Na. Veronica Mwafisi-DODOMA
Tarehe 19 Septemba, 2021.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael
amesema tangu watumishi wa ofisi yake waanze utaratibu wa kufanya mazoezi ya
pamoja mara moja kwa wiki yameongeza kasi ya watumishi kutekeleza majukumu yao
kwa ufanisi kutokana na afya zao kuimarika kupitia mazoezi hayo.
Dkt. Michael aliyasema hayo
jana wakati wa mazoezi ya watumishi wa ofisi yake yaliyoongozwa na Katibu Mkuu
wa ofisi hiyo, Dkt. Laurean Ndumbaro katika Ofisi zilizopo Mji wa Serikali
Mtumba, jijini Dodoma.
Kutokana na mazoezi
wanayofanya, watumishi wamekuwa familia moja hivyo wameongeza wigo wa ushirikiano
katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuimarisha kinga ya miili yao
dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, Dkt. Michael amefafanua.
Aliongeza kuwa, mazoezi yamewawezesha
watumishi wa ofisi yake kuwa na afya njema, kuipa mwili yao nguvu na afya ya
akili inayowawezesha kutekeleza majukumu yao bila uchovu wa aina yoyote.
Kutokana na faida hiyo
waliyoipata kupitia mazoezi, Dkt. Michael, amewahimiza watumishi wa ofisi yake
kuendelea kufanya mazoezi ili kuendelea kuimarisha afya zao kwa ajili ya kuongeza
ufanisi kiutendaji.
Akizungumzia faida waliyoipata
kupitia mazoezi, mmoja wa watumishi wa ofisi hiyo Bi. Elizabeth Fusi amesema,
mazoezi yamemsaidia sana kuimarisha afya yake na kuongeza kuwa amefurahia sana
mchezo wa kukimbiza kuku.
Nimekuwa
mshindi katika mchezo wa kukimbiza kuku na kupewa zawadi hivyo, naushukuru uongozi
wa ofisi yangu kwa kuhamasisha mazoezi kwa watumishi, mazoezi ambayo yamesaidia
kuongeza ufanisi kiutendaji, Bi. Fusi amefafanua.
Kwa
upande wake, mtumishi mwingine Bw. George Kapera amesema kuwa, mazoezi yanazidi
kuimarisha afya zao pamoja na utendaji kazi wao na kuongeza kuwa amefurahi
kucheza mchezo wa kukimbiza kuku pamoja na kukimbia na gunia.
Watumishi
wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa nyakati
tofauti wameushukuru uongozi wa ofisi yao kwa kuweka utaratibu endelevu
unaowapa fursa ya kufanya mazoezi ya pamoja kila Ijumaa ya wiki yenye lengo la
kuimarisha afya zao na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (Wa
kwanza kushoto) akishiriki
kufanya mazoezi ya viungo wakati wa mazoezi ya watumishi wa ofisi yake yaliyofanyika
katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Dkt. Francis Michael akisisitiza ufanyaji wa mazoezi kwa watumishi wa ofisi
yake wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali
Mtumba, jijini Dodoma.
Watumishi
wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya
mazoezi ya viungo ili kuimarisha afya zao wakati wa mazoezi ya watumishi wa
ofisi hiyo yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini
Dodoma.
Baadhi
ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
wakijiandaa kushindana kukimbia na magunia wakati wa mazoezi ya watumishi wa
ofisi hiyo yalifanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini
Dodoma.
Watumishi
wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya
mazoezi ya kuimarisha afya zao katika Ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba
Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment