Na. Lusungu Helela - MWANZA
Amesema
kumekuwa na kasumba iliyojengeka kwa Watendaji wengi wa Serikali ya kuwaona
Wakaguzi hao wa Ndani kama sio Watumishi na wapo pale kwa ajili ya kuharibu
mipango yao ilhali wao ni watu muhimu na jicho la Taasisi.
Mhe.Simbachawene
ametoa kauli hiyo leo Machi 24, 2025 jijini Mwanza wakati akimwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano
wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Umma.
Amesema
Mtendaji yeyote wa Serikali anayewatumia vizuri Wakaguzi wa Ndani
hawezi kuingia kwenye matatizo ya ubadhirifu wa fedha za umma huku akisisitiza
kuwa Wakaguzi hao wapo kwa ajili ya kumsaidia yeye na Taasisi anayoiongoza.
"Acheni
kuwaona Wakaguzi wa Ndani kama wageni na watu wasiotakiwa kwenye maeneo yenu ya
kazi badala yake watumieni ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa
ajili ya miradi ya maendeleo iliyokusudiwa.
Amesema
Wakaguzi wa ndani wanatekeleza jukumu nyeti la kuhakikisha fedha za umma
zinatumika kwa busara, uwazi na kwa madhumuni sahihi. " Bila kazi yenu,
serikali haiwezi kufanya kazi kwa ufanisi" amesisitiza Simbachawene .
Katika hatua
nyingine, Mhe.Simbachawene amewataka Wakaguzi hao kuhakikisha wanapata mafunzo
ya mara kwa mara ili waweze kuendana na mabadiliko ya matumizi ya kidijitali
katika ukaguzi wa fedha hususani katika matumizi ya akili mnemba (AI).
Ameongeza
kuwa '' Dunia inabadilika, teknolojia imeleta mageuzi ya jinsi
tunavyofanya kazi, na kwa hiyo ukaguzi wa ndani na vyombo vya usimamizi wa
taasisi navyo vinapaswa kubadilika.
Amesema
matumizi ya mifumo hiyo imechangia mageuzi makubwa kwenye taasisi za serikali
yenye hatua kubwa zaidi dhidi ya wanaobainika na matumizi mabaya ya fedha za
umma.
Ameongeza
kuwa kesi vikubwa zimechunguzwa na viongozi waliothibitika kuhusika,
wameachishwa kazi, wameshtakiwa na fedha zilizochotwa wamezirejesha, akisema
huo ni ujumbe wa wazi kwamba utumishi wa umma ni kuwatumikia watu na sio
wa kujinufaisha.
Amesema
Serikali imedhamiria kuwa na mfumo wa kuhakikisha rasilimali
zinasimamiwa ipasavyo.
Kwa upande
wake, Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani, Dkt. Zelia Njeza amesema
mahudhurio ya Wakaguzi wa Ndani ni mazuri lakini kwenye ngazi ya
Halmashauri yamekuwa hafifu hali inayochangia wataalamu hao kukosa mafunzo na
hivyo kuendelea kufanya makosa yale yale kwenye kaguzi zao.
Amesema
mkutano huo utafanyika kwa muda wa siku tano ambapo zaidi ya washiriki 800
watajifunza mbinu mbalimbali za ukaguzi ikiwemo matumizi ya akili mnemba
kwenye ukaguzi na hii inatokana na mabadiliko makubwa yanayotokea duniani kote
katika ukaguzi wa fedha za umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akikabidhiwa tuzo ya kuthamini mchango kwa Wakaguzi wa ndani kutoka kwa Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani, Dkt. Zelia Njeza wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kufungua Mkutano wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Umma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akizungumza wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kufungua Mkutano wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Umma



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene (katikati) akiwa ameongoza na baadhi ya wenyeji wa Mkutano wa tatu wa Wakaguzi wa Ndani kwa ajili ya kufungua mkutano huo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan unaofanyika jijini Mwanza. Kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema , Mhe. Senyi Ngaga na kushoto ni Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani, Dkt. Zelia Njeza