Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 09 Septemba, 2021
Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni 2.03 kwa ajili ya kuzikwamua kaya
zote maskini nchini kutoka katika lindi la umaskini ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kipindi cha Pili cha
Awamu ya Tatu ya TASAF kilichoanza 2020 mpaka 2023.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa wakati wa semina ya kuwajengea
uwezo Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa
kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini iliyofanyika leo
katika ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.
Mhe. Mchengerwa amesema, kwa kuwa Serikali imetenga fedha
za kutosha kuzifikia kaya zote maskini, amewaomba wajumbe wa kamati hiyo
kufanya ufuatiliaji ili kaya zote maskini zinazostahili kupata ruzuku
zinanufaika.
“Kama kuna kaya yoyote maskini imesahaulika, nawaomba mtupatie
taarifa haraka ili watendaji wetu wazifikie na kukamilisha taratibu za
kuwawezesha kupata ruzuku na kuongeza kuwa, katika utekelezaji wa awamu hii,
Serikali itahakikisha kila Mtanzania anayestahili kunufaika na mpango huu,
anapata ruzuku,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema licha ya TASAF kuziwezesha
kaya maskini kiuchumi, pia imewawezesha watoto wa kike wanaotoka kwenye kaya
hizo maskini kupata elimu kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu
ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) ameipongeza
Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa azma yake ya kutenga
fedha za kutosha kuziwezesha kaya zote maskini nchini.
Mhe. Polepole amesema, azma ya Mhe. Samia ya kutenga
fedha hizo inaonesha nia ya dhati ya Serikali yake na Watendaji wake ya
kuzikwamua kaya zote maskini.
Akiwasilisha mada kwa kamati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa
TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga amesema, idadi ya kaya za walengwa katika utekelezaji
wa Mpango wa TASAF, Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu inatarajiwa kufikia
milioni moja laki nne na nusu, hivyo wanufaika kwenye kaya hizo watakuwa zaidi
ya watu milioni 10.
Bw. Mwamanga amesema, ofisi yake imetekeleza zoezi la
utambuzi wa kaya maskini kwa kushirikisha jamii na viongozi katika maeneo
husika ili kutatua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa awamu
iliyopita.
Katika kuhakikisha hakuna udanganyifu wakati wa zoezi la uandikishaji wa kaya maskini, Watendaji wanaohusika na zoezi hilo wamesainishwa kiapo cha kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitoa neno la
utangulizi wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyofanyika kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akitoa neno
la utangulizi wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa Wajumbe wa Kamati ya Bunge
ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa LAPF
jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya
Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akizungumza wakati wa
Semina ya kuwajengea uelewa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
iliyofanyika kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma. Kushoto
kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Baadhi ya Watendaji wa Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakimsilikiza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) (hayupo
pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa
majukumu ya TASAF
iliyofanyika kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF), Bw.
Ladislaus Mwamanga akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyofanyika
kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wakisikiliza mada kuhusiana na
utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyowasilishwa
kwao na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga (hayupo pichani).
No comments:
Post a Comment