Na. James Mwanamyoto-Dodoma
25 Septemba, 2020
Katika kukabiliana na changamoto zinazohusiana na suala la usalama wa taarifa za Serikali na mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma kwa umma, Serikali imeziagiza Taasisi zote za Umma kuhakikisha zinatekeleza kikamilifu Sheria ya Serikali Mtandao namba 10 ya Mwaka 2019 na Kanuni zake ambayo imetungwa kwa lengo la kusimamia matumizi ya Serikali Mtandao.
Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Usimamizi
wa Rasilimaliwatu, ACP Ibrahim Mahumi kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifungua mafunzo
kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kuhusu umuhimu wa utekelezaji
wa Sheria ya Serikali Mtandao .
ACP Mahumi amesema, umakini katika suala zima la usalama
mitandaoni na kwenye mifumo unahitajika ili kuunga mkono jitihada za Serikali
kuboresha huduma kwa umma kwa njia ya Serikali Mtandao.
Ameongeza kuwa, kila Taasisi inalo jukumu la kuwaelimisha
watumishi wake ili wawe na uelewa wa pamoja wa namna ya kutekeleza Sheria ya
Serikali Mtandao pamoja na kanuni zake kwa lengo la kuepuka athari zitakazoweza
kujitokeza kwa kutokuzingatia sheria hiyo.
“Watu wa TEHAMA kazi yenu kubwa ni kurahisisha utendaji kazi
Serikalini hivyo, naamini mafunzo haya yatawasaidia kuhimiza utekelezaji wa
Sheria ya Serikali Mtandao na kufanya maboresho kwenye mifumo ya TEHAMA ya
utoaji huduma inayotumiwa na Taasisi zenu,” ACP Mahumi amesisitiza.
Kwa kuzingatia umuhimu wa utoaji huduma bora kwa umma, ACP Mahumi
ameziasa Taasisi za Serikali ambazo zinasuasua kutumia Serikali Mtandao
kuhakikisha zinatumia fursa ya uwepo wa Serikali Mtandao ili wananchi wanufaike
na huduma.
Sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 ya mwaka 2019 ilianza kutumika
rasmi tarehe 15 Disemba, 2019 baada ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambayo iliiwezesha iliyokuwa Wakala ya Serikali Mtandao
kuwa Mamlaka.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, ACP Ibrahim Mahumi akifungua mafunzo ya siku moja
kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao kwa Wakuu wa Idara
na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kwa niaba Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, yaliyofanyika leo jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki
wakimsikiliza Mkurugenzi
wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, ACP Ibrahim Mahumi (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa Sheria ya
Serikali Mtandao kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini yaliyofanyika
leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Bw. Priscus
Kiwango akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo ya siku moja kuhusu umuhimu wa
utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya
TEHAMA Serikalini yaliyofanyika leo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment