Wednesday, December 29, 2021

MHE. NDEJEMBI AMCHANGIA MLENGWA WA TASAF FEDHA YA NAULI NA VIFAA VYA SHULE NA KUMTAKA ASOME KWA BIDII

 Na. Veronica Mwafisi-Mkuranga

Tarehe 29 Disemba, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemchangia fedha ya nauli na ya kununulia vifaa vya shule mlengwa wa TASAF Bi. Siwema Chikawe, ambaye amewezeshwa na mpango wa TASAF kupata elimu ya Msingi, kidato cha kwanza mpaka cha nne na kwa sasa yupo kidato cha tano katika Shule ya Sekondari mojawapo iliyopo Mkoani Kilimanjaro.

Mhe. Ndejembi ametoa mchango huo, wakati akizungumza na wananchi na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kiparang’anda Wilayani Mkuranga.

Mhe. Ndejembi amesema, ameshawishika kumchangia mwanafunzi huyo kutokana na kazi nzuri iliyofanya na mratibu wa TASAF wilayani hapo na TASAF Makao Makuu kwa kumpatia ruzuku iliyomuwezesha kuendelea na masomo.

Akihimiza umuhimu wa elimu kwa walengwa wa TASAF, Mhe. Ndejembi amemtaka mlengwa huyo kutekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha anasoma kwa bidii ili hapo baadae aweze kuwa msaada wa kuikwamua familia yake kutoka katika lindi la umaskini.

“Hakikisha unazingatia masomo ili upate ufaulu mzuri utakaokuwezesha kujiunga na elimu ya juu kwa manufaa yako binafsi, familia yako na Taifa kwa ujumla”, Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake mlengwa huyo wa TASAF Bi. Siwema Chikawe, ameishukuru TASAF kwa kumuwezesha kupata mahitaji ya Shule kwani wazazi wake hawana uwezo wa kumsomesha.

Akieleza sababu ya familia yake kutokuwa na uwezo wa kumsomesha, Bi. Chikawe amesema baba yake mzazi hana uwezo wa kuona wakati mama yake mzazi hana kazi rasmi ya kumuingizia kipato cha kumuwezesha kumudu gharana za masomo yake.

Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Mkuranga yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi na walengwa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Mlengwa wa TASAF Bi. Siwema Chikawe akitoa ushuhuda kwa Naibu Waziri    Mhe. Deogratius Ndejembi wa namna TASAF inavyomuwezesha kupata mahitaji ya Shule, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akijibu hoja za walengwa wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akipokea zawadi ya bidhaa zinazotengenezwa na walengwa wa TASAF Wilayani Mkuranga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani humo.

 



Tuesday, December 28, 2021

NAIBU WAZIRI NDEJEMBI AONYA VITENDO VYA RUSHWA KWA WATUMISHI WA IDARA YA ARDHI MKURANGA

Na. Veronica Mwafisi-Mkuranga

Tarehe 28 Disemba, 2021 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameonya vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.

Akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga katika kikao kazi chake na watumishi hao, Mhe. Ndejembi amewataka kujirekebisha na kufanya kazi kwa uadilifu na weledi ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima inayosababishwa na utendaji kazi wao usioridhisha.

Ameongeza kuwa, watumishi wa Idara hiyo ya ardhi wakiendelea na utamaduni wa kufanya kazi kwa kuweka maslahi binafsi mbele wataipotezea Serikali mapato na kuwanyima haki wananchi wa Mkuranga kupata maendeleo yanayotokana na kodi itayokusanywa na Serikali katika Halmashauri hiyo.

Akisisitiza uadilifu kwa watumishi hao, Mhe.Ndejembi amewataka wabadilike kwa sababu wamekuwa wakilalamikiwa kuwaonea wananchi kwa kuwaomba rushwa na kutowashauri vizuri kwenye masuala yanayohusu umiliki wa ardhi.

