Tuesday, November 28, 2023

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAIBUKA NA USHINDI KATIKA MBIO ZA NYIKA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI

 Na. Veronica Mwafisi-Morogoro

28 Novemba 2023.  

Watumishi wawili wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora waibuka na ushindi katika mbio za Nyika zilizoandaliwa kwa lengo la kuhamasisha uchangiaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za VVU na Ukimwi hapa nchini.

Katika mbio hizo Bw. Kokolo Lusanda ambaye alishiriki mbio za kilometa 5 aliibuka mshindi wa pili na Bi. Juliana Ntukey aliibuka mshindi wa nne katika mbio za kilometa 10.

Bw. Kokolo amesema kuwa mashindano hayo ya mbio za nyika  yamemuongezea ari ya kuendelea kufanya mazoezi na kushiriki katika mashindano mengine yatakayoshirikisha watumishi wa umma kwa kuwa raha ya ushindi ni kuendelea kushiriki na kushinda katika mashindano mengine.

Naye Bi. Juliana alibainisha kuwa mbio za nyika zilikuwa na ushindani mkubwa lakini jitihada zake za kumalizia kama vile ndio anaanza mbio zimemfanya kuwapita wenzake na kupata nafasi hiyo ya nne kwa kishindo.

“Nimefarijika sana kuwa mshindi kwa nafasi ya nne sio haba na kwa mwaka ujao nitaongeza juhudi kubwa ili niweze kushika nafasi ya kwanza kwa kudra za Mwenyezi Mungu” alisema Bi Juliana.

Aidha, washindi hao wameishukuru Menejimemti ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kutoa kibali kwa watumishi wake kushiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambapo wametumia fursa hiyo kushiriki katika mashindano hayo yaliyoandaliwa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, 2023 yanayofanyika Kitaifa Mkoani Morogoro na kuibuka  washindi.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia Idara ya Uendelezaji Sera ipo mkoani Morogoro kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanayofanyika kitaifa mkoani humo ambapo sehemu ya watumishi wake wameshiriki katika mbio hizo za nyika na kuibuka washindi.

Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii na Mratibu wa VVU, Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukiza, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Mwanaamani Mtoo akimpongeza mtumishi wa ofisi hiyo Bw. Kokolo Lusanda aliyepata ushindi wa pili katika mbio za Km. 5 wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani, 2023 yanayoendelea mkoani Morogoro.


Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakishiriki mbio za nyika zinazofanyika mkoani Morogoro. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii na Mratibu wa VVU, Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukiza, Bi. Mwanaamani Mtoo.


Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakifurahia jambo mara baada ya kuhitimisha mbio za nyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani, 2023 yanayoendelea mkoani Morogoro.



No comments:

Post a Comment