Monday, September 16, 2024

MHE. SIMBACHAWENE AWAASA WAHITIMU KUSHIKA ELIMU KWA UJENZI WA TAIFA ENDELEVU.

 Na. Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewaasa wahitimu wa darasa la Saba kushika elimu kwa kuwa elimu ni msingi wa maisha na inajenga taifa endelevu.

Mhe. Simbachawene alisema kuwa, Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua umuhimu wa elimu kwa taifa, hivyo, amewekeza zaidi katika elimu ikiwa ni jitihada za kuendelea kupambana na maadui watatu wa Taifa ambao ni ujinga, umasikini na maradhi.

Aidha, aliwakumbusha kuwa msomi ni mtu yeyote ambaye amefuta ujinga, anaweza kusoma na kuandika na kutanzua mambo yanayomkabili, hivyo elimu ni muhimu na ndiyo mana Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

“Ninawasihi musome kwa bidii ili msije mkajuta hapo baadae katika maisha yenu, ukiwa na elimu utaishi maisha ya kufuata Sheria za nchi, utaheshimu watu, utakuwa na hekima na busara ya kutawala maisha yanayokuzunguka” alisistiza Mhe. Simbachawene.

Katika hotuba yake kwa wahitimu hao wa darasa la saba kwenye Mahafali ya 60 ya Shule ya Msingi Kaloleni iliyopo Kata ya Majengo Jijini Dodoma, Mhe. Simbachawene aliwataka wahitimu hao kutokatishwa tamaa na watu wasiopenda elimu kwa kuwa elimu ni msingi wa utendaji kazi na maendeleo.

Pia, alisema watu wengi wanapotosha sana dhana ya elimu na hivyo kuwakatisha tamaa vijana kuendelea na masomo. Alifafanua kuwa hakuna uhusiano kati ya kusoma na kuwa na pesa, hata wasiosoma wana haki ya kuwa na pesa, suala la maisha mazuri ni bahati na mipango ya mtu binafsi, hakuna uhusiano na elimu.

“Ukiwa na elimu unaweza kuwa na njia bora za kwenda kwenye maisha mazuri kwa sababu anaweza kufanya uamuzi kwa usahihi kuliko yule ambaye hajasoma na wenye pesa wanatumia wasomi kupata pesa zaidi hususani katika masuala ya uvuvi, kilimo, ufugaji na biashara kwa jumla” aliongeza Mhe. Simbachawene.

Vilevile, amewapongeza walimu wote Tanzania kwa kufanya kazi vyema ya kufundisha vema na ameahidi kusimamia na kuangalia maslahi ya walimu hao kwa kuwa wanafanya kazi kubwa sana ya kujenga taifa la kesho.

Katika risala  ya wahitimu ilibainisha kuwa, shule ya msingi Kaloleni inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, ilianzishwa mwaka 1958 ina walimu 18 kati yao wakiume 5 wakike 13. Idadi ya wanafunzi ni 845 wavulana 441 wasichana 404. Hivyo, jumla ya wanafunzi 104 wamehitimu darasa la Saba ikiwa wavulana 48 na wasichana 56.

Hali kadhalika, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Emmanuel S. Enock alimshukuru Waziri Mhe. George Simbachawene kwa kujumuika na familia ya Kaloleni kwenye mahafali ya 60 licha ya kuwa na majukumu mengi ya kijamii na kitaifa.

Mwl. Emmanuel aliongeza kuwa Shule ya Msingi Kaloleni ni eneo salama kwa malezi ya watoto, kwani inaandaa watoto vyema kinadharia na kivitendo kutokana na umahiri mkubwa wa walimu wenye uwezo wa kufundisha, moyo wa upendo, huruma na uchu wa kuelimisha watoto ili kupata taifa imara na lenye wasomi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akizungumza na Wahitimu wa Darasa la Saba na Wazazi (hawapo pichani) wakati wa Mahafali ya 60 ya Shule ya Msingi Kaloleni Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kaloleni wakifuatilia matukio ya Mahafali ya 60 ya Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Kaloleni Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akimkabidhi cheti na zawadi mmoja wa Wahitimu wa Darasa la Saba wakati wa Mahafali ya 60 ya Shule ya Msingi Kaloleni Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wazazi wakifuatilia matukio kwenye Mahafali ya 60 ya Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Kaloleni Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Darasa la Saba wa Shule ya Msingi Kaloleni wakati wa Mahafali ya 60 ya Shule ya Msingi Kaloleni Jijini Dodoma.








No comments:

Post a Comment