“Nimeambiwa hapa Mkuranga hata mimi nikihitaji shamba natakiwa kuwa na kitu kidogo cha kuwapatia watumishi wa Idara ya ardhi ambao wameweka maslahi yao binafsi mbele, na wala sitaki kumtaja mtu mmoja mmoja hapa zaidi ya kuwasisitiza mbadilike”, Mhe. Ndejembi amefafanua.

Kuhusiana na migogoro inayoibuka, Mhe. Ndejembi amewataka Watumishi wa Idara hiyo kuwa watatuzi wa migogoro badala ya kuwa chanzo cha migogoro.

Mhe. Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 


Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao wilayani Mkuranga chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 


Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe. Khadija Ali akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisikiliza hoja ya mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Halmashauri hiyo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.

 


Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Bi. Jessy Mpangala akiwasilisha changamoto ya kiutumishi inayomkabili kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwahimiza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga kutumia mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI kwa kuwasikilizisha makala fupi ya picha za mwendo (video clip) inayotoa muongozo wa namna ya kutumia mfumo huo, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri hiyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Mkuranga Bi. Mwantum Mgonja akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya halmashauri yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi wa Halmashauri hiyo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.












Thursday, December 23, 2021

WAZIRI MCHENGERWA AELEKEZA WALENGWA WA TASAF KUPEWA RUZUKU KABLA YA KRISMASI ILI WAJIPANGE KUBORESHA MAISHA YAO

Na. James K. Mwanamyoto-Kazuramimba

Tarehe 23 Desemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Waratibu wa TASAF nchini kuhakikisha walengwa wanapewa ruzuku kabla ya Sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya ili waweze kujipanga mapema kuboresha maisha yao.

Akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Kazuramimba, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Waziri Mchengerwa amesema Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo ya kuwapatia ruzuku walengwa wa TASAF mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji na uhakiki.

“Waratibu wa TASAF hakikisheni walengwa wa Kazuramimba wanalipwa kwa wakati kabla ya Krismasi ili wapange mikakati madhubuti itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi katika Mwaka Mpya unaokuja, Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Akizungumzia azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi, Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali isiyowajali walengwa wa TASAF ni sawa na Serikali isiyokuwa na huruma kwa wananchi wake na kukosa hofu ya Mwenyezi Mungu.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuzifikia kaya milioni moja na laki tano ambazo ni sawa na Watanzania milioni kumi na tano ambao watanufaika na mpango wa kuzinusuru kaya zenye uhitaji.

Waziri Mchengerwa amesema, Baba wa Taifa alisema kama Taifa hatutaweza kupiga hatua iwapo Watanzania wengi wana hali duni ya maisha na ndio maana Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kuzikwamua kaya zisizojiweza kupitia mpango wa TASAF.

Katika kuhakikisha miradi ya TASAF inatekelezwa ipasavyo, Mhe. Mchengerwa amesema akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya kumsaidia Mhe. Rais kusimamia utekelezaji wa miradi ya TASAF, atahakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kutimiza azma ya Mhe. Rais kuzifikia kaya zote zenye hali duni nchini.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara ya kikazi mkoani Kigoma yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Kazuramimba, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa wa Kigoma.


Baadhi ya wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Kazuramimba wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji hicho Mkoani wa Kigoma.


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi Mhe.Thobias Andengenye akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na wananchi wa Kazuramimba wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akielekea kukagua miradi ya TASAF iliyopo Kijiji cha Kazuramimba, akiwa na viongozi, watendaji na baadhi ya  wananchi wa Kijiji hicho wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisikiliza ushuhuda wa mlengwa wa TASAF, Bi. Hija Kaziyabure wa Kijiji cha Kazuramimba, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF  Mkoani Kigoma. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akimpongeza mlengwa wa TASAF, Bi. Tamasha Zegeli wa Kijiji cha Kazuramimba, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kwa matumizi mazuri ya ruzuku ya TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa wa Kigoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akicheza ngoma na wasanii wa kikundi cha Mapigo Tisa cha Kazuramimba mara baada ya kuwasili Kijijini hapo kwa ajili ya kuzungumza na wananchi na walengwa wa TASAF akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.



