili na unaozingatia Kanuni, Sheria, Taratibu na Miongozo iliyopo.

“Mamlaka uliyonayo katika utumishi wa umma si lazima uyaonyeshe kwa mabavu na kujikweza kwani jamii inatambua na kukuheshimu kwa cheo au nafasi uliyonayo”, Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Ameongeza kuwa, cheo ni kama koti tu kwani ipo siku utalivua na litavaliwa na mwingine aidha kwa kustaafu au Serikali kumpatia mwingine cheo hicho, hivyo amewataka watumishi waliopo mkoani au makao makuu ya taasisi yoyote ile kutojiona kuwa ni bora kuliko wengine.

Amewakumbusha viongozi waliopo katika utumishi wa umma kuwahudumia wengine vizuri ili pindi watakapostaafu na kurejea kupata huduma katika ofisi walizokuwa wakiziongoza wapokelewe kwa heshima na kuhudumiwa vizuri.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Abdallah Malela amesisitiza utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Dkt. Ndumbaro kwa kuwataka Watumishi wa Umma mkoani Katavi kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo mkubwa na kuongeza kuwa, huo ndio utamaduni unaopaswa kuzingatiwa na mtumishi yeyote wa umma.

Dkt. Ndumbaro amehitimisha ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi kwenye halmashauri zilizopo pembezoni, ziara ambayo ililenga kuhimiza utendaji kazi wenye matokeo ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anautaka katika utawala wake, Sanjali na hilo Dkt. Ndumbaro ametumia ziara hiyo kutatua changamoto na kero zinazowakabili Watumishi wa Umma waliopo maeneo ya pembezoni katika mikoa hiyo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Katavi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi walio katika maeneo ya pembezoni. 

Baadhi ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi walio katika wilaya hiyo. 


Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bw. Omari Himidi akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi walio katika wilaya hiyo.

 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Katavi, Manispaa ya Mpanda na Halmashauri za Wilaya ya Nsimbo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Katavi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi walio katika maeneo ya pembezoni mkoani humo.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Bw. Abdallah Mohamed Malela akimshukuru Dkt. Laurean Ndumbaro kwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Katavi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi walio katika maeneo ya pembezoni mkoani humo. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa huduma kwa mtumishi aliyewasilisha changamoto ya kiutumishi mkoani Katavi wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi walio katika maeneo ya pembezoni mkoani humo.


Katibu wa Afya Mkoa wa Katavi Bw. Apolinari Mushi akiwasilisha changamoto za kiutumishi kwa Katibu Mkuu Utumishi, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo mkoani Katavi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi walio katika maeneo ya pembezoni mkoani humo. 


 

Friday, May 28, 2021

UHAMISHO WA WATUMISHI KUFANYIKA KIELEKTRONIKI KUPITIA MFUMO MPYA WA HCMIS KUANZIA MWEZI JULAI, 2021

Na. James K. Mwanamyoto-Sumbawanga

Tarehe 28 Mei, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kuanzia Mwezi Julai, 2021 Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara utatumika kuchakata na kuoanisha maombi ya vibali vya uhamisho wa Watumishi wa Umma, hivyo Serikali kwa kiasi kikubwa itapunguza malalamiko ya watumishi kuhusu changamoto iliyopo ya upatikanaji wa vibali vya uhamisho kuchukua muda mrefu.

Dkt. Ndumbaro amesema hayo mjini Sumbawanga wakati akizungumza na watumishi mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma mkoani humo. 

Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa, mfumo huo utakapoanza kufanya kazi, utaboresha ufanisi wa waajiri katika kuratibu zoezi zima la uhamisho wa Watumishi wa Umma nchini. 

“Baada ya watumishi kuomba uhamisho, maombi yote yataingizwa kwenye mfumo ambapo yatachakatwa, kuoanishwa na kuwasilisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kutoa kibali,” Dkt. Ndumbaro amefafanua. 

Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, ili kuhakikisha uhamisho hauibui tatizo la uhaba wa watumishi kwenye maeneo ya uhitaji mkubwa wa rasilimaliwatu, Wakuu wa Taasisi za Umma, Wakurugenzi Watendaji, Matatibu Tawala Mkoa, Katibu Mkuu TAMISEMI pamoja yeye mwenyewe wamepewa uwezo wa kuona na kuratibu maombi yote ya uhamisho ndani ya maeneo yao ya utawala, hivyo suala la uhamisho litakuwa rahisi kufanyiwa kazi na mamlaka, kwa mantiki hiyo watumishi wataruhusiwa kuhama pasipokuwa na vikwazo visivyo na msingi wowote. 

Kwa upande wake Mtumishi Kilingo ambaye ni Mwalimu, ameipongeza Serikali kwa kuunda mfumo utakaoratibu uhamisho na malipo ya madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi (automatic) na kuongeza kuwa mfumo huo utapunguza kero zilizokuwa zikiwakabili Watumishi wa Umma nchini kwa kipindi kirefu. 

Mwalimu Kilingo amempongeza pia Dkt. Ndumbaro kwa kuupa mkoa wa Rukwa Afisa anayeshughulika na mfumo (approver) anayewajibika kikamilifu tofauti na aliyekuwepo mwanzo ambaye alilalamikiwa kwa kutotekeleza majukumu yake kwa wakati.

Dkt. Laurean Ndumbaro amehitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Rukwa na kuelekea mkoani Katavi kuendelea na ziara yake yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi waliopo katika mkoa huo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na Watumishi wa Umma mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao mkoani humo. 


Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao. 


Mwalimu Kilingo wa Manispaa ya Sumbawanga akiipongeza Serikali kuunda mfumo wa kielektroniki utakaoratibu uhamisho na malipo madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa ushauri wa kiutumishi kwa Mwalimu Kiligo wa Manispaa ya Sumbawanga wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu Utumishi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Mkoa wa Rukwa. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akifanya mawasiliano kwa njia ya kwa simu ya kiganjani na Afisa wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI aliyepo Dodoma ili kutatua changamoto ya kiutumishi inayomkabili Mtumishi wa Manispaa ya Sumbawanga. 

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitatua changamoto za kiutumishi za watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu Utumishi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma mkoani humo. 





 

Thursday, May 27, 2021

WATUMISHI TOENI HUDUMA NZURI KWA WANANCHI NA WATUMISHI WENZENU ILI WANUFAIKE NA HUDUMA ZITOLEWAZO NA SERIKALI

Na. James K. Mwanamyoto-Kalambo

Tarehe 27 Mei, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na maeneo mengine nchini kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kutoa huduma nzuri kwa wananchi na watumishi wenzao ili wanufaike na huduma bora zitolewazo na Serikali yao kupitia Taasisi zake.

Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo akiwa kwenye ziara ya kikazi Wilayani Kalambo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. 

Dkt. Ndumbaro amewaasa watumishi hao kuwajibika kikamilifu kwa kutoa huduma bora pindi wananchi wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi kwani wameajiriwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. 

Akizungumzia changamoto ya utoaji wa huduma kwa baadhi ya watumishi wa makao makuu ya Halmashauri za Wilaya au Taasisi za Umma, Dkt. Ndumbaro amewahimiza watumishi wote waliopo makao makuu kutoa kipaumbele cha utoaji huduma kwa wananchi na watumishi wanaolazimika kusafiri umbali mrefu ili kufuata huduma. 

Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, kipaumbele cha huduma kikitolewa kwa wananchi na watumishi wanaosafiri umbali mrefu kufuata huduma, hawataingia gharama za malazi kwani watakuwa wamehudumiwa kwa wakati na kurejea katika makazi yao.

“Tumieni saa za kazi ipasavyo kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na watumishi wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma badala ya kutumia muda mwingi kwenye mambo yasiyo na tija kwa taifa, Dkt. Ndumbaro amesisitiza.” 

Ameongeza kuwa, Watumishi wanaposafiri umbali mrefu kufuata huduma na wasipopatiwa huduma stahiki kwa wakati, watumishi hao wanakosa morali ya kufanya kazi na hatimaye kushindwa kutoa huduma nzuri kwa wananchi hivyo kuibua malalamiko dhidi ya Serikali. 

Akitoa shukrani kwa niaba ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Mkuu wa TAKUKURU (W) Bi. Lupakisyo Mwakyolile amempongeza Dkt. Ndumbaro kwa kuitembelea wilaya hiyo iliyopo pembezoni, na kumshukuru kwa kusikiliza na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa wilaya hiyo kwa muda mrefu. 

Bi. Mwakyolile amesema, ziara ya Dkt. Ndumbaro imejenga morali ya kufanya kazi kwa watumishi wa Wilaya ya Kalambo na kumhakikishia Dkt. Ndumbaro kuwa watachapa kazi kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anavyosisitiza kupitia kaulimbiu yake isemayo KAZI IENDELEE.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ameanza ziara ya kikazi mkoani Rukwa kwa kuitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo iliyopo pembezoni ili kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi waliopo katika wilaya hiyo ambapo anatarajia kuhitimisha ziara hiyo kesho kwa kuzungumza na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa na baadae kuelekea mkoani Katavi kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi waliopo katika mkoa huo.

 

 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za watumishi hao. 


Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za watumishi hao. 


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Bw. Palela Msongela akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya wilaya yake kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za kiutumishi.


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akijibu hoja za kiutumishi zilizowasilishwa wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kalambo. 


Mwalimu Shinuna Khalfan wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo Wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za kiutumishi.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akipitia changamoto na kero zilizowasilishwa kwake na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ili azitatue. 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akijibu hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za kiutumishi. 


Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kalambo, Bi. Lupakisyo Mwakyolile akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, mara baada ya Dkt. Ndumbaro kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili watumishi wa Halmashauri hiyo.


 

Wednesday, May 26, 2021

WATUMISHI WILAYANI ILEJE NA MOMBA WATAKIWA KUWA WAADILIFU ILI KUTEKELEZA AZMA YA RAIS YA KUBORESHA UTUMISHI WA UMMA

Na. James K. Mwanamyoto-Ileje na Momba

Tarehe 26 Mei, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma wa Halmashauri za Wilaya ya Ileje na Momba mkoani Songwe kuwa waadilifu mahala pa kazi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuujenga Utumishi wa Umma kuwa unaozingatia uadilifu wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.

Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo kwa watumishi hao wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, ikiwa ni pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi walio katika wilaya hizo zilizoko pembezoni.

Dkt. Ndumbaro amewaambia watumishi hao kuwa uadilifu unajengeka kwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma na kuongeza kuwa, wakizingatia hayo hakutakuwa na upendeleo wakati wa utoaji huduma kwa wananchi na watumishi wanaohitaji huduma za kiutumishi kwa waajiri.

Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, wakati wa utoaji wa huduma kwa wananchi, watumishi hao wanapaswa kuhakikisha wanazingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005 ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, Dkt. Ndumbaro ametumia fursa hiyo kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa Wilaya za Ileje na Momba na kuzipatia ufumbuzi ili kuwawezesha watumishi hao kufanya kazi kwa weledi pasipo kuwa na changamoto ambazo kwa namna moja au nyingine zitakwamisha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kuhusu changamoto ambazo zinahitaji muda, viambatisho au vielelezo muhimu, Dkt. Ndumbaro amezichukua ili zikafanyiwe kazi na ofisi yake mapema iwezekanavyo na kuwaahidi kuwapatia mrejesho watumishi hao huku akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii wakati akishughulikia kero na changamoto zao.

Akishiriki kutatua kero za watumishi hao, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama amemtaka Katibu wa TSC Wilaya ya Ileje kufuatilia jarada la Mwalimu Kostadi Kasunga Makao Makuu ya TSC ili kumuwezesha mtumishi huyo kupata taarifa zake muhimu za kiutumishi alizozipoteza baada ya jarada lake kupotea mahala pa kazi.

Kufuatia maelekezo hayo, Mwalimu Kostadi Kasunga amemshukuru Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kwa ziara yake ya kikazi ambayo imekuwa ni chachu ya utatuzi wa changamoto za kiutumishi zinazowakabili watumishi walio katika wilaya hiyo.

Naye Bw. Ntuale Mwakabanje ambaye ni Afisa Muuguzi Msaidizi Mkuu wilayani Ileje amemshukuru Dkt. Ndumbaro kwa kufanya ziara katika halmashauri hiyo iliyopo pembezoni kwa lengo la kuzifanyia kazi changamoto na kero zinazowakabili kiutendaji.

Mara baada ya Katibu Mkuu kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma wilayani Momba, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Dkt. Seif Shekalaghe amemshukuru Dkt. Ndumbaro kwa kufika wilaya ya Momba ambayo iko pembezoni na kuongeza kuwa kitendo hicho kinadhihirisha kwamba yeye ni Katibu Mkuu wa UTUMISHI anayewajali watumishi wote bila kujali mazingira waliyopo.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Songwe, yenye lengo la kuhimiza utendaji kazi wenye matokeo ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anautaka katika utawala wake, Sanjali na hilo Dkt. Ndumbaro ametatua changamoto na kero zinazowakabili watumishi wa mkoani humo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo. 


Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo wilayani Ileje yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo. 


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Bw. Haji Musa Mnasi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya halmashauri yake kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo wilayani Ileje yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo.


Mwalimu Elius Majoba wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo wilayani Ileje yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo.


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akijibu hoja za kiutumishi zilizowasilishwa na watumishi wa Wilaya ya Ileje wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Dkt. Seif Shekalaghe akimshukuru Dkt. Ndumbaro kwa kufanya ziara ya kikazi wilayani Momba na Mkoa wa Songwe kwa ujumla yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo. 


Afisa Biashara, Bw. Maximillan Mtui wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba akiwasilisha changamoto za kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo wilayani Momba yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo.


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama akijibu hoja za kiutumishi zilizowasilishwa na watumishi wa Wilaya ya Momba wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo.


 

Tuesday, May 25, 2021

WATUMISHI SONGWE WATAKIWA KUCHAPA KAZI KAMA MHESHIMIWA RAIS ALIVYOELEKEZA ILI KULETA MAENDELEO KWA WANANCHI

Na. James K. Mwanamyoto-Songwe

Tarehe 25 Mei, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewahimiza Watumishi wa Umma wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo kufanya kazi kwa bidii na maarifa kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza ili kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaletea maendeleo.

Dkt. Ndumbaro amesema hayo mkoani Songwe akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi mkoani humo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais, ambapo ameambatana na Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ambao kwa pamoja wamehimiza pia ufanisi kiutendaji katika Taasisi zinazosimamia utoaji wa haki kwa wananchi.

Dkt. Ndumbaro amewakumbusha watumishi hao moja ya hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa na kusisitiza Watumishi wa Umma nchini kuchapa kazi tu, na kuongeza kuwa watumishi wakifanya kazi kwa bidii watakuwa wakiunga mkono kaulimbiu ya Mhe. Rais ya Kazi Iendelee ambayo ina manufaa kwa maendeleo ya taifa.

Amefafanua kuwa, Watumishi wa Umma hawana budi kuendeleza utamaduni wa kufanya kazi zenye matokeo chanya, tija kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amewasisitiza Waajiri na Maafisa Utumishi kutekeleza kwa vitendo azma ya Mhe. Rais ya kuhakikisha Watumishi wa Umma wanapewa haki zao wanazostahili ili kuwajengea morali na ari ya utendaji kazi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome amewataka Watumishi wa Umma nchini kuishi maisha ya kiutumishi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma ili kufikia malengo ya uwepo wa Utumishi wa Umma.

