Na.
Veronica Mwafisi-RUFIJI na KILOSA
06 Septemba, 2021
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya kimkakati ambapo ikikamilika itatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.
Dkt. Ndumbaro aliyasema
hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi na watumishi wa ofisi yake wa kada
mbalimbali ya kutembelea miradi ya kimkakati ukiwemo Mradi wa Kufua Umeme kwa
Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) uliopo Wilayani Rufiji na Mradi wa
Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) uliopo Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Katika ziara hiyo,
Dkt. Ndumbaro amewasihi Watumishi wa Umma kufanya kazi kwa juhudi na kuendelea
kuiunga mkono serikali ya Awamu ya Sita ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa
haraka na kuwa na matokeo chanya.
“Niwaombe Watumishi
wa Umma muendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ikiwemo hii ya kimkakati ili ikamilike kwa wakati, hivyo kila mmoja wetu
afanye kazi kwa uadilifu, uzalendo na kwa juhudi ili iweze kuzaa matunda katika
kuleta maendeleo ya nchi yetu,” Dkt. Ndumbaro ameongeza.
Dkt. Ndumbaro
amesema ameamua kuambatana na watumishi wa kada mbalimbali wa ofisi yake ili
kuwa na uwakilishi mzuri wa watumishi wengine ambao hawakupata fursa ya
kushiriki katika kujionea juhudi zinazofanywa na Serikali katika miradi hiyo ya
kimkakati kwa lengo la kuwa mabalozi wazuri wa shughuli zinazofanywa na
serikali.
Naye Mkurugenzi
Rasilimaliwatu na Utawala (TRC), Bi. Amina Lumuli ameishukuru Serikali
inayoongozwa na Mhe. Rais Samia kwa mchango mkubwa wanaowapa katika kutekeleza
ujenzi wa mradi huo ambao mpaka sasa kipande cha kwanza kimefikia asilimia 98.
Bi. Lumuli
amemshukuru na kumpongeza Dkt. Laurean Ndumbaro kwa kuwapeleka watumishi wa
ofisi yake katika mradi hiyo ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo.
Bi. Lumuli
amemuomba Dkt. Ndumbaro, kuwapatia ushirikiano pale watakapotaka kuajiri
watumishi wenye taaluma mbalimbali pamoja na kuwapatia mafunzo watumishi hao
watakaokuwa wanaendesha reli hiyo ya kisasa.
Mmoja wa Watumishi
wa Ofisi ya Rais, Menejimemti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, walioshiriki
ziara hiyo, Bw. Humfrey Mbuma, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa
kwao kwani wamejionea jinsi miradi hiyo inavyotekelezwa kwa fedha za Watanzania
ambapo mradi wa JNHPP utapunguza au kumaliza tatizo la umeme nchini.
“Tunaishukuru na
kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia kwa kutekeleza mradi huu na
mingine mingi ya kimkakati, Watanzania tumefurahi, tutaendelea kumuunga mkono
kwa kuchapa kazi kama tunavyosema Kazi Iendelee,” amesema.
Kwa upande wao
Watumishi Josephine Manase na Maynesy Mollel wamemshukuru Dkt. Ndumbaro kwa
kuwapa fursa watumishi wa ofisi yake ya kutembelea miradi ya kimkakati na
kuahidi kuwa mabalozi wazuri katika kuelezea umuhimu wa utekelezaji wa miradi
hiyo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cosmas Ngangaji
amesema miradi hiyo ni mizuri sana kwa maslahi mapana ya nchi, hivyo hatuna
budi kuwapongeza waliowaza kuianzisha, walioidhinisha na walioanza utekelezaji
wake.
Katika ziara hiyo, kwa
upande wa JNHPP watumishi hao wametembelea ujenzi wa tuta kuu la kuzuia maji,
ujenzi wa handaki tatu za kupeleka maji kwenye mitambo zenye urefu wa mita 550
kila moja, ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha umeme ulioongezwa nguvu
kutoka kilovoti 15.7 hadi kilovoti 400 chenye urefu wa mita 400 pamoja na
ujenzi wa nyumba za makazi za kudumu za watumishi watakaokuwa wakiendesha mitambo pindi mradi huo
utakapokamilika pia wamefanikiwa kutembelea Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na
kujionea handaki lililopo chini ya mlima
ambalo reli hiyo ya kisasa itapita.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (Kushoto) akimsikiliza
Mkandarasi Mshauri Mhandisi John Mageni alipokuwa katika ziara ya kikazi na
watumishi wa ofisi yake ya kutembelea Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa
Julius Nyerere uliopo Wilayani Rufiji. Nyuma yake ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (wa kwanza kushoto toka
kwa Mhandisi Mageni aliyeshika kipaza sauti) akimsikiliza Mkandarasi Mshauri
Mhandisi John Mageni (aliyeshika kipaza sauti) alipokuwa akiwaonyesha ujenzi wa
tuta kuu la kuzuia maji wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo na
watumishi wa ofisi yake ya kutembelea Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa
Julius Nyerere uliopo Wilayani Rufiji. Wa kwanza kulia toka kwa Mhandisi Mageni
ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI Dkt. Francis Michael.
Baadhi
ya Watumishi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
wakielekea kutazama ujenzi wa jengo la mitambo (power house) ikiwa ni moja ya
Mradi wa Kufua Umeme kwa nguvu za maji wa Julius Nyerere wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea mradi
huo uliopo Wilayani Rufiji.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi
ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakitazama michoro ya
Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kabla ya kuingia kwenye handaki ambapo
reli hiyo imepita wakati wa ziara ya kikazi waliyoifanya Wilayani Kilosa Mkoani
Morogoro.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa ofisi yake wakati wa ziara ya
kikazi ya kutembelea Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) Wilayani Kilosa
mkoani Morogoro. Kulia kwake ni Mkurugenzi Rasilimaliwatu na Utawala (TRC) Bi.
Amina Lumuli na wengine ni wafanyakazi wa ujenzi wa mradi huo.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro
akipewa maelezo na Mkandarasi Mshauri Mhandisi John Mageni kuhusu vifaa
vilivyotumika kwenye reli hiyo iliyopita ndani ya handaki wakati wa ziara ya
kikazi ya kutembelea mradi huo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro. Wengine ni
watumishi wa ofisi yake aliombatana nao kwenye ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment