Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 02 Septemba, 2020.
Watumishi wa Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) wapatiwa mafunzo
yatakayowawezesha kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na ufanisi ili kuboresha
utoaji huduma kwa umma na wadau wengine wa masuala ya kiutumishi na utawala
bora.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis
Michael wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa ofisi yake
yatakayotoa fursa ya kuwajengea uwezo kwenye eneo la uandishi wa nyaraka za
ofisi, utunzaji bora wa kumbukumbu na nyaraka, mapambano dhidi ya rushwa ikiwa
ni pamoja na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahala pa kazi.
Dkt. Michael amewaka
watumishi hao kufuatilia kwa umakini mafunzo hayo ili wapate elimu na weledi
kuhusu namna bora ya uandishi wa nyaraka, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka,
kuepuka vitendo vya rushwa na msongo wa mawazo ambavyo kwa kiasi kikubwa
vinaweza kuathiri utendaji kazi wao wa kila siku.
“Mafunzo haya ni muhimu
katika kuiwezesha ofisi kupata watumishi mahiri, waadilifu, wenye kuzingatia
weledi na ufanisi kiutendaji”, Dkt. Michael amesisitiza.
Dkt. Michael amefafanua
kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama
zilivyo taasisi nyingine nyeti, inapaswa kuwa na watumishi bora na wenye ujuzi
na maarifa yatakayowaongezea ufanisi kiutendaji na ndio maana menejimenti
imeamua kuwapatia mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kutoa huduma bora kwa
wananchi na wadau wengine.
Mafunzo haya ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa OR-MUUUB yanafanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia tarehe 02 hadi 04/09/2020 na yatahudhuriwa na watumishi 218.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akifungua mafunzo
ya siku tatu kwa watumishi wa ofisi yake (hawapo pichani) yenye lengo la
kuwajengea uwezo kiutendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau
wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.
Baadhi ya watumishi wa Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifurahia ufunguzi
wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uandishi wa nyaraka za ofisi, utunzaji wa
kumbukumbu na nyaraka, mapambano dhidi ya rushwa pamoja na namna bora ya
kukabiliana na msongo wa mawazo mahala pa kazi.
Mkurugenzi Msaidizi, Idara
ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Mwanaheri Cheyo akitoa neno la utangulizi kabla
ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa
ofisi hiyo yaliyoanza Septemba 2, 2020 katika Ukumbi wa UDOM na yatahitimishwa
Septemba 4, 2020.
No comments:
Post a Comment