Wednesday, November 15, 2023

MHE. SIMBACHAWENE ARIDHISHWA NA UJENZI WA OFISI ZA TAKUKURU NA TUME YA UTUMISHI WA UMMA JIJINI DODOMA

 Na. Rainer Budodi na Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 15 Novemba, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewasisitiza wakandarasi wanaojenga majengo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (TAKUKURU) na Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba.

Mhe. Simbachawene amesema hayo kwa nyakati tofauti leo tarehe 15 Novemba, 2023 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo jijini Dodoma.

Aidha, Mhe. Simbachawene amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi na kwa wakati kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi kwa taasisi zilizo chini ya ofisi yake.

“Majengo haya yameanza kujengwa wakati Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani na kulikuwa na mtikisiko wa uchumi na majanga mbalimbali duniani lakini hakusitisha kuleta fedha za ujenzi wa majengo haya. Hivyo, hatuna budi kuendelea kumuombea dua na sala ili aendelee kutuongoza kwa hekima na busara” amesema Mhe. Simbachawene.

Pia, amewapongeza TAKUKURU kwa ubunifu wa kulipa Mkandarasi kwa mfumo wa milestone lengo likiwa ni kuimarisha mtiririko wa fedha kwa mkandarasi kulingana na kazi inavyofanyika na kutoa fursa ya kukamilisha jengo kwa wakati.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema kwa kibali cha mamlaka ya bajeti, Mshitiri ameridhia malipo ya mkandarasi yafanyike kwa kutumia utaratibu wa milestone  badala ya kutumia utaratibu wa vyeti vya malipo ya mpito (interim payment certificates) ili kukamilisha mradi wa ujenzi ifikapo Julai, 2024.

Kamishna Hamduni ameongeza kuwa, mpango wa kutumia utaratibu wa malipo kwa milestone utaanza tarehe 4 Disemba, 2023 na utatoa fursa kwa mkandarasi kulipwa kiasi cha fedha kulingana na kazi alizopanga kuzifanya na kuzikamilisha kwa asilimia 100.

Katika hatua nyingine, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Simbachawene amesema katika kipindi cha miezi kumi (10) mkandarasi ambaye ni Kampuni ya CRJE (East Africa) amefanya kazi kubwa, kwa haraka na ufanisi ya ujenzi wa ofisi hiyo.

“Ninawasisitiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kusimamia kwa ukamilifu ujenzi huu ili jengo likamilike kama linavyoonekana kwenye mchoro wa jengo hili” amesema Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama amesema ujenzi huo unajumuisha ujenzi wa jengo la sakafu sita (6), nyumba ya mlinzi, chumba cha kuhifadhi mitambo ya umeme, kibanda cha kukusanya taka, ujenzi wa uzio na utengenezaji wa mandhari ya nje ya jengo ambapo hadi sasa mkandarasi amefikia asilimia 50 ya kazi zote.

Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma ulianza terehe 12 Januari, 2023 na Mkadarasi akiwa ni Kampuni ya CRJE (East Africa) na kwa mujibu wa  mkataba anatakiwa kukabidhi jengo hilo ifikapo Septemba, 2024.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akisikiliza maelezo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya TAKUKURU kutoka kwa Mhandisi Stephano Mlacha kabla ya Waziri huyo kuanza kukagua jengo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Dodoma.

Sehemu ya watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo jijini Dodoma


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na watendaji wa ofisi hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo jijini Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akielekea kukagua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akitazama ubora wa vitendea kazi vinavyotumika katika ujenzi wa mradi wa Ofisi ya TAKUKURU wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi huo jijini Dodoma.


Mwonekano wa jengo jipya la Ofisi ya TAKUKURU jijini Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wakandarasi na watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma wakati wa kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akitazama michoro ya jengo la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo jijini Dodoma. Anayetoa maelezo ni Mbunifu Majengo kutoka TBA, Bw. Kelvin Chuma.


Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa maelezo ya awali kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kabla ya Waziri huyo kuanza kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akipokelewa na watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma mara baada ya kuwasili katika eneo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma mara baada ya kuhitimisha ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama. Wengine ni wakandarasi wanaojenga jengo hilo.


Mwonekano wa jengo jipya la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma ambalo ujenzi wake unaendelea jijini Dodoma



No comments:

Post a Comment