Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 07 Septemba, 2021
Serikali imetoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na
utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa kwa lengo la kuwawezesha wajumbe hao kushirikiana
na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na ulinzi wa rasilimali za umma.
Akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
amesema, Waheshimiwa wajumbe wa kamati hiyo watapata fursa ya kufahamu vema
makosa ya rushwa kama yanavyotamkwa katika Sheria Na. 11 ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa ya Mwaka 2007 na hatimaye kuwa na mchango mkubwa wa kutetea
mapendekezo ya maboresho ya sheria hiyo pindi itakapowasilishwa Bungeni.
“Ikumbukwe kuwa, tunayo sheria ya muda mrefu ya kuzuia na
kupambana na rushwa inayohitaji maboresho hivyo, naamini wajumbe wa kamati hii
kupitia elimu mtakayoipata mtatoa mchango mkubwa wa kuiboresha,” Mhe.
Mchengerwa amefafanua.
Ameongeza kuwa, ni wakati muafaka kwa wajumbe wa kamati
hiyo kuielewa vema Sheria hiyo Na. 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka
2007 na kuwa mabalozi wazuri kuhimiza maboresho yake ili iwe na manufaa katika
mapambano dhidi ya rushwa na ulinzi wa rasilimali za umma kwa ujumla.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo (Mb) amesema
kamati yake imehudhuria mafunzo hayo yenye lengo la kuwaelimisha namna ya
kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa ili nao waweze kuwa sehemu ya
mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Aidha, Mhe. Chaurembo ameongeza kuwa, Serikali inapeleka
fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwenye halmashauri, hivyo amemuomba Mhe.
Mchengerwa kuhakikisha TAKUKURU inaendelea kutoa mafunzo ya mapambano dhidi ya
rushwa katika halmashauri zote kwa lengo la kudhibiti mianya ya upotevu wa
fedha za umma zinazotolewa na Serikali ili kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo.
“Naomba halmashauri zote nchini zipatiwe mafunzo ya
kupambana na vitendo vya rushwa wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ili kuwezesha fedha za walipa kodi wa kitanzania kutumika vizuri,” Mhe.
Chaurembo amesisitiza.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi
Salum Hamduni amesema, semina hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa imelenga kubadilishana uzoefu, kutoa elimu ya
kupambana na rushwa na kutekeleza takwa la kisheria ambalo linaitaka TAKUKURU
kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu
mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
akitoa neno la utangulizi wakati wa Semina iliyoandaliwa na TAKUKURU kutoa
elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Takwimu jijini
Dodoma.
Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe.
Abdallah Chaurembo (Mb) akizungumza na wajumbe wa kamati yake kabla ya kuanza
kwa Semina iliyoandaliwa na TAKUKURU kwa lengo la kutoa elimu ya mapambano
dhidi ya rushwa iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa
Elimu kwa Umma TAKUKURU Mhandisi Dkt. Emmanuel Kiyabo akiwasilisha Mada ya
Wajibu wa Wabunge katika Mapambano dhidi ya Rushwa kwa wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa semina iliyofanyika
kwenye Ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.
Baadhi ya
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakisikiliza
Mada ya Wajibu wa Wabunge katika Mapambano dhidi ya Rushwa iliyowasilishwa kwao
na Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa TAKUKURU Mhandisi Dkt. Emmanuel Kiyabo
(hayupo pichani).
Mkurugenzi Mkuu
wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi Salum Hamduni akieleza majukumu ya taasisi yake
kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati
wa semina iliyotolewa na taasisi yake kwa wajumbe wa kamati hiyo yenye lengo la
kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa.
Mmoja wa
wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Magreth Sitta (Mb) akiwasilisha hoja kuhusu
mapambano dhidi ya rushwa wakati wa semina iliyotolewa na TAKUKURU kwa wajumbe
wa kamati hiyo yenye lengo la kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa zilizowasilishwa na wajumbe hao wakati wa Semina
iliyoandaliwa na TAKUKURU kwa ajili ya kutoa elimu ya mapambano dhidi ya
rushwa.
Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakiwa katika picha
ya pamoja na watendaji wa Ofisi ya Rais na TAKUKURU mara baada ya kumalizika
kwa semina iliyoandaliwa na TAKUKURU kwa lengo la kutoa elimu ya mapambano
dhidi ya rushwa kwa wajumbe wa kamati hiyo.
No comments:
Post a Comment