Saturday, September 25, 2021

SERIKALI YAJA NA MWAROBAINI WA KUTATUA CHANGAMOTO YA KUHAMA KWA WATUMISHI WANAOAJIRIWA PEMBEZONI MWA NCHI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Rufiji

Tarehe 25 Septemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watumishi wanaofanya kazi za kujitolea maeneo ya pembezoni mwa nchi kuendelea kuwahudumia wananchi kwani Serikali itatoa kipaumbele cha ajira kwao ili kuondokana na changamoto ya kuajiri watumishi ambao baada ya muda mfupi wanaomba uhamisho.

Akiwa kwenye ziara yake ya kikazi Wilayani Rufiji, Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa watumishi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya katika maeneo ya pembezoni, hivyo watumishi wanaojitolea katika maeneo hayo watapewa kipaumbele cha ajira badala ya kuwaajiri wanaotoka maeneo mengine ambao pindi wakiajiriwa hawataki kukaa katika vituo walivyopangiwa kwa kisingizio cha uwepo wa mazingira magumu.

“Yapo maeneo ya kimkakati ambayo Serikali itahakikisha wanaojitolea katika maeneo hayo wanaajiriwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni msikivu kwa wananchi wake na ndio maana anaendelea kutoa ajira katika sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya ili wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotolewa katika sekta hizo.

Mhe. Mchengerwa amesema licha ya nchi ya Tanzania kuwa kubwa na yenye uhitaji mkubwa wa Watumishi wa Umma, Serikali itaendelea kutoa ajira ili kuboresha utumishi wa umma kwa maendeleo ya taifa.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwani kila Mtanzania anayo haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu miradi inayotekelezwa na Serikali kwa manufaa ya umma.

“Ni haki yenu kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yenu, mkiona haiendi sawa au kuna dalili zozote za rushwa toeni taarifa TAKUKURU kwa kupiga namba 113 ili hatua zichukuliwe dhidi ya wote wanaohusika,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi katika Mikoa ya pembezoni pamoja na kukabiliana na vitendo vya rushwa ambavyo ni kikwazo kwa maendeleo ya taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi na Watumishi wa Umma wa Kitongoji cha Tapika, Kata ya Ngarambe wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Rufiji.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishiriki zoezi la uwekaji wa nguzo za umeme Kata ya Ngarambe wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Rufiji.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi na Watumishi wa Umma Kata ya Utete wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Rufiji.


Sehemu ya umati wa wananchi na Watumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Rufiji.

 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisalimiana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Ngarambe wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Rufiji.


Mwalimu Monica Paul wa Shule ya Msingi Ngarambe akiwasilisha hoja ya masuala ya kiutumishi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa Wilayani Rufiji.

 

 

 

No comments:

Post a Comment