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewakumbusha watumishi wa Songwe kuwa, muda mwingi wanautumia kazini, hivyo wahakikishe wanaishi vizuri na watumishi wengine mahala pa kazi, na kuongeza kuwa wasipoishi vizuri wataharibikiwa na hatimaye kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo ya Makatibu Wakuu hao, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Seif Shekalaghe amewaasa watumishi anaowasimamia kubadilika na kuanza kufanya kazi kwa bidii na weledi, na kuongeza kuwa amepokea maelekezo waliyoyatoa na kuahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wake. 

Ziara ya Kikazi mkoani Songwe ya Makatibu Wakuu hao imelenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi mkoani humo, sanjali na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Mhe. Rais ya kuhakikisha watumishi wanapata stahili zao kwa wakati ili kuwajengea morali ya kuutumikia umma kwa uadilifu na ufanisi.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na Watumishi wa Umma wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa mkoa huo.

Baadhi ya Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.


Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome akiwasisitiza watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma nchini.


Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwahimiza watumishi wa Songwe kushirikiana mahali pa kazi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akijibu hoja za Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo walizoziwasilisha wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa mkoa huo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Bi. Hanji Godigodi akiwasilisha changamoto za kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama akiwahudumia watumishi wanaowasilisha changamoto za kiutumishi wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo. 


Afisa Elimu Halmashauri ya Mji Tunduma Bw. Franco Ngonya akiwasilisha changamoto za kiutumishi zinazomkabili kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama akisoma moja ya nyaraka ya mtumishi aliyewasilisha changamoto ya kiutumishi wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Dkt. Seif Shekalaghe akiwaasa watumishi anaowasimamia kufanya kazi kwa bidii na weledi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo waliyoyatoa Makatibu Wakuu wa  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.

 


 

Friday, May 21, 2021

MAKATIBU MAHSUSI NCHINI WATAKIWA KUWA NA LUGHA YA STAHA WAKATI WA KUTOA HUDUMA KWA UMMA


 

MAKATIBU MAHSUSI NCHINI WATAKIWA KUWA NA LUGHA YA STAHA WAKATI WA KUTOA HUDUMA KWA UMMA

Na. James K. Mwanamyoto-Arusha

Tarehe 21 Mei, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Makatibu Mahsusi kutumia lugha yenye staha wakati wa kuwahudumia watumishi na wananchi wanaofuata huduma katika taasisi zao.

Akifungua mkutano wa 8 wa mwaka wa Makatibu Mahsusi kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Phillip Mpango jijini Arusha, Mhe. Mchengerwa amesema, Makatibu Mahsusi ni kioo cha ofisi yoyote ambayo wageni wanaofuata huduma wanapata taswira halisi ya huduma zitolewazo, hivyo wanapaswa kuwa na kauli nzuri na kutoa huduma bora.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa Makatibu Mahsusi katika uendeshaji wa shughuli za kila siku za ofisi, hivyo hawana budi kuendelea kuilinda imani ya Serikali kwa kuwajibika kikamilifu.

Akizungumzia dhamira ya kuboresha Utumishi wa Umma nchini, Mhe. Mchengerwa amesema hakuna haki isiyokuwa na wajibu, hivyo amewataka Makatibu Mahsusi kutofanya kazi kwa mazoea na wale ambao ni kikwazo katika kutoa huduma wabadilike ili kuendana na azma ya Serikali.

Mhe. Mchengerwa amewaasa Makatibu Mahsusi kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia uadilifu hususan utunzaji wa siri za ofisi na kuongeza kuwa watakaobainika kutozingatia hayo wataondolewa katika ofisi zao.

“Tunahitaji watumishi wachapakazi na waadilifu, kwani dhamira ya serikali ni kusonga mbele, kama utashindwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu utaondolewa bila kujali taasisi uliyopo.” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Katika kuhimiza uadilifu kwa Makatibu Mahsusi, Mhe. Mchengerwa aliwataka Makatibu Mahsusi hao kula kiapo cha Uadilifu kwa Watumishi wa Umma ambapo watumishi hao walitekeleza.

