Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 30 Julai, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama ameiasa
Tume ya Utumishi wa Umma kusimamia haki wakati wa kutoa maamuzi ya mashauri ya kinidhamu
ya watumishi wa umma yaliyowasilishwa ili kutolewa maamuzi.
Mhe. Jenista ametoa nasaha
hizo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na Makamishna wa Tume ya Utumishi
wa Umma, kilichofanyika ofisini kwake kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika
Tume ya Utumishi wa Umma.
Mhe. Jenista ameitaka Tume ya
Utumishi wa Umma kutoa maamuzi ya mashauri yote ya kinidhamu kwa kuzingatia
haki, kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma
iliyopo.
Waziri Jenista ameongeza kuwa,
Tume isipo yashughulikia mashauri ya kinidhamu kwa haki na wakati, inakwamisha
maendeleo ya nchi yasipatikane kwa wakati na ndio maana Serikali imekuwa ikiihimiza
Tume ya Utumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao kwa wakati na kwa kutenda haki.
“Jambo la msingi hakikisheni haki inatendeka
katika mashauri ya kinidhamu, mkifanya hivyo mtakuwa mnasimamia na kujenga
nidhamu nzuri ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Aidha, Mhe. Jenista
amezungumzia changamoto ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumishi wa umma unaofanywa na baadhi ya
waajiri na watumishi, hivyo amewataka Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma kufanyia
kazi changamoto hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe.
Balozi John Haule amemshukuru Mhe. Jenista Mhagama kwa kuwahimiza
kutenda haki wakati wa kushughulikia mashauri ya kinidhamu na kumuahidi kuwa
watatoa maamuzi ya mashauri ya kinidhamu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu
na Miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma.
Tume ya Utumishi wa Umma imeundwa
chini ya kifungu Na. 9 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298. Tume
hii ina jukumu la kufuatilia na kusimamia uendeshaji wa shughuli za
rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Utumishi
wa umma unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Jenista Mhagama akizungumza na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma (hawapo
pichani) wakati wa kikao kazi chake na Makamishna wa Tume hiyo chenye lengo la
kuhimiza uwajibikaji.
Makamishna
wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (meza kuu
katikati) wakati akizungumza nao kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Naibu
Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akitoa neno la utangulizi kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza
na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji (Mst.)
Hamisa Kalombola akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi
wa Umma kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kabla ya Waziri huyo kuzungumza na Makamishna
wa Tume hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Kamishna
wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Balozi
John Haule akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama mara baada
ya Waziri huyo kuzungumza nao kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Katibu
wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akiwatambulisha Makamishna wa
Tume ya Utumishi wa Umma (hawapo pichani) kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kabla ya
Waziri huyo kuzungumza na Makamishna wa Tume hiyo kwa lengo la kuhimiza
uwajibikaji.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna
wa Tume ya Utumishi wa Umma, mara baada ya kuzungumza na makamishna hao kwa lengo
la kuhimiza uwajibikaji.