Na. Rainer Budodi na Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 20 Novemba, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka Viongozi wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kutafakari kwa kina na kujadili changamoto
zinazowakabili katika utendaji kazi na kuzifanya kuwa fursa kwa maendeleo ya
Taifa.
Mhe. Simbachawene amesema hayo leo tarehe 20 Novemba,
2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU-2023 katika
ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma.
“Ninaamini mtatumia fursa ya mkutano huu wa mwaka kujadili
masuala yote yanayoonekana kuwa ni changamoto katika utendaji kazi ili kupata
suluhu ya pamoja” ameongeza Mhe. Simbachawene.
Aidha, katika hotuba yake amebainisha kuwa kila mmoja katika
mazingira tofauti na kwa namna ya pekee ameruhusu au ameathiriwa na rushwa,
hivyo ametoa rai kwa wananchi wote kuhakikisha wanazuia mianya ya rushwa ili kutoathiri
vizazi vijavyo.
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa TAKUKURU inatakiwa kuitumia
vizuri programu iliyoianzisha ya TAKUKURU Rafiki kwa lengo la kupanua wigo na
kuwashirikisha wananchi katika kupambana na rushwa.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi
Salum Hamduni amesema ofisi yake inaendelea na utekelezaji wa shughuli zake kwa
mujibu wa Sheria na sasa wamejikita zaidi katika kuzuia rushwa.
“Tunaendelea na kazi ya kuelimisha umma kuhusu masuala
ya rushwa na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Serikali ambapo tumeokoa fedha
nyingi ambazo kama isingekuwa TAKUKURU basi fedha hizo zingeishia mikononi mwa
watu binafsi” amesema Bw. Hamduni.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU
hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubainisha changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi wao na
kutafuta ufumbuzi wa pamoja.
Mkutano huu wa Mwaka kwa mwaka 2023 una kaulimbiu ya Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Viongozi wa TAKUKURU wakati
akifungua Mkutano Mkuu
wa Mwaka 2023 wa Viongozi hao
jijini Dodoma.
Sehemu ya Viongozi wa TAKUKURU na Wawezeshaji wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu
wa Mwaka 2023 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU, Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni akitoa taarifa fupi ya utekelezaji
wa majukumu ya ofisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu
wa Mwaka 2023 wa Viongozi wa
Taasisi hiyo uliofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi,
Salum Hamduni akimkabidhi Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene tuzo
ya kuthamini mchango wake katika mapambano dhidi ya rushwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 wa Viongozi wa Taasisi hiyo uliofanyika
jijini Dodoma.
Naibu Mkurugenzi
Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye akitoa
neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu
wa Mwaka 2023 wa Viongozi wa
TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana
na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa St. Gasper
jijini Dodoma kwenye ufunguzi
wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023
wa Viongozi wa TAKUKURU. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule.
No comments:
Post a Comment