Akifafanua changamoto iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TAPSEA, Bi. Zuhura Maganga kuhusu Makatibu Mahsusi ambao wana umri mkubwa kutothaminiwa hivi sasa na kufikia hatua ya kutopewa kipaumbele kuwahudumia viongozi, Mhe. Mchengerwa amewataka waajiri kuthamini umuhimu wa Makatibu Mahsusi hao ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi kwa kutumia uzoefu walio nao ikiwa ni pamoja na uadilifu na uchapakazi wao.

Ili kuendana na Kaulimbiu ya mwaka huu inayohimiza ubunifu, umahiri na uzingatiaji wa weledi katika utendaji kazi kwa Makatibu Mahsusi, Mhe. Mchengerwa amewataka kuitekeleza kwa vitendo kwa kujiendeleza kitaaluma hususan katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewapongeza viongozi wa TAPSEA kwa kuandaa mkutano huo na kuweka utaratibu wa Makatibu Mahsusi kuchangia damu itakayohifadhiwa katika benki ya damu kwa lengo la kuwahudumia wenye mahitaji katika hospitali mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella amezungumzia umuhimu wa Makatibu Mahsusi na kusema kuwa, watumishi hawa ni muhimu sana kiutendaji kiasi kwamba wakiondolewa hata kwa siku moja, utekelezaji wa majukumu ya taasisi yoyote ile utayumba.

Akitoa nasaha zake kabla ya kumkaribisha Mhe. Waziri kuzungumza na Makatibu Mahsusi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kada ya Uhazili ni kada muhimu sana ambayo inategemewa na viongozi na watumishi wengine katika utendaji kazi wa kila siku, hivyo amewataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja na kutunza siri za ofisi ili kusukuma gurudumu la maendeleo mbele.

Dkt. Ndumbaro amewapongeza Viongozi wa TAPSEA kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo uliohudhuriwa na washiriki wengi ambao watapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa kazi, hivyo amewasisitiza kuhamasisha ushiriki wa Makatibu Mahsusi wengi zaidi katika mkutano ujao.

Awali akitoa maelezo kuhusu TAPSEA, Mwenyekiti wa TAPSEA, Bi. Zuhura Maganga alisema Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) kilianzishwa mwaka 2008 kwa lengo la kukuza na kudumisha taaluma ya Makatibu Mahsusi na kuhimiza uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa umma.

Mkutano wa mwaka huu wa TAPSEA unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Kuwa Mbunifu Mahiri, Zingatia Weledi katika Kuleta Mabadiliko ya Uchumi Tanzania.” ambapo zaidi ya Makatibu Mahsusi 3000 wameshiriki Mkutano huo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Makatibu Mahsusi Jijini Arusha alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA).

 



Baadhi ya Makatibu Mahsusi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akitoa salamu za mkoa wake wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro, akifafanua masuala ya kiutumishi kwa upande wa Tanzania wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) jijini Arusha leo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Seif Mwinyi, akizungumzia masuala ya kiutumishi kwa upande wa Zanzibar wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) jijini Arusha leo.


Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) Bi. Zuhura Maganga akitoa maelezo ya awali kuhusu chama chake wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa chama hicho jijini Arusha leo.

 


Makatibu Mahsusi wakila kiapo cha uadilifu kwa Watumishi wa Umma wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akimkabidhi cheti Mkurugenzi Msaidizi, Bw. Gubas Vyagusa kwa niaba ya Ofisi ya Rais Utumishi cha kutambua mchango wa Ofisi hiyo katika kufanikisha mkutano wa Makatibu Mahsusi wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na mchangiaji wa damu salama alipowasili kufungua mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Serikali na baadhi ya Makatibu Mahsusi baada ya kufungua mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.