Tuesday, December 21, 2021

TASAF YAJENGA NYUMBA YA MGANGA KIJIJI CHA KAGONGO-KIGOMA KUWAWEZESHA WANANCHI KUPATA HUDUMA KWA WAKATI

Na. James K. Mwanamyoto-Kigoma

Tarehe 21 Desemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema TASAF imejenga nyumba ya Mganga katika Kijiji cha Kagongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati katika Zahanati ya kijiji hicho.

Akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Kagongo, Mhe. Mchengerwa amesema, ujenzi wa nyumba hiyo umewaondolea adha wananchi wa kijijiji hicho ya kuchelewa kupata huduma kwani Mganga aliyekuwa akiwahudumia alilazimika kusafiri takribani kilomita kumi kila siku ili kutoa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho.

“Tumefanikisha ujenzi wa nyumba hii, Mganga anaishi hapa na huduma zinatolewa kwa wakati, hii ndio dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwasogezea huduma wananchi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Serikali kupitia TASAF itaendelea kuboresha huduma za kijamii ili wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na Serikali yao kama ambavyo Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria.

Katika kuhakikisha dhamira hiyo inatekelezwa, Mhe. Mchengerwa amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kutosha kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii katika maeneo yote yenye uhitaji.

“Nataka niwatoe hofu Watanzania wenzangu waliokuwa wanafikiri mradi huu wa TASAF hautaendelea, napenda niwaambie kuwa, Rais wetu ametupatia kiasi cha shilingi trilioni 2.03 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya TASAF, hii ina maana kuwa, tutazifikia kaya zote maskini nchini ambazo hazikufikiwa na mpango katika awamu zilizopita,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Mhe. Mchengerwa anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Kigoma ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akimpongeza mlengwa wa TASAF, Bw. Luciano Miheze wa Kijiji cha Kagongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa matumizi mazuri ya ruzuku ya TASAF wakati wa  ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa wa Kigoma. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akilakiwa na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Kagongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Kagongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mbele ya nyumba ya Mganga wa Zahanati ya Kijiji cha Kagongo iliyojengwa na TASAF, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa wa Kigoma. 


Umati wa wananchi na walengwa wa TASAF wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa wa Kigoma.



Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Emmanuel Macha akitoa salam za TASAF kwa walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Kagongo wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.

Baadhi ya wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Kagongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wakiwa kwenye mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisikiliza ushuhuda wa mlengwa wa TASAF, Bw. Luciano Miheze wa Kijiji cha Kagongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa wa Kigoma. 

 

SITOWASALITI WATUMISHI WANAOCHAPA KAZI KWA BIDII, WELEDI NA UADILIFU - Mhe. Mchengerwa


 

Monday, December 20, 2021

SITOWASALITI WATUMISHI WANAOCHAPA KAZI KWA BIDII, WELEDI NA UADILIFU - Mhe. Mchengerwa

Na. James K. Mwanamyoto-Kigoma

Tarehe 20 Desemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika uongozi wake hatowasaliti katika kutetea stahiki zao Watumishi wa Umma wanaofanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na uzalendo kwa taifa lao.

Akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Mchengerwa amesema atahakikisha anasimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma nchini kwa lengo la kuwaongezea morali ya utendaji kazi kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.

Kufuatia uamuzi wake wa kusimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa watumishi wote wa umma nchini kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuendana na kasi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan badala ya kufanya kazi kwa mazoea kwani wasipowajibika hatokuwa tayari kutetea stahiki zao.

“Pale ambapo tutabaini kuna mtumishi mzembe, mla rushwa na mbadhirifu wa mali za umma sitokuwa tayari kumtetea lakini nitakuwa tayari kupambana na kumtetea mtumishi yeyote mwadilifu, mchapakazi na mzalendo kwa taifa lake muda wote asubuhi, mchana, jioni na usiku,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amewaelekeza watendaji kufuatilia utendaji kazi wa watumishi walio chini yao mara kwa mara na kumtaka kila mtumishi kuongeza ubunifu katika eneo lake la kazi ili aweze kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma nchini.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka waajiri kutenga bajeti ya mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa Umma walio katika maeneo yao ili waweze kuwa na weledi, ubunifu na kuongeza ufanisi kiutendaji.

