Na. Aaron Mrikaria-Dodoma
Tarehe 10 Septemba, 2020
Serikali imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma ambao utatoa maelekezo ya namna ya kujumuisha masuala ya kijinsia mahala pa kazi na kujenga mazingira bora na wezeshi kwa makundi mbalimbali kwenye taasisi za umma, ili mwongozo huo uwe ni chachu ya kuongeza tija kiutendaji kwa Watumishi wa Umma na Serikali kwa ujumla.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis
Michael wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kilichohudhuriwa na Wakurugenzi
wa Wizara zote kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha rasimu hiyo, kikao
hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini
DODOMA.
Dkt. Michael amewasititiza waajiri
kuwa, pendekezo la urithishanaji
madaraka kuzingatia suala la kijinsia lipewe umuhimu mkubwa katika utekelezaji
wake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawake wanapata fursa kujumuishwa kwenye
mipango ya mafunzo ili kujengewa uwezo kiutendaji.
Licha ya kuafiki pendekezo la
kutilia mkazo haja ya wanawake kupewa kipaumbele katika nafasi za uongozi na kuwekewa
mazingira wezeshi katika utekelezaji wa majukumu yao mahala pa kazi, Dkt.
Michael pia amehimiza umuhimu wa rasimu hiyo kuyawezesha makundi yote kutekeleza
wajibu wao kwa ufanisi katika Utumishi wa Umma.
Aidha,
Dkt. Michael awetaka viongozi katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanabaini
watumishi wenye vipaji maalum kutoka makundi anuai na kuviendeleza vipaji
hivyo, pamoja na kuangalia namna ya kuanzisha vituo vya malezi kwa watoto
katika majengo ya Ofisi za Umma ili mtumishi anayenyonyesha aweze kutumia muda
wake kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya kikazi.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi Anuai za
Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila
Mavika, amesema tofauti na Mwongozo wa mwaka 2010, rasimu hii inayoboreshwa
imezingatia masuala ya jinsia na usimamizi wa rasilimaliwatu, hivyo muongozo
huu ukiidhinishwa rasmi kutumika utakuwa ni mahususi kuratibu ujumuishwaji wa masuala
ya jinsia katika usimamizi wa rasilimaliwatu kwenye Utumishi wa Umma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akizungumza na washiriki wa kikao kazi cha
siku mbili kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha Rasimu ya Mwongozo
wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma, kabla ya kufunga
rasmi kikao kazi hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa jijini DODOMA jana jioni.
Mmoja wa washiriki
(aliyesimama) wa kikao kazi cha siku mbili
kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa
Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma akitoa mchango wake
katika kikao kazi hicho, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu
na Nyaraka za Taifa jijini DODOMA jana jioni.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa
kikao kazi cha siku mbili kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha Rasimu
ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma, mara
baada ya kufunga rasmi kikao kazi hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo
cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini DODOMA jana jioni.
No comments:
Post a Comment