Na. Veronica Mwafisi-Morogoro
Tarehe 26 Novemba, 2023
Ofisi ya Rais-UTUMISHI kupitia Idara ya Uendelezaji
Sera imetoa mafunzo kwa
waratibu na waelimisha rika wa Wizara, Mikoa na Taasisi za umma kwa lengo la kuwajengea uwezo na stadi za
utekelezaji wa afua kwa ajili ya kuwalinda watumishi wa umma dhidi
ya VVU na Ukimwi.
Katika mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi Anuai
za Jamii na Mratibu wa VVU, Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukiza, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Bi. Mwanaamani Mtoo amesema Ofisi ya
Rais-UTUMISHI inaungana na Rais, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kutokomeza VVU na Ukimwi ili
kuendelea kuwa na nguvukazi hususani katika utumishi wa umma yenye afya njema
ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Bi. Mtoo ameongeza kuwa mafunzo haya ni endelevu
kwa kuwa ni sehemu ya mapambano dhidi
ya VVU na Ukimwi
ili kuwalinda watumishi wa umma na kuhakikisha taifa linaondokana na vifo vitokanavyo na Ukimwi ifikapo mwaka 2030.
“Tunatoa mafunzo haya kwa waratibu na waelimisha
rika wa Wizara, Mikoa na Taasisi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi ili
waende kutoa elimu ya kudhibiti VVU na Ukimwi mahali pa kazi katika Utumishi wa
Umma” amefafanua Bi. Mwanaamani.
Naye, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mratibu
wa VVU na Ukimwi kutoka Hospital ya Rufaa ya Tumbi-Pwani, Dkt. Hapiness Ruta
ameishukuru Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kutoa mafunzo hayo ya VVU na Ukimwi na
kuahidi kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watumishi wa umma waliopo katika maeneo yao ya kazi.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, kupitia Idara ya Uendelezaji Sera ipo mkoani Morogoro kwenye Maadhimisho ya Siku ya
Ukimwi Duniani yanayofanyika kitaifa mkoani humo kuanzia tarehe 24 Novemba hadi
tarehe 02 Disemba, 2023. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni Jamii iongoze
kutokomeza Ukimwi.
Mkurugenzi Msaidizi Anuai
za Jamii na Mratibu wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Bi. Mwanaamani Mtoo akielezea madhumuni ya kikao
kazi cha kuwajengea uwezo waratibu
na waelimisha rika wa Wizara, Mikoa na Taasisi wakati wa maadhimisho ya Siku ya
Ukimwi yanayofanyika Kitaifa mkoani Morogoro.
Afisa Ustawi
wa Jamii Mwandamizi na Mratibu wa kitaifa wa kudhibiti VVU, UKIMWI na MSY, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Bi. Juliana
Ntukey akiwasilisha mada kuhusu sababu za kuwepo kwa Afua za VVU, UKIMWI na MSY
mahali pa kazi wakati
wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi yanayofanyika Kitaifa mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi Anuai
za Jamii na Mratibu wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Bi. Mwanaamani Mtoo akiwa katika picha ya pamoja
na waelimisha rika wa Wizara,
Mikoa na Taasisi mara baada ya kuhitimisha kikao kazi wakati wa Maadhimisho ya
Siku ya Ukimwi yanayofanyika Kitaifa mkoani Morogoro.
No comments:
Post a Comment