Na
James Mwanamyoto- Dodoma
Tarehe 14 Septemba, 2020
Mfumo mpya wa Taarifa
Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) uliotengenezwa na wataalam wa
ndani una uwezo wa kuhifadhi taarifa muhimu za Watumishi wa Umma tangu
kuajiriwa kwao na utatatua changamoto nyingi za kiutumishi ikiwamo ya madai ya
muda mrefu ya malimbikizo ya mishahara.
Hayo yamesemwa leo na Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Dkt. Francis Michael wakati akifungua Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi
la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma,
Singida na Morogoro yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini
Dodoma.
Dkt. Michael amesema Mfumo
huo pamoja na kujumuisha taarifa zote muhimu zinazohusu maendeleo ya Mtumishi
wa Umma tangu aajiriwe hadi anapofikia ukomo wa ajira yake, pia unajumuisha
taratibu zote muhimu za kiutendaji katika Utumishi wa Umma.
“Tofauti na Mfumo wa Lawson unaotumika hivi sasa, Mfumo huu
mpya unahifadhi taarifa za Miundo ya Taasisi za Umma, Miundo ya Maendeleo ya
Utumishi, Miundo ya Mishahara ya Watumishi, Ikama na Bajeti, taarifa za Ajira
za Watumishi na matukio yote yanayowahusu, malipo ya mishahara yao, makato ya
marupurupu yao kwa kila mwezi na upandishwaji vyeo,” Dkt. Michael amefafanua.
Dkt. Michael ameainisha kuwa,
Mfumo mpya utaondoa changamoto ya madai ya malimbikizo ya mshahara ya muda
mrefu pindi Mtumishi anapopandishwa cheo, kwani mara baada ya kupanda cheo,
taarifa zake zitabadilishwa kwa wakati ikiwa ni pamoja na kupata mshahara mpya.
Naibu Katibu Mkuu huyo
amesisitiza kuwa, Mfumo huo uliotengenezwa na wataalam wa ndani wa Serikali,
unaakisi mahitaji ya ndani ya Serikali, utaimarisha usalama wa taarifa na
nyaraka pamoja na kupunguza gharama za matengenezo na ulipiaji leseni ambapo
Serikali ilikuwa ikitumia dola 217,000 kwa mwaka ambazo hivi sasa zitatumika katika miradi ya
maendeleo nchini.
Akizungumza kwa niaba ya
Washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Wilaya ya
Kondoa, Bw. Archanus Kilaja, ameipongeza Serikali kutengeneza Mfumo kwa kutumia
wataalam wa ndani, kitendo kinachoashiria nchi yetu imeanza kujitegemea kwenye
eneo la mifumo.
Bw. Kilaja ameahidi
kuyafanyia kazi mafunzo watakayoyapata ili watakaporejea kwenye maeneo yao ya
kazi waweze kuutumia mfumo vizuri kama Serikali ilivyokusudia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Bw. Priscus Kiwango amesema, Mafunzo yatakayotolewa kwa kundi la kwanza
la Maafisa Utumishi na Utawala, yamepewa muda mrefu wa wiki mbili kwani ndio
walengwa wakuu na watumiaji wa mfumo, muda huo utawawezesha kufahamu vizuri namna
mfumo unavyofanya kazi.
Bw, Kiwango ameongeza kuwa,
Mfumo mpya ambao utatumika badala ya Mfumo wa Lawson unaotumika hivi sasa, umeshafanyiwa majaribio, na Serikali
imejiridhisha kwamba uko tayari kwa ajili ya kuanza kufanya kazi rasmi na
utakuwa bora zaidi ya unaotumika sasa.
Maandalizi ya Mfumo Mpya wa
HCMIS ulianza mwaka 2018 kwa kukusanya mahitaji ya wadau kutoka kwenye taasisi
mbalimbali za Serikali, usanifu na ujenzi wa Mfumo ulianza mwaka 2019 na
kukamilika mwezi Juni, 2020.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael
akifungua Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha
Maafisa Utumishi Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro
yaliyofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo
ya Mfumo Mpya wa HCMIS kwa kundi la kwanza linalojumuisha Maafisa Utumishi
Utawala kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifungua
Mafunzo hayo leo kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa TEHAMA
Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw.
Priscus Kiwango akitoa neno la utangulizi kuhusiana na mafunzo ya Mfumo Mpya wa
HCMIS yaliyofunguliwa na Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt.
Francis Michael kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA Jijini Dodoma leo.
Mkuu wa Idara ya Utumishi na
Utawala, Wilaya ya Kondoa, Bw. Archanus Kilaja, akitoa neno la shukrani kwa
niaba ya Washiriki wa Mafunzo ya Mfumo Mpya wa HCMIS mara baada ya Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt.
Francis Michael kufungua Mafunzo leo kwenye ukumbi wa
mikutano wa VETA Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment