Na Veronica Mwafisi-DODOMA
Tarehe 29, Septemba, 2021
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma nchini kuutumikia umma kwa
uzalendo, uadilifu na weledi ili kutimiza azma ya Serikali ya kutoa
huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo
wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha taasisi simamizi za maadili na vyama
vya kitaaluma chenye lengo la kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa maadili, kilichofanyika
katika ukumbi wa Ofisi ya RaiS-UTUMISHI Mtumba, jijini Dodoma.
Dkt. Ndumbaro amesema uzalendo,
uadilifu na utendaji kazi unaozingatia weledi ndio nguzo kuu ya utendaji kazi wa
Watumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na ustawi wa taifa.
Ameongeza kuwa, ofisi yake imekuwa
na utamaduni endelevu wa kushirikiana na taasisi zinazosimamia maadili na vyama
vya kitaaluma ili kujenga taifa imara lenye Watumishi wa Umma wazalendo na waadilifu.
“Ushirikiano uliopo kati ya ofisi
yangu na taasisi simamizi za maadili na vyama vya kitaaluma, utasaidia kujenga uadilifu
kwenye utumishi wa umma na jamii kwa ujumla”, Dkt. Ndumbaro amefafanua.
Dkt. Ndumbaro amesema, Watumishi
wa Umma nchini wanao wajibu wa kuunga mkono kwa vitendo azma ya Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan ya kuujenga Utumishi wa Umma kuwa wenye kuzingatia uadilifu,
uwajibikaji, Kanuni, Sheria, Taratibu na miongozo iliyopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Leila Mavika amesema lengo
kuu la kikao kazi hicho ni kukumbushana uzingatiaji wa maadili, kujadili changamoto
za usimamizi wa maadili katika Utumishi wa Umma na kuzitafutia ufumbuzi.
Mwanasheria wa Bodi ya Wataalamu
ya Ununuzi na Ugavi, Bw. Suleiman Mzava ambaye ni mmoja wa washiriki
wa kikao kazi hicho amesema, kikao kazi hicho kitasaidia kujenga uadilifu miongoni
mwa taasisi za umma hivyo ameipongeza Serikali kwa kuweka nguvu kubwa katika usimamizi
wa maadili.
Watumishiwa Umma wa wakizingatia
uzalendo, uadilifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, watatoa
huduma bora kwa wananchi na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.
Laurean Ndumbaro akifungua
kikao kazi cha ofisi yake na Taasisi zinazosimamia Maadili
na vyama vya kitaaluma chenye lengo la kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa
maadili, kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
Baadhi
ya washiriki wa kikao kazi cha Taasisi zinazosimamia Maadili na vyama vya
kitaaluma chenye lengo la kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa maadili wakimsikiliza
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani)
wakati akifungua kikao kazi hicho kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya
Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara
ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Leila Mavika (wa kwanza
kushoto) akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha ofisi
yake na Taasisi zinazosimamia Maadili na vyama vya kitaaluma chenye lengo la kubadilishana
uzoefu wa usimamizi wa maadili, kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI
Mtumba jijini Dodoma.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha Taasisi
zinazosimamia Maadili na vyama vya kitaaluma chenye lengo la kubadilishana
uzoefu wa usimamizi wa maadili mara baada ya kukufungua kikao kazi hicho,
kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment