Wednesday, November 22, 2023

MHE. RIDHIWANI KIKWETE AFURAHISHWA NA MIRADI YA TASAF IRINGA


Na. Lusungu Helela- Iringa 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Mhe Ridhiwani Kikwete ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa usimamizi mzuri katika utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF.

Amesema kupitia usimamizi mzuri wa utelekezaji wa miradi hiyo, TASAF imeweza kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika kaya za walengwa pamoja na wananchi katika maeneo ya utekelezaji.

Mhe Ridhiwani amesema hayo mkoani Iringa wakati akizungumza na Walengwa wa Tasaf  wa Kata ya Ruaha iliyopo katika Manispaa ya Iringa  mara baada ya kukagua daraja lilojengwa katika eneo la Kingemgosi  ikiwa ni utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na TASAF.

Kwa mujibu wa taarifa ya TASAF mkoa wa Iringa inaonesha kuwa jumla ya miradi 474 ikiwemo uchimbaji wa visima vya asili, utengenezaji wa barabara, uzibaji wa makorongo na kuanzishwa kwa mashamba ya korosho ilitekelezwa kati ya Julai 2022 na Juni 2023.

Pia,  mkoa ulipokea  jumla ya  shilingi  bilioni 10.3, kati ya hizo shilingi bilioni 8.9 zilitolewa kwa Walengwa 30,988 kutoka vijiji 585 wakati shilingi  bilioni 21.6 zilikuwa ni kwa ajili ya usimamizi  ngazi ya mkoa na halmashauri.

“Nimefarijika sana kwa namna shughuli za TASAF zinavofanyika hapa katika mkoa wa Iringa likiwemo daraja lililojengwa katika eneo la Kigenamgosi,  haya ni matokeo ya ushirikiano thabiti kati ya uongozi wa mkoa na watendaji wote wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii,” amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Oscar Maduhu amewahakikishia na walengwa wa TASAF kuwa waendelea kubuni miradi ya kimaendeleo kwani serikali imetanga jumla ya Sh. 51 bilioni kwa ajili ya Walengwa hao.

 “TASAF inaendelea kuhakikisha walengwa wote wanahudumiwa ipasavyo ili kuwaondoa katika hali ya umasikini uliokithiri kupitia ruzuku,miradi ya ajira za muda pamoja na kuwapa elimu ya kuweka na kukopa katika vikundi mbalimbali,” alisema Maduhu.

Awali, Mkuu wa wilaya ya Iringa Mjini, Mhe. Veronika Kessy amesema mpango wa TASAF umesaidia kuinua hali za uchumi kwa walengwa pamoja na kuchechemua biashara mbalimbali kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Amesema, utoaji fedha za Mpango umewezesha kaya za walengwa kuboresha makazi na kujenga nyumba za matofali ya kuchoma na kuezeka kwa bati badala ya nyasi.

“Hadi kufikia mwezi Juni 2023, jumla ya walengwa 918 wa TASAF katika mkoa wa Iringa waliweza kuboresha makazi yao,” amesema.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF) mara baada ya kukagua daraja lilijengwa na wanufaika hao kataika eneo la Kinegamgosi, Kata ya Ruaha mkoani Iringa
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Iringa wakikagua daraja lilijengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)  wanufaika hao katika eneo la Kinegamgosi, Kata ya Ruaha mkoani Iringa
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Oscar Maduhu akizungumza  wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)     mara baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete  kuzungumza nao.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa , Mhe. Rita Kabati akizungumza  wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)     mara kabla ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete  kuzungumza nao.
Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini , Mhe. Jesca Msambatavangu akizungumza  wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)     mara kabla ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete  kuzungumza nao.


 Sehemu ya wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF) wakifurahia jambo wakati Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akizungumza nao katika kata ya Ruaha iliyopo katika Manispaa ya Iringa

 


No comments:

Post a Comment