Na. James
K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 27 Oktoba, 2021
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Abdallah Chaurembo ameipongeza
Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kubuni mifumo ya utoaji
huduma kwa wananchi na kutatua kero zinazowakabili pindi wanapohitaji huduma
katika taasisi za umma.
Mhe. Chaurembo ametoa pongezi hizo leo
wakati wa kikao kazi cha kamati yake na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika katika Kituo cha Utafiti na
Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.
Mhe. Chaurembo amesema, kamati yake
inaridhika na utendaji kazi wa Ofisi hiyo hasa katika kubuni mifumo ya TEHAMA
inayosaidia kuondoa malalamiko ya wananchi.
Mhe. Chaurembo amesema kamati yake
itaendelea kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora na kuwasisitiza wajumbe wa kamati yake kutoa elimu ya matumizi
ya mifumo hiyo kwa wananchi wanapokuwa kwenye maeneo yao ya utawala.
“Mambo mazuri sana yamefanywa na Ofisi
hii pamoja na taasisi zake, hasa hili la kubuni mifumo ya TEHAMA inayoondoa
malalamiko, hivyo wajumbe wa kamati hii tuwasaidie kutoa elimu ya umuhimu wa
mifumo hii kwa wananchi, tuwasisitize wananchi watumie mifumo hii kuondoa
malalamiko,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.
Akitoa neno la utangulizi, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa amesema, Serikali kupitia wataalam wa ndani wa Mamlaka ya
Serikali Mtandao (eGA) imekuwa ikibuni mifumo mbalimbali kwa lengo la kusogeza
huduma za Serikali karibu na wananchi na kuwaweka wananchi karibu na Serikali
yao.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa Ofisi
yake iliona ni vema kufanya ubunifu wa kutengeneza mifumo ya TEHAMA ya utoaji
huduma kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili Watumishi
wa Umma na wananchi kwa kipindi cha muda mrefu.
Akifafanua jinsi mfumo mmojawapo
uliobuniwa na wataalam hao ujulikanao kwa jina la Sema na Waziri wa UTUMISHI
unavyofanya kazi, Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo huu unamuwezesha mwananchi kuwasilisha
kero au lalamiko lake moja kwa moja kwake na kulifanyia kazi.
Mhe. Mchengerwa amewaomba Wajumbe wa
Kamati ya USEMI kutoa elimu ya faida za mfumo huu kwa watumishi na wananchi
katika maeneo yao ili utumike kutatua changamoto zinazowakabili.
“Mkiwa kama wawakilishi wa wananchi,
tunaomba mtusaidie kupeleka ujumbe kwa wananchi kuhusu faida za mfumo huu kwani
tunataka kupunguza kabisa malalamiko na kutatua changamoto za kiutumishi
zinazowakabili Watumishi wa Umma kwa muda mrefu.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa
ameishukuru kamati kwa kuiongoza na kuishauri vema ofisi yake na kuahidi
kuendelea kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na kamati hiyo kwa maslahi ya
taifa.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Mhandisi
Benedict Ndomba amesema Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali
Mtandao kimelenga kwenye ubunifu na utafiti
katika TEHAMA ili kuwa na mifumo itakayoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhandisi Ndomba amesema falsafa ya Kituo hicho ni kutumia wataalam wa ndani katika kujenga mifumo hiyo ya TEHAMA ili kuweza kutatuta matatizo yetu wenyewe.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akiongoza
kikao kazi cha kamati yake na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora wakati wa ziara ya kamati hiyo kwenye Kituo cha Utafiti
na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika kwenye Kituo cha
Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali
Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
majukumu ya taasisi yake kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika kwenye
Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Utawala na Serikali za Mitaa wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa Mamlaka
ya Serikali Mtandao iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo,
Mhandisi Benedict Ndomba wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika
kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini
Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Saasisha Mafuwe akiwasilisha hoja wakati wa
kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha
Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akiwa katika
picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati yake na Watendaji wa Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mara baada ya kuhitimisha ziara
ya kamati hiyo kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali
Mtandao jijini Dodoma.