Na. James Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 30 Septemba, 2020.
Maafisa
Utumishi watakaozembea na kusababisha Watumishi wa Umma nchini kutolipwa
mishahara yao kwa wakati, watasimamishiwa mishahara na Serikali mpaka
watakapohakikisha watumishi hao wamelipwa mishahara yao.
Hayo
yamesemwa jana na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya
wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la
Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 140 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara,
Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara,
Kigoma na Tabora yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.
DKt.
Michael amesema, kuna tatizo katika baadhi ya Taasisi za Umma kwani wapo
Maafisa Utumishi wanajifanya miungu watu wakati wajibu wao ni kumtengenezea
mazingira mazuri ya kikazi mtumishi ili ajisikie yuko sehemu salama na aweze
kutekeleza ipasavyo jukumu la kuwahudumia wananchi.
“Msiwafanye
watumishi mnaowasimamia kuona sehemu ya kazi kama jehanamu, hivyo mbadilike
kwani Serikali haitomvumilia yeyote atakaye kinzana na azma yake ya kuboresha
huduma kwa wananchi”, Dkt. Michael alisisitiza.
Ameongeza
kuwa, ni lazima Maafisa Utumishi wabadilike kwa kuwajengea mazingira Watumishi
wa Umma kuipenda Serikali yao kwasababu inawajali na kuthamini mchango wao
katika maendeleo ya taifa.
Dkt.
Michael amefafanua kuwa, Serikali inamhakikishia mtumishi usalama wa ajira yake
tofauti na sekta binafsi, hivyo hakuna Afisa Utumishi atakayevumiliwa pindi akisababisha
Serikali kulaumiwa na Watumishi wa Umma au Wananchi.
Naye, Mkuu
wa Idara ya Utawala na Utumishi, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw. Boniface
B. Chatila kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameahidi kuwa, wakirejea
katika maeneo yao ya kazi watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu
ili kuondoa kero ya Watumishi wa Umma kufuata huduma Ofisi ya Rais Utumishi
Dodoma, huduma ambazo wanastahili kupewa katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, Bw.
Chatila amemhakikishia Dkt. Michael kuwa, ujuzi watakaoupata kupitia mafunzo ya
Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara watautumia
ipasavyo kuongeza ufanisi kiutendaji ili kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP
Ibrahim Mahumi amesema, suala la mtumishi kukosa mshahara hivi sasa
linachukuliwa kama ni kosa kubwa hivyo Afisa Utumishi atakayebainika
atasimamishiwa mshahara ikiwa ni hatua ya awali na atachukuliwa hatua za
kinidhamu ikizingatiwa kuwa, mfumo mpya utaonesha uzembe wa afisa huyo.
Mfumo Mpya
wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara utaanza kutumika rasmi
Mwezi Novemba, 2020 mara baada ya kukamilika kwa mafunzo ya makundi yote ya
Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala ambao ndio wenye jukumu la kuutumia mfumo
huo kiutendaji.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akizungumza na washiriki wa mafunzo ya
wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara
kwa kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 140 yanayofanyika
jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.
Baadhi
ya Washiriki wa mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za
Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala
140 wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika jijini
Dodoma katika Ukumbi wa VETA.
Mkurugenzi
wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi akitoa
ufafanuzi wa utekelezaji wa maelekezo ya Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael aliyoyatoa wakati
akifungua mafunzo ya kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Utawala 140 yanayofanyika
jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.
Mkuu
wa Idara ya Utawala na Utumishi, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw. Boniface
B. Chatila akiahidi kutekeleza maelekezo ya Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa niaba ya kundi la pili la washiriki 140 wa mafunzo ya Mfumo Mpya wa
Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara yanayofanyika jijini Dodoma
katika Ukumbi wa VETA.
No comments:
Post a Comment