Serikali itawaondoa katika
orodha ya malipo ya Serikali Katibu Tawala na Wakurugenzi wa Mamlaka za
Serikali za Mitaa watakaoshindwa kusimamia kwa weledi zoezi la kuondoa taarifa zisizotakiwa
(chafu) katika Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) kabla ya
mwisho wa mwezi Desemba 2015.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Tixon Nzunda ametoa maelekezo hayo
katika kikao kazi kilichoendeshwa kwa njia ya Video (Video Conference) iliyokutanisha
kwa pamoja mikoa kumi na mbili (12) ambayo ni Arusha, Kagera, Tanga, Tabora, Manyara,
katavi, kilimanajaro, Simiyu, Dar es salaam, Rukwa, Mwanza na Mbeya.
Bw. Nzunda katika kikao
hicho alisema ni jukumu la waajiri kuhakikisha usimamizi wa rasilimaliwatu ni
mzuri ili kuepuka malalamiko miongoni mwa Watumishi na kuwezesha wananchi kupokea
huduma kwa kiwango kinachotakiwa kutoka Serikalini.
“Mamlaka ambayo itashindwa
kusafisha takwimu chafu watendaji na wahusika wote wataondolewa katika orodha
ya malipo kwa sababu watakuwa wameshindwa kutimiza wajibu wao” Bw. Nzunda
alisema na kusisitiza kuwa zoezi hilo lifanyike kabla ya mwisho wa mwezi
Desemba 2015.
Kaimu Katibu Mkuu Bw. Nzunda
alisema ni jambo la msingi kuzingatia misingi ya weledi, uwajibikaji na utalaamu
katika kutekeleza majukumu na kutoa tahadhari kwa Maafisi Utumishi
wasiowajibika kuchukulia hatua stahiki.
Maelekezo mengine
yaliyotolewa kwa Watendaji Wakuu wote wa Serikali ni kuhakikisha kila mtumishi anafika
mahala pa kazi saa moja na nusu asubuhi (01:30) na kusaini kitabu muda wa
kufika na kutoka.
Watumishi wa Umma kuwa na
kitambulisho chenye jina na cheo husika na huduma zinazotolewa ziwe zenye tija
na kutolewa kwa wakati. Pamoja na hilo, Ofisi za malalamiko zifanye kazi na
kuanzisha dawati la kuwasikiliza wateja.
Vitengo vya Habari Serikalini
viimarishwe ili Umma uhabarishwe ipasavyo na kwa wakati kuhusu kazi mbalimbali
na huduma zinazotolewa na Serikali.
Watumishi wote wa Umma
waweke Ahadi ya Uadilifu kwa Umma wakati wa Wiki ya Uadilifu. Fomu ya kuweka
Ahadi ya Uadilifu inapatikana katika Tovuti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma yenye anuani www.utumishi.go.tz
. Ofisi ya Rais-Utumishi itafuatilia utekelezaji wa kiapo hicho.
Pamoja na maelekezo hayo, Bw.
Nzunda alifafanua kuhusu mafunzo ndani na nje ya nchi kuwa maagizo yaliyotolewa
yanapotoshwa na kusisitiza kuwa safari na mafunzo yenye masilahi kwa nchi
yanaruhusiwa kwa kibali kuombwa kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma.
Katibu Mkuu Bw. Nzunda alisisitiza
suala la nidhamu katika utendaji kazi na pale inapokiukwa hatua stahiki za
kinidhamu zichukuliwe mara moja kwa Watumishi wasiotaka kutumiza wajibu wao.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Kny: Katibu Mkuu-Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma
No comments:
Post a Comment