Na. Mwandishi Wetu
Septemba 5, 2024
“Tuwawajibishe au kuachana na
watumishi wasiokuwa waadilifu kwa kuwa sisi ndio tunaotakiwa kusimamia uadilifu
lakini miongoni mwetu tunakuwa na watu wasiokuwa waadilifu”
Maneno hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu wakati akiongea
na viongozi na watumishi wa TAKUKURU makao makuu Dodoma.
Amewakumbusha Viongozi na watumishi hao kuwa suala la
uadilifu limeandikwa hata katika vitabu vya dini zote ambapo likizingatiwa kwa
usahihi amani na utulivu hutamalaki miongoni mwa wananchi.
Alisema, TAKUKURU ni taasisi muhimu na nyeti katika
taifa la Tanzania na msingi wake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lengo
ikiwa ni kuzuia na kupambana na rushwa katika jamii. Hivyo, Viongozi na
watumishi wote wa Umma wakiongozwa na TAKUKURU hawanabudi kumuunga mkono Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mapambano hayo.
Mhe. Sangu ametoa rai kwa TAKUKURU kuangalia kwa kwa
makini eneo la Ununuzi wa Umma ambapo zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya
Serikali inaelekezwa katika eneo hilo. Hivyo, eneo hilo lazima litazamwe na kupewa
kipaumbele ili kuziba mianya ya rushwa.
Aliongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepeleka fedha nyingi kwenye miradi ya
maendeleo Tanzania nzima, hivyo ameielekeza TAKUKURU kufuatilia na kusimamia
vyema miradi hiyo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa mujibu wa mikataba.
Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu Bw. Mululi
Majula Mahendeka amesema TAKUKURU ni muhimu kwa usalama wa nchi hasa katika
kuzuia na kupambana na rushwa.
“Rushwa ikishamili na usalama wa nchi unateteleka kwa
kuwa wananchi wanakosa imani na Serikali yao, hivyo ametoa wito
kwa watumishi hao kufanya kazi kwa juhudu na maarifa ili Serikali iendelee
kuiaminika kwa umma” alisisitiza Bw. Mahendeka.
Alibainisha kuwa, usiri na utengano sambamba ni jambo
la msingi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na mambo hayo
yasipozingatiwa na kutiliwa mkazo yanaweza kubomoa msingi wa umoja wa Taifa
ambao uliwekwa na unaendelea kusimamiwa vyema na Viongozi wetu wakuu.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin
Chalamila alimuahidi Mhe. Sangu kupata ushirikiano wa dhati kutoka kwa Viongozi
na Watumishi wa TAKUKURU ili kutekeleza majukumu aliyopewa kwa ufanisi.
Pia, alimuomba Mhe. Sangu kufikisha salaamu za
shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akizungumza
na Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyofanyika jijini
Dodoma.
Baadhi ya Watendaji na Watumishi na wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila akielezea utekelezaji wa
majukumu ya ofisi hiyo
kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu (hayupo
pichani) wakati
wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo
iliyofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila
(hayupo pichani) wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya
ofisi hiyo alipofanya
ziara ya kikazi. Kulia ni Katibu Mkuu-IKULU, Bw. Mululi Majula
Mahendeka.
Baadhi ya Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akipokea baadhi ya vitendea kazi vya Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati alipofanya ziara ya kikazi
katika ofisi hiyo jijini Dodoma kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu
na kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akisalimiana na baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati alipowasili katika ofisi hiyo kwa ziara ya kikazi jijini
Dodoma.
Kwaya ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
ikitoa elimu kupitia nyimbo wakati Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus
Sangu alipofanya ziara katika ofisi hiyo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa
majukumu na kuhimiza uwajibikaji.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus
Sangu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) baada ya kuhitimisha ziara
yake ya kikazi katika ofisi hiyo iliyopo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment