Na. James K. Mwanamyoto-Dar es
Salaam
Tarehe 03 Septemba, 2021
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa amewatahadharisha Watumishi wa Umma, wastaafu na wananchi
kuwa makini na matapeli wanaotumia simu za viganjani kujipatia fedha kwa
ulaghai kwa lengo la kuwasaidia katika masuala ya kiutumishi.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amesema matapeli
hao wamekuwa wakitumia majina ya Viongozi mbalimbali wa Kiserikali na Kisiasa kwa
kuwapigia simu Watumishi wa Umma na wastaafu na kuwataka watoe taarifa zao za
kiutumishi ili wawasaidie kuwapandisha madaraja, kuwateuwa kwenye nafasi za
uongozi, kuwapatia ajira na masuala mengine ya kiutumishi.
Mhe.
Mchengerewa amewataka wananchi na wadau wote wa masuala ya kiutumishi kuacha
kutoa taarifa zozote zinazoombwa na mtu yeyote kwa njia ya simu kwani Serikali
inao utaratibu wa kuwasiliana na wadau wake pindi inapohitaji taarifa za
kiutumishi kwa ajili ya kuzifanyia kazi.
“Kutoa
taarifa kiholela si vizuri kwani zinaweza kutumika visivyo na kumsababishia matatizo
aliyetoa taarifa hizo,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe.
Mchengerwa ameongeza kuwa, yawezekana matapeli hao wanapata fursa ya kufanya
uhalifu huo kutokana na baadhi ya Viongozi na Watendaji kutofikika kiurahisi
pindi wadau wanapohitaji huduma, hivyo amewataka Viongozi na Watendaji hao
kuacha urasimu usiokuwa na tija.
Katika
kusogeza huduma karibu na wananchi, Mhe. Mchengerwa amewataka wadau ambao
wanahitaji ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi kupiga simu namba
026-216-0240 ya kituo cha mawasiliano (Call Centre) cha ofisi yake na namba
026-2160-210 ya kituo cha mawasiliano cha Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Aidha, Mhe.
Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi na wadau wa masuala ya kitumishi kutoa
taarifa za matapeli kwenye ofisi yake na vyombo vya dola ili zisaidie
kukabiliana na tatizo hilo.
Mhe. Mchengerwa
ametoa onyo kali kwa matapeli hao kwani Serikali kupitia vyombo vya dola inaendelea
kufuatilia nyendo zao ili kuwabaini na hatimaye kuwachukulia hatua kwa mujibu
wa sheria zilizopo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo
Jijini Dar es Salaam juu ya utapeli unaofanywa kwa Watumishi wa Umma na
Wastaafu. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utawala wa Utumishi wa Umma, Bw. Mathew
Kirama.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo Jijini Dar es Salaam juu ya utapeli unaofanywa kwa Watumishi wa Umma na Wastaafu.
Mkurugenzi
wa Utawala wa Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akimkaribisha Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa kuzungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam juu ya
utapeli unaofanywa kwa Watumishi wa Umma na Wastaafu.
No comments:
Post a Comment