Waziri Mchengerwa yuko kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Kigoma yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani humo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kigoma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.

Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Umma wa Umma wa Mkoa wa Kigoma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, CP Thobias Andengenye akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kigoma wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.


Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Mkoa wa Kigoma, Bw. Jumanne Tenganya akiwasilisha hoja za kiutumishi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika mkoa huo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijibu hoja za Watumishi wa Mkoa wa Kigoma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi akifafanua hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Mkoa wa Kigoma wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa na watumishi wa mkoa huo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.


 

Sunday, December 19, 2021

WAZIRI MCHENGERWA AKEMEA HUDUMA MBAYA ZINAZOTOLEWA HOSPITALI YA MKOA WA KAGERA

Na. James K. Mwanamyoto-Kagera

Tarehe 19 Desemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amekemea huduma mbaya zinazotolewa kwa wananchi katika hospitali ya Mkoa wa Kagera.

Akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, Mhe. Mchengerwa amesema, amekuwa akipokea malalamiko mengi ya wananchi wanaopata huduma katika hospitali hiyo kuhusu huduma mbaya zinazotolewa hospitalini hapo.

Kufuatia malalamiko hayo, Mhe. Mchengerwa amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Issesanda Kaniki kukutana na watumishi wa hospitali hiyo kwa lengo la kuwahimiza waboreshe utendaji kazi wao.

 “Nimepokea malalamiko mengi kupitia ujumbe mfupi na kupigiwa simu, watendaji wetu hawana lugha nzuri na utendaji kazi wao hauridhishi na kuna baadhi wanaomba rushwa kwa wananchi ili wawapatie huduma, hivyo tubadilike, turudi katika maadili ya taaluma ya kitabibu na misingi ya utoaji wa huduma bora.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayostahili katika hospitali hiyo, Mhe. Mchengerwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Kagera kuwa na utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwa lengo la kubaini changamoto wanazokutana nazo wananchi hao na kuchukua hatua stahiki.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, kutokana na huduma mbaya zinazotolewa na hospitali hiyo, inawalazimu baadhi ya wananchi kusafiri kwenda mkoa mwingine ili kupata huduma, jambo ambalo halileti taswira nzuri kwa umma na linawaondolea imani wananchi kwa serikali yao.

Amesema pamoja na kukemea kitendo hicho, atawasilisha malalamiko hayo kwenye mamlaka husika zinazosimamia taaluma za kitabibu ili nazo ziweze kufanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia taratibu zao za kitaaluma.

Mhe. Mchengerwa amehimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za kiafya zitakazoimarisha afya zao ili waweze kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisisitiza uwajibikaji kwa Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.


Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Umma wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Issesanda Kaniki akipokea maelekezo kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kuboresha utendaji kazi katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera wakati wa kikao kazi cha Mhe. Mchengerwa na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera.


Mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Bw. Ezekia Nsinkala akipokea maelekezo kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kufanya ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa katika Hopitali ya Mkoa wa Kagera, wakati wa kikao kazi cha Mhe. Mchengerwa na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera.


 

Saturday, December 18, 2021

WAZIRI MCHENGERWA AELEKEZA AFISA MANUNUZI MKUU TARURA KUONDOLEWA ILI KUPISHA UCHUNGUZI WA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA MIRADI


Na. James K. Mwanamyoto-Kagera

Tarehe 18 Desemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu-UTUMISHI, kumuondoa kwenye nafasi yake Afisa Manunuzi Mkuu wa TARURA ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha za miradi.

Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

Mhe. Mchengerwa amesema, uamuzi wa kumuondoa mtumishi huyo, unatokana na taarifa za uwepo wa mikataba mingi iliyosainiwa na baada ya muda ikafanyiwa mapitio na kuongezwa fedha jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

“Wakati uchunguzi unaendelea, Afisa Manunuzi Mkuu huyo aripoti Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora siku ya Jumatatu tarehe 20 Desemba, 2021 na apelekwe Afisa mwingine atakayetekeleza majukumu yake,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Aidha, amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kupitia mikataba yote ya TARURA na kuchukua hatua stahiki pale itakapothibitika kuna ubadhirifu wa fedha.

“Namuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwenda TARURA kupitia mikataba yote kwa makini ili achukue hatua stahiki kwa watendaji ambao wanashiriki vitendo vya ubadhirifu vinavyokwamisha taifa kusonga mbele,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amesema kama taifa, ni lazima kufanya maamuzi magumu pale inapobidi ili nchi iweze kupiga hatua katika maendeleo na wananchi wanufaike.

Amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipofungua fursa za kiuchumi katika utekelezaji wa miradi ya serikali, alitaka taifa lipige hatua katika maendeleo na sio watu wafanye ubadhirifu wa fedha za umma, hivyo tumuunge mkono kwa kupinga vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, Watumishi wa Umma hawana sababu ya kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ubadhirifu kwasababu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anajali maslahi yao na yeye ni msikivu kwa watumishi.

Mhe. Mchengerwa amefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Kagera ambapo amezungumzat na watumishi, walengwa wa TASAF na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kagera.


Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Umma wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kagera.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijadiliana jambo na   Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi wakati wa kikao kazi cha Mhe. Mchengerwa na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akifafanua hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Mkoa wa Kagera wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa mkoa huo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.


Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa na watumishi wa Mkoa wa Kagera kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitunuku cheti cha utambuzi wa utendaji kazi mzuri kwa mtumishi wa Mkoa wa Kagera, Bi. Maria Valentine-Msaidizi wa Kumbukumbu Daraja la II, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kagera.


 

HAKUNA MRADI ULIONZISHWA NA SERIKALI YA AWAMU YA TANO UTAKAOSHINDIKANA KUTEKELEZWA NA SERIKALI YA AWAMU YA SITA


Na. James K. Mwanamyoto-Chato

Tarehe 18 Desemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hakuna mradi ulionzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano utakaoshindikana kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Nyabilezi wilayani Chato, Mhe. Mchengerwa amewaeleza wananchi hao kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukamilisha utekelezaji wa miradi yote iliyoanzishwa na mtangulizi wake.

Mhe. Mchengerwa amewasisitiza wananchi hao kufikisha ujumbe kwa wananchi wengine katika maeneo mbalimbali juu ya dhamira hiyo, hivyo waunge mkono jitihada za Mhe. Rais kwa manufaa ya taifa.

Amesema pamoja na dhamira yake ya kukamilisha miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yeye binafsi ametenga fedha ya kutosha kuanzisha miradi mingine ya kuwanyanyua kiuchumi wananchi wa kawaida.

“Mhe. Rais Samia ametenga kiasi cha shilingi bilioni 130 za kuwezesha kuwanyanyua kiuchumi wananchi wa mikoa mitano ikiwemo Geita,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewasisitiza wananchi wa Wilaya ya Chato kuibua miradi itakayotatua changamoto za kijamii ili iweze kutekelezwa na Serikali kupitia fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

“Mhe. Rais Samia amesema fedha anazo za kutosha, hivyo ni jukumu lenu Wanachato kuibua miradi itakayoboresha huduma katika sekta ya elimu, afya na miundombinu ya barabara,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Geita yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Chato, mkoani Geita.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishiriki shughuli za ujenzi wa karo kwenye Zahanati ya Nyabilezi iliyojengwa kwa ufadhili wa TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Chato, mkoani Geita. Anayeshirikiana naye ni Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Nyabilezi, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani Chato mkoani Geita.


Walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Nyabilezi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Chato, mkoani Geita.